Mahakama yakataa zuio kesi ya Mpina, yaruhusu mubashara

Dodoma. Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma imekataa ombi la mwanachama wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Luhaga Mpina, la kuzuia uchapishaji wa fomu za kupigia kura kwa nafasi ya urais.

Mpina ametoa ombi hilo leo, Septemba 29, 2025, kupitia jopo la mawakili wake katika shauri lake la kikatiba la kupinga kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu 2025, ulipangwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 24027 limefunguliwa na Mpina na Bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo (waombaji wa kwanza na wa pili mtawalia) dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wajibu maombi wa kwanza na wa pili mtawalia.

Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji watatu–Fredrick Manyanda (kiongozi wa jopo), Abdallah Gonzi na Sylvester Kainda, lilipangwa leo kwa ajili ya Mahakama kutoa amri muhimu kuhusiana na mwelekeo wa usikilizwaji wake.

Mahakama, baada ya kujiridhisha kuwa hatua ya ubadilishanaji nyaraka za kesi baina ya pande mbili zinazohusika imekamilika, imepanga kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya maandishi, kufuatia maombi yaliyowasilishwa na wajibu maombi kupitia jopo la mawakili wao.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa wajibu maombi, Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo (kiongozi wa jopo), anayesaidiana na mawakili wa Serikali, Vivian Method, Stanley Kalokola na Erigh Rumisha, ameiomba Mahakama hiyo usikilizwaji ufanyike kwa njia ya maandishi.

Kutokana na maombi hayo, Kiongozi wa jopo la mawakili wa Mpina, John Seka, akisaidiana na mawakili Edson Kilatu na Jasper Sabuni, ameieleza Mahakama kuwa hana pingamizi na maombi ya wajibu maombi shauri hilo kusikilizwa kwa njia ya maandishi.

Hata hivyo, ameiomba Mahakama ipange tarehe za karibu za uwasilishaji wa hoja za maandishi za kila upande na pia kutoa amri ya zuio la muda dhidi ya wajibu maombi, ili fomu za kura zisichapishwe.

Wakili Seka amedai kuwa muda uliosalia kabla ya siku ya kupiga kura ni mfupi, na kwamba, kama karatasi zitaruhusiwa kuchapishwa, zinaweza kuathiri mchakato, hivyo ameiomba Mahakama hiyo itoe amri hiyo ya zuio kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi.

“Sisi hatuna pingamizi na maombi ya usikilizwaji wa shauri hili kwa njia ya maandishi. Hata hivyo sisi tuna mapendekezo”, amesema wakili Sekoa na kufafanua.

“Kwa kuwa shauri hili ni nyeti hasa kwenye mchakato wa uchaguzi unaondelea na mleta maombi wa kwanza anapigania haki yake, hivyo basi, tunaiomba Mahakama hii itoe amri ya zuio ili mjibu maombi wa kwanza asiendelee na mchakato wa uchapishaji wa karatasi za kura (ballot paper)”.

Pia, Wakili Seka ameiomba Mahakama iruhusu siku ya usikilizwaji wa mwisho na mawakili wa pande zote watawasilisha hoja zao za mwisho kwa njia ya mdomo, kufafanua baadhi ya mambo katika hoja za maandishi, shauri hilo lirushwe mubashara.

Wakili Seka ametaja ombi hili kuwa, wanaiomba Mahakama iruhusu kesi hiyo itakapotajwa iruhusiwe kuwa mubashara kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kuisikiliza kokote waliko ili pia kupunguza msongamano wa kwenda mahakamani.

Akijibu hoja hizo, wakili Mulwambo amesema hawana pingamizi na suala la Mahakama kupanga muda mfupi wa kuwasilisha hoja kwa kila upande, kama waombaji walivyoomba kutokana na haraka ya jambo.

Ameeleza kuwa hawana pingamizi shauri kurushwa mubashara kwa maslahi ya umma, lakini akaiachia Mahakama suala la udhibiti wa upotoshaji wa matangazo hayo.

Hata hivyo, amepinga ombi la amri ya zuio la muda kuhusu uchapishaji wa karatasi za kura, akidai kuwa hilo ni gumu na akaiomba Mahakama likatae.

Wakili Seka amesisitiza hoja hiyo, akidai kuwa waliwasilisha ombi hilo kwa sababu maalumu huku akidai mawakili wa wajibu maombi hajaeleza kama amri hiyo itakuwa na hasara yoyote kwa upande wao.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Manyanda amekubaliana na maombi ya usikilizwaji wa shauri hilo kwa njia ya maandishi, huku akiutoa muda wa siku mbili kwa kila upande kuwasilisha hoja zake za maandishi.

Jaji Manyanda ameelekeza kuwa hatua hiyo inapaswa kuwa imekamilika kufikia Oktoba 4, 2025, saa sita mchana, huku akipanga shauri hilo lisikilizwe kwa mdomo, ambapo mawakili watafafanua baadhi ya hoja zao za maandishi Oktoba 6, 2025.

Mahakama pia imekubaliana na ombi la waombaji kuhusu kurushwa mubashara shauri hilo.

Hivyo, Jaji Manyanda amemuagiza Naibu Msajili wa mahakama kushughulikia jambo hilo na ahakikishe siku ya Oktoba 6, 2025 shauri liwe mubashara na wananchi waweze kufuatilia.

Kuhusu amri ya zuio la kuchapisha karatasi za kura, Jaji Manyanda amesema jambo hilo lingeweza kutekelezwa iwapo tu, kama kuna hatari kubwa au uharibifu mkubwa, lakini kwa kuzingatia mazingira ya sasa, hawawezi kutoa amri hiyo.

Amesisitiza kuwa amri hiyo inaweza kuanguka ikiwa shauri litakamilika haraka na kutoa uamuzi wa mwisho kwa wakati unaofaa.

Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo Agosti 6, 2025 kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.