Andabwile afichua jambo Yanga | Mwanaspoti

Andabwile aliyewahi kutamba ndani ya Mbeya City na Singida Fountain Gate, kwa sasa anakipiga Yanga ukiwa ni msimu wake wa pili huku akianza vizuri 2025-2026 akiwa na uhakika wa namba kufuatia kuaminiwa na benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Romain Folz.

Akizungumza jijini Mbeya wakati Yanga ikijiandaa kuikabili Mbeya City hapo kesho katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Andabwile amesema kujituma na kushirikiana na wenzake kikosini ndio siri ya yeye kung’ara akiahidi kuwa bado wanahitaji kufanya vizuri kwenye mechi zao.

Amesema mafanikio yake yanatokana na muunganiko na timu kwa ujumla ikiwamo kufuata maelekezo ya kocha kuhakikisha anachoelekeza kinafanyika kwa faida ya Yanga.

NGET 01


“Kikubwa ni kutimiza majukumu yangu, lakini sifanyi peke yangu bali kwa ushirikiano wa wenzangu, kufuata maelekezo ya kocha kuhakikisha Yanga inafanya vizuri, kiu ya kila mmoja ni kutoa mchango wake,” amesema Andabwile.

Amesema matarajio yake ni kuendeleza kiwango kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye mashindano yote na kuendeleza kipaji akitamba kuwa kila mchezo kwao ni vita ya kutafuta pointi tatu.

Katika mechi nne za mashindano ilizocheza Yanga msimu huu, nyota huyo amecheza tatu kwa dakika zote tisini, huku moja pekee dhidi ya Pamba Jiji akitokea benchi wakati timu hiyo ikishinda mabao 3-0.

NGET 02


Yanga ilianza dhidi ya watani zao wa jadi Simba na kushinda bao 1-0, ikaifuata Wiliete nchini Angola katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda 3-0. Mechi hizi zote Andabwile alicheza dakika tisini sambamba na ile ya marudiano dhidi ya Wiliete iliyochezwa Septemba 27, 2025 na kushinda 2-0. Kabla ya hapo, Yanga iliilaza Pamba Jiji mabao 3-0.

Kiungo huyo katika mechi hizo amefunga mabao mawili yote dhidi ya Wiliete akianza ugenini na kumalizia nyumbani, huku akiwakuna mashabiki kwa kuupiga mwingi katika mechi zote.

NGET 03


Msimu uliopita Andabwile hakuwa na nafasi kubwa ya kucheza kwenye kikosi cha Yanga kilichofundishwa na makocha watatu tofauti akianza Miguel Gamondi, kisha Sead Ramovic na kumalizia Miloud Hamdi.

Kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, Andabwile alicheza mechi tano pekee kwa dakika 125, hakufunga wala kuasisti.