Magonjwa, dawa na kelele vyatajwa vyanzo upungufu wa usikivu

Dar es Salaam. Watoto 16 wenye changamoto ya kusikia, wenye umri wa chini ya miaka mitano, wamepatiwa vifaa maalumu vya kusaidia kusikia (cochlear implant) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Kupewa vifaa hivi ni kutokana na kuongezeka kwa matatizo ya usikivu nchini, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa nchini, wawili wanakutana na changamoto hiyo.

Kwa upande wa watu wazima, tatizo la upungufu wa usikivu linazidi kuongezeka, huku baadhi ya sababu zinazotajwa kuwa ni matumizi ya vifaa vya kielektroniki (headphone, earphone) kwa sauti kubwa, magonjwa sugu, matumizi ya dawa, na kukaa kwenye mazingira yenye kelele kwa muda mrefu.

Kauli hiyo imetolewa leo, Septemba 29, 2025 katika hafla ya kuwasha vifaa16 kwa watoto waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo la kutosikia iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Belilah Kimambo akizungumza na wazazi ambao hawapo pichani hospitalini hapo leo Septemba 29, 2025.



Daktari bingwa wa upasuaji wa masikio, pua na koo, Aslam Nkya ameeleza kuwa huduma hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa watoto, hasa walio na umri chini ya miaka mitano.

“Kila mtoto anayezaliwa katika Hospitali ya Muhimbili sasa tunampima ili kubaini kama ana tatizo la usikivu, huduma hii inafaa zaidi kwa watoto walio na umri mdogo, kwani kwa watoto hawa, matibabu yana matokeo mazuri zaidi,” amesema Dk Nkya.

Dk Nkya amesema watu wazima wengi wanakutana na changamoto ya usikivu kutokana na matumizi ya vifaa hivyo kwa sauti kubwa, kukaa kwenye mazingira yenye kelele kwa muda mrefu, na magonjwa sugu ambayo husababisha madhara kwenye masikio.

Aidha, ameweka wazi kuwa baadhi ya watoto wanazaliwa na changamoto hii au wanapata matatizo ya usikivu kutokana na matumizi ya dawa na ajali mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Dk Delilah Kimambo, ameeleza kuwa huduma za usikivu hospitalini hapo zimeimarika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017, ambapo watoto 103 wameshapata vifaa vya kusikia.

Daktari Bingwa wa upasuaji wa masikio, pua na koo, Aslam Nkya kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akizungumza na wazazi wenye watoto ambao wanachangamoto ya usikivu hawapo pichani wakati wa  leo Septemba 29, 2025 hospitalini hapo.



Dk Kimambo amesema kuwa huduma hiyo ni muhimu kwa watoto na kwamba wazazi wanapaswa kuhamasisha jamii kuhusu uwepo wa huduma hiyo ili kusaidia kupambana na changamoto hiyo.

“Huduma hii ilianza kutolewa mwaka 2017 na hadi sasa tumewasaidia watoto 103, ingawa bado idadi ni ndogo. Tunawataka wazazi kuwahamasisha wenzao na jamii ili tukomeshe tatizo hili la usikivu nchini,” amesisitiza Dk Kimambo.

Dk Kimambo amefafanua kuwa awali, Serikali iligharamia watoto 50 kwenda kutibiwa nje ya nchi kati ya mwaka 2010 na 2016, kwa gharama ya Sh6 bilioni. Hata hivyo, tangu huduma hiyo itolewe nchini, Serikali imegharamia watoto 34 kwa Sh1.5 bilioni, ambapo wangeenda kutibiwa nje ya nchi gharama yake ingekuwa Sh4 bilioni.

Juma Puta, ambaye mtoto wake alipata huduma hiyo hospitalini hapo, amesema aligundua mtoto wake ana changamoto ya kusikia akiwa na umri wa miaka miwili.

Alimpeleka Hospitali ya Muhimbili ambapo alipatiwa matibabu na kwa sasa anaendelea vizuri akiwa kidato cha pili.

“Mwanangu aligundulika kuwa na changamoto ya usikivu akiwa na umri wa miaka miwili, nilimleta hapa Muhimbili kwa matibabu. Sasa anaendelea vizuri na amefika kidato cha pili, ni muhimu wazazi wawahi kutoa matibabu mapema kwa watoto,” amesema Puta.

Naye Mariamu Mndeme, ambaye mtoto wake alizaliwa akiwa na uwezo wa kusikia lakini akaanza kuupoteza taratibu, amesema walichukua hatua ya kumpeleka mtoto wao kwenye matibabu.

Amesisitiza kuwa ni muhimu wazazi wachukue hatua haraka ili kuepuka madhara zaidi kwa watoto wao.