Bandari ya Dar itakavyokabili ongezeko la mizigo mwisho wa mwaka

Dar es Salaam. Kadri msimu wa kilele cha usafirishaji wa mwisho wa mwaka unavyokaribia, wadau wa bandari wanaongeza kasi ya maandalizi kushughulikia kile kinachotarajiwa kwenye msimu wenye shughuli nyingi za mizigo bandarini.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa kushirikiana na waendeshaji binafsi, imetangaza hatua kadhaa za kimkakati zinazolenga kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa kusubiri kwa meli na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji cha kuaminika katika ukanda huu.

Miongoni mwa miradi ya mfano ni utekelezaji wa mfumo wa fixed berthing window katika gati namba 8 hadi 11, yanayosimamiwa na Kampuni ya Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited.

Mfumo huu ulioanzishwa mwaka huu, unarahisisha upangaji wa ratiba za meli, kupunguza sintofahamu kuhusu nyakati za kuwasili na kupunguza msongamano.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, ameliambia gazeti dada la The Citizen leo kuwa njia hiyo mpya tayari inaleta matokeo.

“Mpango huu unarahisisha upangaji bora na uratibu wa kuwasili kwa meli, jambo linalopunguza kwa kiasi kikubwa msongamano bandarini. Meli zinajua kwa uhakika muda zitakapotia nanga, na upatikanaji huu wa taarifa unabadilisha mfumo mzima wa shughuli,” amesema.

Mabadiliko hayo yanajiri wakati Bandari ya Dar es Salaam ikiwa imefunga mwaka wa fedha 2024/25 kwa rekodi mpya ya shehena ya mizigo iliyofikia tani milioni 27.7 sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka tani milioni 23.69 za mwaka uliopita, na kuwa kiwango cha juu zaidi katika historia yake.

Takwimu hizo pia zinaashiria ongezeko kubwa kutoka tani milioni 18 mwaka wa fedha 2021/22.

Kwa mujibu wa TPA, ongezeko hilo linaonesha matokeo ya maboresho ya miundombinu, mageuzi ya uendeshaji na kasi ya huduma ambayo yamevutia zaidi mashirika ya usafirishaji na wamiliki wa mizigo.

Katika gati namba 0 hadi 7, yanayosimamiwa na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji DP World, uwezo unaongezwa zaidi kupitia ununuzi wa crane mbili mpya za ship-to-shore, na kufanya jumla kufikia tano.

Uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza kasi ya kushughulikia makontena na kupunguza muda wa meli kukaa bandarini, hivyo kurahisisha mtiririko wa bidhaa msimu wa kilele.

Uhusiano wa usafirishaji wa ndani unabaki kuwa kipaumbele. TPA inashirikiana kwa karibu na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuimarisha uhusiano na Bandari Kavu ya Kwala. Injini mbili zilizokarabatiwa zinatarajiwa kuanza kazi ifikapo Oktoba, zikiongeza uwezo wa reli kusafirisha makontena kutoka katikati ya jiji lililojaa msongamano.

Ujenzi wa Kurasini Logistics Centre, kituo muhimu cha kusaidia shughuli, pia unaendelea.

Kituo hicho ambacho sasa kimekamilika kwa asilimia 40, kitapunguza shinikizo katika maeneo ya kuhifadhi mizigo bandarini.

Mbossa amesema maboresho hayo yatazalisha manufaa kamili iwapo wamiliki wa mizigo na mawakala wa ushuru pia watafanya sehemu yao.

“Ili kuhakikisha maboresho ya miundombinu yanatafsirika kwenye urahisi wa shughuli, tunatoa wito kwa wadau kuharakisha ukaguzi na uchukuaji wa mizigo. Mikutano ya mara kwa mara inaendelea kuratibu upangaji wa usafirishaji na kuepusha vikwazo wakati wa miezi ya shughuli nyingi inayokuja,” amesema.

“Dar es Salaam inashuhudia mageuzi makubwa,” amesema Mbossa.

 “Msingi unaowekwa sasa si tu kwa ajili ya msimu huu wa kilele, bali kwa ajili ya ukuaji endelevu utakaoiweka Tanzania katika ushindani wa biashara za kikanda na kimataifa.”

Kwa upande wa wasafirishaji, ongezeko linalotarajiwa ni changamoto na fursa kwa wakati mmoja. Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay, ameiambia The Citizen kuwa wanachama wanajiandaa kuhakikisha usafirishaji wa mizigo unaenda vizuri.

“Tunashukuru kwa maboresho makubwa yaliyofanyika bandarini. Ongezeko la mizigo linatoa fursa kubwa kwa wasafirishaji,” amesema Lukumay.

Amebainisha kuwa ingawa sekta bado inakabiliwa na changamoto, ikiwamo ugumu wa kupata mizigo ya kurudi baada ya safari, hatua kubwa zimepigwa.

“Magari mengi hurudi tupu baada ya kupeleka bidhaa katika nchi jirani, jambo ambalo ni ghali. Lakini juhudi zinaendelea kuanzisha njia za kupata mizigo ya kurudi. Wakati huohuo, ufanisi ulioongezeka bandarini na maboresho ya barabara yanavutia uwekezaji mpya katika sekta ya usafirishaji,” amesema.

Msimu wa usafirishaji mwisho wa mwaka, ambao kwa kawaida huanza Septemba na kuendelea hadi Februari, daima umekuwa mtihani muhimu kwa Bandari ya Dar es Salaam.

Kipindi hiki huambatana na wafanyabiashara kuagiza bidhaa kuelekea Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Kichina na msimu wa sherehe.

Bandari hiyo pia hutumika kama lango kwa nchi zisizo na bandari kama Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambazo huhitaji huduma zaidi kutokana na ukuaji wa shughuli za madini na upanuzi wa uchumi katika ukanda huu.

Mwaka Mpya wa Kichina, pia hujulikana kama Spring Festival au Lunar New Year, ni sikukuu muhimu zaidi katika utamaduni wa Kichina na mwaka 2024 uliwekwa katika orodha ya Urithi wa Tamaduni Usioshikika wa Unesco.

Tarehe yake hubadilika kila mwaka katika kalenda ya magharibi, lakini huangukia Januari au Februari. Mwaka 2026, Mwaka Mpya wa Kichina utakuwa Februari 17, na mwaka 2027 utakuwa Februari 6.

Maofisa wa TPA na wadau wa sekta wamesema kuwa maboresho ya pamoja katika magati, reli na mitandao ya barabara yataihakikishia nchi maandalizi bora zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa.