New King yakaribishwa Ligi Kuu Zanzibar kwa kipigo

WAGENI katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), New King wamekaribishwa na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Mwembe Makumbi katika mwendelezo wa ligi hiyo, mechi ikichezwa leo Septemba 29, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.

Said Suleiman aliitanguliza New King kwa bao la mapema dakika ya 17 huku Yakoub Mohamed akiisawazisha Mwembe Makumbo dakika ya 42. Timu zikaenda mapumziko  matokeo yakiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili, Salum Mlinde aliihakikishia ushindi Mwembe Makumbi alipofunga mabao mawili, la kwanza dakika ya 72 kisha akahitimisha kwa mkwaju wa penalti dakika ya 82.

Katika mechi hiyo, kadi nne zilionyeshwa kutokana na matukio yasiyo ya kinidhamu, kati ya hizo tatu za njano ambapo mbili zikienda Mwembe Makumbi na moja New King, huku kipa wa timu hiyo pia akionyeshewa kadi nyekundu iliyofanya timu hiyo kumaliza ikiwa pungufu.

New King imekuwa timu ya pili mchezaji wake kuonyeshwa kadi nyekundi katika Ligi Kuu Zanzibar msimu huu baada ya Uhamiaji katika mechi ya kwanza dhidi ya Polisi ambapo Ali Issa alikuwa wa kwanza kupata adhabu hiyo.