MENEJA WA TRA KILOMBERO AHIMIZA ULIPAJI KODI KWA HIARI

Kilombero 

Wakati awamu ya tatu ya kulipa Kodi ikitarajiwa kuhitimishwa hapo kesho tarehe 30.09.2025, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro Bw. Innocent Minja amewataka Walipakodi ambao bado hawajakamilisha malipo ya Kodi zao, kulipa kwa hiari ndani ya muda uliosalia.

Akizungumza na Walipakodi wakati wa zoezi la elimu ya Kodi mlango kwa wilayani Kilombero mkoani Morogoro lililoanza Septemba 26.2025 Bw. Minja amesema ni vema kila Mlipakodi akatimiza wajibu wake wa kulipa kodi kwa hiari ili kuepuka riba na adhabu inayotozwa baada ya kuchelewa kulipa Kodi.

Bw. Minja amesema malengo ya makusanyo yaliyowekwa na Serikali yatafikiwa iwapo kila mtu mwenye kipato atalipa kodi ambapo ndiyo maana TRA inaendesha zoezi la kutoa elimu ya Kodi mlango kwa mlango.

Amesema wakati wa kutoa elimu pia wanatumia fursa hiyo kuwakumbusha Walipakodi kulipa Kodi ya awamu ya tatu mnamo au kabla ya tarehe 30.09.2025.

“Tunapita kutoa elimu ya kodi mlango kwa mlango kwa Wafanyabiashara kwa lengo la kuwawezesha  wanaotaka kulipa Kodi lakini hawajui mahala pa kuanzia kuanza kulipa Kodi jambo ambalo litaongeza wigo wa kodi” alisema Bw. Minja.

Baadhi ya Wafanyabiashara waliotembelewa wakizungumza kwa nyakati tofauti wameshauri zoezi hilo liwe endelevu na kuwapongeza TRA kwa kuwafuata na kuwapa elimu katika biashara zao.

 

= = = = = =