Jipange na gharama hizi za matibabu ya moyo, usipoacha haya

Dar es Salaam. Kama huzingatii ushauri wa wataalamu juu ya kubadili mfumo wa maisha, upo hatarini kupata maradhi ya moyo ambayo kulingana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) matibabu yake ni hadi Sh30 milioni.

Maradhi mengine ambayo wataalamu wanaonya kuathiri moyo, ni shambulio la moyo ambayo matibabu ni Sh6 milioni kuzibua mshipa mmoja, kuwezesha umeme wa moyo kwa kufunga kifaa maalumu ni Sh10 milioni na moyo kushindwa kufanya kazi Sh30 milioni matibabu yake.

Wataalamu wa moyo wanasema asilimia 70 ya magonjwa ya moyo hutokana na shinikizo la juu la damu ambalo hupatikana kwa mtu kutofanya mazoezi, kula vyakula vyenye mafuta mengi na matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Haya yameelezwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo JKCI, Dar Group, Tulizo Shemu katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika katika taasisi hiyo kwa wananchi kupimwa afya zao.

“Moyo unashambuliwa na changamoto mbalimbali ni muhimu mtu akafika kituo cha afya walau mara moja au mbili kwa mwaka, kupima afya yake na wale wanaobainika kuwa na shida watumie dawa,” amesema.

Dk Shemu amesema ilikuwa kawaida miaka ya nyuma watu wenye miaka 70 na kuendelea kushambuliwa na maradhi ya moyo, lakini sasa hali hiyo imebadilika kwani makundi yote yanashambuliwa na maradhi hayo.

“Kutokana na mtindo mbovu wa maisha tumeanza kuona vijana wa miaka 30 hadi 20 wakisumbuliwa na maradhi ya moyo, ulihitajika kuwa na miaka 70 na kuendelea ili upate shinikizo la juu la damu sasa mambo ni tofauti, hii inatukumbusha kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji bora,” amesema.

Dk Shemu ameshauri watu kupunguza ulaji wa nyama nyekundu, matumizi ya tumbaku, sigara, kuepuka vyakula vilivyosindikwa na kupunguza msongo wa mawazo kama njia mojawapo kukabiliana na maradhi ya moyo ikiwemo shinikizo la juu la damu.

Mtaalamu huyo amesema ugonjwa huo unaweza kushambulia afya ya mtu pasipo mtu kufahamu akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wanaweza kupata ugonjwa huo na kutotambua hali waliyonayo.

Dk Shemu amesema, katika kila watu 1,000 wanaofanyiwa uchunguzi kwenye taasisi hiyo, asilimia 50 hadi 60 wanafika kwa ajili ya shinikizo la juu la damu huku akidokeza pia kwa watu 100 wanaofika kupima 70 ni kwa ajili ya tatizo hilo.

Dalili za tatizo hilo, Dk Shemu ametaja ni maumivu ya kichwa, uchovu usio na sababu, mapigo ya moyo kwenda haraka, kushindwa kuona vyema (kuona ukungu kwenye macho), maumivu makali ya moyo, kupooza upande mmoja wa mwili.

Shinikizo la damu ni hali ambayo presha ya damu inazidi kiwango cha kawaida cha 120/80.

Shinikizo la damu hutokea pale ambapo nguvu ya msukumo wa damu kwenye kuta za mishipa ni kubwa kupita kiasi, hali inayoweza kusababisha uharibifu wa mishipa ya damu na viungo muhimu.

Takwimu za Mfumo wa Ukusanyaji wa Taarifa za Afya Tanzania (DHIS2) zinaonyesha ongezeko la wagonjwa kutoka 1,315,000 mwaka 2019/2020 hadi 1,665,019 mwaka 2023/2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dk Peter Kisenge, amesema tatizo la kisukari nalo linachangia mtu kupata shida ya mishipa ya moyo.

“Watoto nao wanapata matatizo ya moyo, unapokuwa na mimba na ukatumia pombe unaweza kujifungua mtoto mwenye shida ya tundu la moyo, kutopata chanjo ya magonjwa mbalimbali, kupata mimba ukiwa na kisukari nako kunachangia tatizo la moyo,

“Kutumia dawa bila kuzingatia ushauri wa daktari, kuna dawa ambazo si nzuri kwa mtoto unapotumia dawa holela unahatarisha afya ya mtoto aliye tumboni,” amesema.

Amesema Tanzania kuna watoto 10,000 wenye matatizo ya moyo na watoto 4,000 wanahitaji upasuaji wa haraka, hivyo ni muhimu wananchi kutambua kinga ni bora kuliko tiba.

Mama wa miaka (51) Siwema Mussa amesema mara kwa mara amekuwa akisikia maumivu ya mwili upande mmoja huku miguu ikiisha nguvu hivyo amejitokeza kupima kufahamu hali yake.

Amesema baada ya vipimo amebainika kuwa na shida kwenye mgongo na shinikizo la damu hivyo amepewa maelekezo ya namna anavyopaswa kuzingatia lishe bora.

Mkazi wa Uwanja wa Ndege, Salum Kunguni (60) amesema ameitumia siku ya maadhimisho ya moyo duniani kufahamu hali yake na kujifunza namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Shaban Salum mkazi wa Segerea Dar es Salaam amesema baada ya vipimo amegundulika kuwa na shinikizo la juu la damu.

“Sikuwa nimepima afya yangu, leo nimepita hapa kufanya uchunguzi nikagundulika nina shinikizo la juu damu na nimeambiwa nianze kuja Hospitali kwa ajili ya kliniki, sikuwa naona dalili zozote lakini nilipopimwa ndio tatizo limeonekana,” amesema.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kukosekana kwa uelewa wa maradhi ya moyo na kuwa na mfumo bora wa maisha, kumechangia ugonjwa wa moyo kuwa tatizo linaoongoza kusababisha vifo duniani kwa asilimia 31.

Idadi hiyo ni sawa na takriban watu milioni 17.9 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa hayo.

Septemba 29 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya moyo na mwaka huu maadhimisho haya yanaongozwa na kaulimbiu isemayo:  ‘Linda pigo la moyo wako’ ikiwa ni msisitizo wa umuhimu wa kuwa makini kila wakati kuhusu afya ya moyo, ikihimiza watu kuwa na msimamo wa kuchukua tahadhari mapema kwa kutozipuuza dalili za maradhi na kudumisha tabia bora za afya.