Hungary kufadhili mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Biharamulo

Dar es Salaam. Serikali ya Hungary inafadhili mradi mkubwa wa maji safi ya kunywa kutoka Ziwa Victoria hadi Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera ili kuwapatia wananchi wa eneo hilo maji safi na salama.

Mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 55 milioni (sawa na Sh134.75 bilioni), utatekelezwa na kampuni kutoka Hungary, ukihusisha kusafirisha maji umbali wa kilomita 40 pamoja na kuyasafisha maji hayo kabla ya kuwafikia wananchi.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 29, 2025 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo baada ya kufanya mazungumzo na mgeni wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary, Peter Szijjártó ambaye yuko nchini kwa mwaliko wake.

Kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari, wawili hao walikuwa na mazungumzo ya faragha ambapo walijadiliana mambo tofauti kuhusu ushirikiano baina ya Serikali zao pamoja na ushirikiano wa sekta binafsi za pande zote mbili.

Balozi Kombo amesema wamejadiliana kuhusu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Biharamulo utakaowawezesha wananchi zaidi ya 200,000 kupata maji safi na salama kupitia teknolojia ya Hungary.

“Wenzetu wa Hungary wana teknolojia kubwa, kwa hiyo watatumia teknolojia yao ya kusafisha maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya watu wetu. Tuko katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji katika mradi huu,” amesema Balozi Kombo.

Wakati huohuo, Balozi Kombo amesema Hungary imefungua ubalozi wake uliofungwa miaka kadhaa nyuma, hivyo kuhamisha shughuli zake zilizokuwa zikifanyikia Nairobi, Kenya. Hivyo, Hungary inaungana na nchi nyingine zaidi ya 100 zilizo na balozi zao hapa nchini.

Vilevile, amesema wamejadiliana kuimarisha ushirikiano wa biashara baina yao ambapo sasa urari wa biashara umefikia dola 2.8 bilioni. Wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi baina yao.

Kwa upande wake, Szijjártó amesema changamoto kubwa inayozikabili nchi za Afrika ni kufikisha huduma ya maji kwa wananchi ambao idadi yao inaongezeka kila siku. Kwa kutambua hilo, amesema Hungary inafanya kazi ya kusaidia kufikisha maji safi kwa wananchi kupitia teknolojia yake.

Amesema kampuni za Hungary zina teknolojia ya juu ya kusafisha maji kwa ajili ya kunywa, hivyo zitahusika katika mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Biharamulo wenye thamani ya Dola 55 milioni.

“Teknolojia ya Hungary itatumika kusafirisha maji umbali wa kilomita 40, kampuni za Hungary zitafanya kazi hiyo, zitajenga matanki ya maji na kuyasafisha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Vicent Minja amesema wanashirikiana na kampuni za Hungary kwenye masuala ya teknolojia, hivyo wametiliana saini makubaliano kwenye masuala ya teknolojia hasa akili mnemba.

“Hawa wenzetu wana uwezo mkubwa katika kutengeneza programu za kilimo za kutumia akili bandia na hii ni mwendelezo wa MoU nyingi ambazo tunasaini kwa kuwasaidia wafanyabiashara wa Tanzania.

“Kwa hiyo tunajaribu kuwaleta hawa hapa Tanzania ili kilimo chetu kibadilike kiwe chenye teknolojia. Tumesaini MoU nyingi sana, hii inatokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuifungua nchi, hivyo tunapokea wageni wengi sana ambao tunashirikiana,” amesema.