……………….
Na: Mwandishi Wetu, Ubungo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda amesema wananchi wa Jimbo la Ubungo Jijini Dar es Salaam wamemuhakikishia kuwa Oktoba 29, 2025, watachagua wagombea wote watokanao na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani wameridhika na utekelezaji wa Ilani Jimboni hapo.
Chatanda ameyasema hayo Septemba 29, 2025 , katika mwendelezo wa ushiriki wake katika ziara ya Mgombea mwenza wa Urais kupitia CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi Jijini Dar es Salaam.
“Mimi kama mratibu na wenzangu tulipowatembelea wanzetu wa Ubungo walituagiza wakasema wanataka tuwape nafasi waonane na Dkt. Samia Suluhu Hassan ili wamwambie kuwa watampa kura za ndiyo, nikawaambia subirini anakuja Dkt. Nchimbi, Mgombea mwenza yeye ndiye mtamwonyesha na kumpa hizo salamu ili awafikishie, sasa leo wapo hapa, utawaona na watakuthibitishia kwamba watampa kura za kishindo, kura za mafuriko,” amesema Chatanda.
Sambamba na hilo, Chatanda amesisitiza kuwa amepata fursa ya kuongea na wanawake na makundi mengine ya jamii ndani ya Jimbo la Ubungo, ambao pia wamemuhakikishia kuwa watawachagua wagombea wote wa CCM ili kuharakisha kasi ya maendeleo.
UWT ni moja ya taasisi chini ya CCM ambayo inategemewa sana katika ushawishi wa wapigakura ili kukipatia Chama hicho ushindi wa kishindo wakiongozwa na msemo wa “wanawake ni jeshi kubwa”.