SERIKALI YAZINDUA MAFUNZO YA NDANI YA NCHI KWA WATAALAM WA MAWASILIANO VIJIJINI

Na Karama Kenyunko, Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezindua rasmi Mafunzo ya Ndani ya Nchi kwa wataalamu wanaosimamia Mradi wa Mawasiliano Vijijini (Tanzania Mobile Network for Rural Coverage Project – TMN4RCP).

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo, Septemba 29, 2025.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Salome Kessy amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, mjini au kijijini, anapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano ya simu, intaneti, na usikivu wa redio kupitia TBC Taifa.

“Katika dunia ya sasa inayosukumwa na kasi ya maendeleo ya kidijitali, hakuna taifa linaloweza kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi bila mifumo thabiti ya mawasiliano. Mradi wa Mawasiliano Vijijini ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira hii, na unakusudia kuwafikishia wananchi wote huduma bora za mawasiliano,” amesema.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwajengea wataalamu uwezo wa kusimamia miradi ya TEHAMA vijijini kwa weledi. Mafunzo yanahusisha usimamizi na uboreshaji wa mitandao ya simu vijijini (2G na 4G), teknolojia za LTE, uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano (Core Network), pamoja na mbinu za kushughulikia changamoto za sauti, intaneti na malipo ya simu vijijini.

Ameishukuru taasisi washirika TTCL, TBC na UCSAF kwa mchango wao katika utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kuwa jukumu la wataalamu hao ni sehemu ya mageuzi makubwa ya mawasiliano nchini.

Kwa upande wake, Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa wizara hiyo, alisema mradi huo umebuniwa na Serikali ili kuhakikisha maeneo yote ya Tanzania yanapata mawasiliano na usikivu wa redio.

“Kwa sasa, usikivu wa mawasiliano unafikia asilimia 75 pekee ya eneo lote la kijiografia la nchi. Kuna maeneo mengi hayana kabisa mawasiliano wala usikivu wa redio, ndiyo maana Serikali imekuja na mradi huu,” amesema.

Amesema kuwa mradi huo ni wa miaka miwili, ulioanza kutekelezwa Desemba 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Munaku, mradi unahusisha ujenzi wa minara 636, kati ya hiyo 621 kwa ajili ya mawasiliano ya simu ambayo itaendeshwa na TTCL na makampuni mengine ya simu, huku 15 ikiwa ni ya redio itakayoendeshwa na TBC.

Amesema Serikali iliona umuhimu wa mafunzo kwa wataalamu wa ndani kwa kuwa mitambo hiyo inajengwa kwa teknolojia ya kisasa, na hivyo wataalamu 140 kutoka TBC na TTCL wanashiriki mafunzo hayo.

Aidha, kabla ya mafunzo haya ya ndani, wataalamu 72 kutoka mashirika mbalimbali walihudhuria mafunzo nchini China kati ya Februari na Juni mwaka huu.

Kwa upande wake, Kelvin Mwakaleke, Meneja wa Mradi huo, amesema Serikali ilisaini mkataba wa utekelezaji na Mkandarasi China Technical Import and Export Corporation (CNTIC) Oktoba 23, 2023 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 108.5, mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya China.

Utekelezaji wa mradi huo wa miezi 24 umeshaanza, ambapo hadi kufikia Septemba 29, 2025 umekamilika kwa asilimia 56. Kati ya minara 621 ya simu, upembuzi yakinifu wa minara 467 umekamilika, 261 imejengwa na 130 kati yake tayari inatoa huduma.

Ujenzi wa minara ya redio 15 unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 30 mwaka huu. Vilevile, ufungaji wa miundombinu mikuu ya mawasiliano katika TTCL Dar es Salaam na Dodoma umekamilika kwa asilimia 90, huku ugomboaji wa vifaa ukiwa umefikia asilimia 65.

Mafunzo ya ndani yanayozinduliwa leo yataendelea hadi Novemba 7, 2025 na yanatarajiwa kuwanufaisha wataalamu 140 katika maeneo ya Radio Access Network (BTS Systems), Transmission (Backhauling), Power Systems, Civil Works (Towers), na Core Network.

Kwa hatua hiyo, Serikali imedhihirisha dhamira ya kuhakikisha kila kijiji nchini kinafikiwa na huduma za mawasiliano, ili kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutawala.