Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
Nyaraka hizo ni Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, taarifa za benki na tamko la mali za chama kuanzia mwaka 2019 hadi 2024.
Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Hamidu Mwanga wakati kesi namba 8323/2025 ilipoitwa kwa ajili ya uamuzi mdogo.
Katika kesi hiyo Walalamikaji ni Said Issa Mohamed, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, wakijitambulisha kama wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema Zanzibar wakilishwa na mawakili Alvan Fidelis, Dido Simfukwe na Fabian Joseph, huku upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na mawakili Hekima Mwasipu na Dk Rugemeleza Nshala.
Walalamikaji wanadai kuwa Katiba ya chama na Sheria ya Vyama vya Siasa zimekiukwa, hususani kwenye mgawanyo wa rasilimali kati ya Bara na Zanzibar.
Katika uamuzi wa mahakama Jaji Mwanga alisema sheria inaruhusu upande wa pili kuwasilisha nyaraka zilizoombwa iwapo zitathibitishwa na kutumika kusaidia mwenendo wa shauri hilo
“Kwa hali hiyo, natoa siku 14 nyaraka hizo ziwasilishwe Mahakamani na upande wa pili wapewe, kisha zipitiwe ndani ya siku 19 za kazi, yaani hadi Oktoba 24, mwaka huu. Baada ya hapo tutakutana kusikiliza mapingamizi yaliyowasilishwa na walalamikiwa,” alisema Jaji Mwanga.
Hata hivyo, alibainisha kuwa nyaraka za mihutasari ya vikao haziwezi kutolewa kwa kuwa mlalamikaji hakutaja tarehe mahsusi za vikao anavyohitaji, na pia baadhi ni siri za chama.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Oktoba 30, mwaka huu.
Awali, wakili wa walalamikaji Alvan Fidelis alidai nyaraka hizo zina umuhimu mkubwa kwa shauri, kwani ndizo zitakazoonyesha iwapo rasilimali za chama ziligawanywa sawa kati ya Bara na Zanzibar.
“Nyaraka ziko mikononi mwa wajibu maombi. Hawajakataa kuwa nazo, bali wamedai kuna amri ya zuio. Lakini zuio hilo ni la kuzitumia, si kuziwasilisha,” alisisitiza.
Kwa upande wao, wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu, alidai maombi hayo hayana mashiko kwa sababu nyaraka za kumbukumbu za vikao vya Kamati Kuu hazina uhusiano na kesi ya msingi.
Alidai walalamikaji walipaswa kubainisha ni kikao kipi kilijadili suala linalohusu mgogoro wao. Pia alidai kuwa nyaraka hizo zinaweza kupatikana kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa iwapo Mahakama itaagiza.
Naye Dk Nshala alidai baadhi ya walalamikaji hawana viapo vinavyowaruhusu kuendelea na maombi hayo, huku akidai kuwa Said Mohamed si kiongozi tena wa Chadema baada ya uchaguzi wa Januari 21, 2025, na hivyo kujitambulisha kama kiongozi mwandamizi ni upotoshaji.