Mwinyi: Wananchi Mji Mkongwe mtapewa makazi, nyumba zenu zikikarabatiwa

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amewaondolea hofu wananchi wa Mji Mkongwe kwamba licha ya mpango maalumu wa kuzifanyia marekebisho makubwa nyumba za mji huo, hakuna mwananchi hata mmoja atakayehamishwa katika eneo hilo.

Pia, ameeleza alivyokataa wawekezaji wa Dola za Marekani 30 milioni, sawa na Sh73.5 bilioni kuwekeza katika eneo la Bwawani kwa kile alichoeleza kwamba eneo hilo lina thamani kubwa kuliko kiwango hicho.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Septemba 29, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa Malindi katika ukumbi wa Bwawani Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni sehemu ya kampeni za chama hicho.

Itakumbukwa kwamba tayari Serikali imeshatenga Sh13 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya Mji Mkongwe.

“Tuna mpango maalumu kufanya marekebisho ya Mji Mkongwe kuutengeneza ili kuta zake ziweze kuishi miaka mingine zaidi ya 100, lakini niwaondoe hofu ndugu zangu hakuna atakayeondolewa isipokuwa tunaandaa nyumba za muda ambazo watu watakaa wakati tukitengeneza nyumba hizo,” amesema.

Amesema tayari mpango huo umeanza ambapo mji huo utakuwa wa kisasa zaidi ukiwa na miundombinu ya umeme, maji na intaneti itakayopita chini ya ardhi tofauti na ilivyo sasa ambapo nyaya nyingi zinazopita juu, hivyo kuondosha haiba ya mji huo ambao ni urithi wa kidunia.

“Magari ya umeme ndio yatakayoingia katikati ya mji huu ili kuondosha mtetemeko wa nyumba,” amesema

Licha ya nyumba hizo kuwa na wamiliki wa aina tatu tofauti, Serikali ambaye anasimamiwa na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), nyumba za wakfu na nyumba binafsi, lakini mpango huo unahusu nyumba zote.

“Hakuna atakayehamishwa hata mmoja, watu watahamishiwa kwa muda kwenye nyumba zinazoandaliwa na mpango huu ukikamilika watarejea wote katika nyumba hizo,” amesema.

Kuhusu uwekezaji wa Bwawani, Dk Mwinyi amesema wamekuja wawekezaji kadhaa lakini anawakataa kwa sababu walikuwa na kiwango kidogo cha mtaji kati kwani eneo hilo lipo kimkakati zaidi.

“Wapo wenzetu wanasema wameleta wawekezaji lakini tumewakataa, dola 3 milioni kweli uwekeze hapa? Hata aje mwenye dola 30 milioni, siwezi kukubali, hapa tunahitaji mwekezaji mkubwa zaidi,” amesema.

Amesema iwapo wakirejea madarakani wataona uwekezaji utakaofanyika katika eneo hilo, hivyo amewaomba wananchi hao kumpa ridhaa tena akabadilishe eneo hilo.

Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kuzungumza, licha ya kupongeza hatua zilizofikiwa, wametaja changamoto zinazowakabili katika eneo hilo ikiwemo kero ya makontena kutokana na bandari iliyopo katika eneo hilo.

Mohamed Abdulrhaman amesema kinatokea vumbi kali inayosababishwa na magari makubwa yanayobeba makontena hayo.

“Ukiangalia hata vumbi linakuwa kubwa sana kiasi kwamba hata taa za umeme wa jua zinashindwa kuwaka kutokana na kujaa vumbi, hii ni changamoto yetu kubwa licha ya jitihada zinazofanyika,” amesema.

Amina Haji ambaye ni mjasiriamali katika eneo hilo, amesema wanasumbuliwa kufukuzwa na kunyang’anywa bidhaa zao, hivyo wanaomba kuangaliwa kwa jicho la kipekee.

Akitolea ufafanuzi wa kero hizo, Dk Mwinyi amesema mipango mizuri inakuja kikubwa wamrejeshe madarakani ili kushughulikia changamoto hizo.

Hata hivyo, amesema tayari wameshaanza kuchukua hatua ikiwa ni kujenga bandari zingine za Mangapwani na Fumba, iwapo zikikamilika Malindi itabaki kuwa ya kitalii mizigo na makontena vitatushushwa katika bandari hizo.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema kazi iliyofanywa na Dk Mwinyi ni kubwa kwa kipindi cha miaka mitano, kwa hiyo hakuna mbadala waendelee kuichagua CCM ili ikamilishe makubwa inayoendelea kufanya.

“Leo faraja yetu Wazanzibari ni Dk Mwinyi, jukumu letu ni kumpa kura tena ili kuifanya Zanzibar kuzidi kusonga mbele,” amesema.