Wafugaji Monduli kulipa ada ya kusomesha watoto kwa ng’ombe

Monduli. Wafugaji wa jamii ya Kimasai katika Wilaya ya Monduli mkoani Arusha imebuni njia ya kipekee ya kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya mitaala ya Kiingereza, kwa kutoa mifugo kulipa ada ya shule, badala ya fedha taslimu kama ilivyozoeleka katika shule nyingi nchini.

Lengo kubwa la mpango huo ni kuongeza idadi ya watoto wa jamii hiyo shuleni lakini pia kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyowazuia kupata elimu bora kutoka shule binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika tamasha la utamaduni wa jamii ya Kimasai, Mkurugenzi wa Jukwaa la Mtandao Tanzania (TPN), Edward Malecela amesema wamebuni mbinu hiyo ili kuongeza kiwango cha ushiriki wa watoto wa jamii hiyo katika elimu, hususan wasichana.

Amesema mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya shule za binafsi wazazi na viongozi wa kijamii wa Kimasai, kama daraja la kuaminiana kati ya mfumo wa jadi wa maisha ya kifugaji na mahitaji ya kisasa ya elimu.

“Jamii ya kifugaji wana mifugo mingi lakini linapokuja suala la ada ya watoto wao wanasema hawana hela, hivyo sisi kama jukwaa la kutoa elimu tumeamua kuwahamasisha baadhi ya shule binafsi zilizoko katika jamii hizi kupokea mifugo badala ya ada,” amesema.

Amesema kuwa wameanza mazungumzo na shule zote zilizoko katika jamii hiyo na miongoni mwazo zimekubali.

“Hii itasaidia kuongeza idadi ya watoto shuleni lakini itaokoa wasichana wengi ambao wamekuwa katika hatari kubwa ya ndoa za utotoni kutokana na kukaa nyumbani kisa hakuna fedha ya shule,” amesema.

Amesema mpango huo unakwenda sambamba pia na michango midogomidogo ya shule ambayo italipwa kwa kutumia kuku au mbuzi kwa kuthaminishwa.

Mkurugenzi wa Shule ya Oola Academy, (moja ya shule zinazotekeleza mpango huo), Samwel Oola, amesema kwa kushirikiana na TPN wamepokea wanafunzi wengi ambao wanalipa ada zao kwa mifugo.

Amesema mpango huo umeibua miradi ya ufugaji shuleni hapo na kuvutia wanafunzi wengi zaidi ambao wanapenda mifugo kubaki shule kwa kujiona wako mazingira kama ya nyumbani na sehemu salama kuishi.

“Kulipa kwa ng’ombe unatoa fursa kwa wazazi ambao mara nyingi hawana fedha taslimu lakini wanamiliki mifugo, hivyo huleta na inathaminishwa kisha thamani yake inahesabiwa kama ada ya mtoto kwa muhula husika na kupewa risiti halali kwa malipo ya ada.

“Hii imekuwa mkombozi mkubwa kwa familia ambazo awali zilishindwa kupeleka watoto shule, lakini pia imeibua miradi ya ufugaji shuleni ambayo tunatumia kama somo la mtaala wa amali kwa kunenepesha wale mifugo kwa njia za kisasa na salama, kisha kuuza kwa bei kubwa na kuongeza mapato ya shule,” amesema.

Amesema wakati Serikali ikihamasisha elimu ya amali shuleni wameweza kufundisha watoto wao ufugaji wa kisasa na sasa wanaohitimu wanamiliki miradi yao ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na hata kuku na kuanza kujipatia kipato baada ya kuhitimu huku wakisubiri matokeo ya ngazi nyingine ya elimu.

Mmoja wa wazazi walionufaika na mpango huo, Amani Meshuko Laiboni amesema ubunifu huo umewafanya kupata hamasa na kuona  ni rahisi kusomesha watoto.

“Hii itasaidia sana mbali na  kupunguza ndoa za utotoni kwa wasichana wa Kimasai, pia imeleta hamasa kwa kuwa wazazi sasa wanaona thamani kubwa zaidi ya kumpeleka mtoto shuleni kwa mfano wa waliofanikiwa badala ya kumuozesha mapema kwa mahari ya ng’ombe,” amesema.

Naserian Saitoti amesema wakati wao waliolewa wako baadhi ya wenzao walipelekwa shule na sasa wamekuwa watu wa kuigwa katika jamii kutokana na mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia elimu huku wengine wakiwa sauti yao waliokimbilia ndoa.

 “Tulizoea kuona ng’ombe kama kila kitu, lakini sasa tunagundua elimu ndiyo urithi bora kwa watoto wetu. Kwa kumpeleka shule, tunavuna faida kubwa zaidi ya maisha yake ya baadaye,” amesema Saitoti.

Mmoja ya wanafunzi wa Shule ya Oola Academy, Agness Samweli amewashukuru wadau wote waliowezesha mpango huo ulimfanikisha kuishi na kupata elimu bora na kuepukana na changamoto za kijinsia.

“Mimi nasoma hapa mwaka wa sita nikiwa naishi shuleni, nishukuru wadau waliofanikisha hilo na kusaidia watoto wengi hasa wasichana ambao tuko hapa tunasoma kwa uhuru, amani na utulivu mbali na changamoto za kijinsia ambazo tungekutana nazo mitaani,” amesema.

Mmoja wa wazazi, Lesikar Mollel amesema utaratibu huo unachukuliwa kama kielelezo cha jinsi suluhu za kijamii zinazoheshimu mila na tamaduni zinavyoweza kuleta mabadiliko ya kweli.

“Elimu kupitia ‘ng’ombe badala ya fedha’ si tu kwamba imeongeza ushirikiano wa jamii na shule, bali pia imeweka msingi wa mustakabali bora wa watoto wa Kimasai, hivyo ikibidi wamiliki wote wa shule binafsi katika jamii hizi ziige mfano huu uliotusaidia sisi Monduli,” amesema.