SI umeona kilichotokea wikiendi kwa wawakilishi wetu wa Tanzania kimataifa? Basi majibu ya nani anakwenda kucheza hatua ya makundi yatapatikana wiki ya mwisho ya Oktoba 2025.
Ipo hivi; Msimu huu 2025-2026, Tanzania imekuwa na jumla ya wawakilishi sita katika mashindano ya kimataifa, nne kutoka Tanzania Bara na mbili Zanzibar.
Tanzania Bara kuna Yanga na Simba zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam na Singida Black Stars zikicheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Kule Zanzibar, Mlandege ilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika, imeishia hatua ya awali ikiondoshwa na Ethiopian Insurance, lakini imebaki KMKM inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa hatua ya pili ya mtoano, kuna uhakika mbele ya safari kuiona timu moja ya Tanzania ikicheza hatua ya makundi upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, hii inatokana na KMKM kukutana na Azam. Hapo atakayeshinda kwa matokeo ya jumla ndiye anafuzu makundi.
Azam haijawahi kucheza hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa tangu kuanza kushiriki kwake mwaka 2015 ambapo ilianzia Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka huo ilikuwa sambamba na KMKM, zote zikaishia hatua ya awali.

Safari hii, Azam ipo chini ya Florent Ibenge, kocha mwenye rekodi kubwa katika michuano ya CAF akibeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2021-2022 akiinoa RS Berkane ya Morocco.
Kikosi hicho kwa kuonyesha kimepania kufanya kweli msimu huu, hatua ya awali imeiondosha Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0. Ilishinda mechi zote mbili nyumbani na ugenini kwa mabao 2-0.
Kwa upande wa KMKM, hatua ya awali imeitoa AS Ports ya Djibouti, huku mechi zote mbili zilizochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, imeshinda kwa mabao 2-1, jumla imefuzu kwa ushindi wa 4-2.

Simba iliyofundishwa na makocha wawili tofauti akianza Fadlu Davids kisha Hemed Suleiman ‘Morocco’, imefuzu baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Gaborone United na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-1. Kumbuka ugenini Simba ilishinda 1-0.
Yanga imeitoa Wiliete ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0. Imepiga mtu nje ndani ambapo mechi ya kwanza ugenini ilishinda 3-0, nyumbani ikaibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0. Imefuzu kwa kishindo bila ya kuruhusu bao kama ilivyo kwa Azam.
KITUO KINACHOFUATA
Kati ya Oktoba 17 hadi 19 mwaka huu, mechi za mtoano hatua ya pili zinakwenda kuchezwa ambapo faida nyingine ilizonazo timu za Tanzania, zinaanzia tena ugenini kama ilivyokuwa awali. Baada ya hapo, marudiano ni kati ya Oktoba 24 na 26 mwaka huu.
Simba itakuwa mgeni wa Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, kisha marudiano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Nsingizini Hotspurs haijafika hapa kwa bahati kwani imepindua matokeo kufuatia ugenini kufungwa 1-0 dhidi ya Simba Bhora, kisha nyumbani ikapata ushindi kama huo. Katika penalti, ikashinda 4-2.
Kwa upande mwingine, Yanga itakuwa mgeni wa Silver Strikers ya Malawi, kabla ya kurudiana Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwania kufuzu makundi.

Yanga inasaka rekodi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kufanya hivyo 2023-2024 na 2024-2025 ikiwa chini ya Miguel Gamondi ambaye sasa anainoa Singida Black Stars.
Matokeo ya 0-0 iliyopata Silver Strikers nyumbani dhidi ya Elgeco Plus, yameivusha timu hiyo baada ya ugenini kutoka 1-1, hivyo bao la ugenini limeibeba.
Yanga msimu huu imeshinda mechi zote nne za mashindano ilizocheza, tena haijaruhusu bao lolote ikifunga mabao tisa.
Mchezo wa ndugu wawili ni huu hapa katika Kombe la Shirikisho Afrika, KMKM ikianza kuikaribisha Azam kwenye Uwanja wa New Amaan Cmplex, kisha marudiano ni pale Azam Complex.
KMKM ushindi wa jumla wa mabao 4-2 dhidi ya AS Port, umeifanya timu hiyo kuipeperusha Zanzibar kimataifa, wakati wapinzani wao Azam wakiwatoa Al Merreikh Bentiu kwa mabao 4-0.
“Hakuna mchezo rahisi, Al Merikh walikuja wakiwa hawana cha kupoteza, nadhani hatujacheza vizuri zaidi tuwezavyo, sababu hatujafunga nafasi zetu za wazi, lakini tumetengeneza nafasi za wazi ambazo pia mambo mazuri tutayafanyia kazi kwa njia hiyo ili kupata ushindi zaidi ya leo (juzi).
“Tunakwenda kujiandaa na mchezo dhidi ya KMKM kwa kucheza Ligi ya Tanzania Jumatano. Tuna mchezo mkubwa wa kucheza dhidi ya JKT. Kwa hiyo tutazingatia mchezo huu kwanza na baada ya hapo tutafikiria kuhusu huo mchezo,” amesema Ibenge.
Flambeau du Centre ya Burundi inakwenda kuikaribisha Singida Black Stars kuwania kuweka rekodi katika Kombe la Shirikisho Afrika, lakini pia Singida Black Stars nayo inaitaka hiyo rekodi ambayo itaihitimisha nyumbani kati ya Oktoba 24 na 26 mwaka huu.
Singida Black Stars inayofundishwa na Miguel Gamondi, imeitoa Rayon Sports kwa jumla ya mabao 3-1, ilianzia ugenini na kushinda bao 1-0, nyumbani ikashinda tena 2-1. Kwa upande wa Flambeau du Centre imeitoa Al Akhdar ya Libya kwa jumla ya mabao 4-3.
WAFAHAMU WAPINZANI
Nsingizini Hotspurs inayokwenda kucheza dhidi ya Simba, imeanzishwa mwaka 1984, kwa sasa ina miaka 41, wakati Simba imefiksha 89.
Hao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Eswatini msimu wa 2024-2025. Ikumbukwe msimu uliopita 2024-2025 wakati Simba ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Nsingizini Hotspurs iliishia hatua ya awali ya michuano hiyo ikiondolewa na Stellenbosch kwa jumla ya mabao 8-0, nyumbani ilifungwa 3-0 na ugenini ikachapwa 5-0. Stellenbosch ilipokutana na Simba hatua ya nusu fainali, ikapoteza kwa bao 1-0.
Nsingizini Hotspurs imepata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Eswatini msimu wa 2024–25 ikiwa chini ya kocha wa muda, Simon Ngomane, kwa sasa inafundishwa na Mandla David Qhogi.
Katika michuano ya kimataifa, inatumia uwanja wa Somhlolo wenye nyasi bandia ukiwa unapatikana mji wa Lobamba nchini Eswatini. Una uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000.

Jina la utani la Nsingizini Hotspurs ni Insingizi Yezulu lenye maana ya Sauti ya Anga au Umgugudla Lomkhulu ikimaanisha Wimbi Kubwa.
Silver Strikers ni wapinzani wa Yanga, katika michuano ya kimataifa inatumia uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 41,100. Klabu hii Ilianzishwa mwaka 1977.
Jina la utani The Bankers ikiwa chini ya Reserve Bank of Malawi. Inafundishwa na Kocha Etson Kadenge Mwafulirwa.
Flambeau du Centre immeanzishwa mwaka 2016 ikiwa na miaka tisa hivi sasa, inapatikana Gitega, Burundi. Hawa ni wapinzani wa Singida Black Stars katika Kombe la Shirikisho Afrika. Inatumia Uwanja wa Intwari uliopo Bujumbura nchini Burundi wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 10,000.
Flambeau du Centre ilianza kushiriki mashindano ya kimataifa mwaka 2022 katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mwaka huu inashiriki kwa mara ya pili ambapo ipo Kombe la Shirikisho Afrika.
Msimu wa 2022–2023 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, iliishia hatua ya pili ikitolewa na Zamalek kwa jumla ya mabao 6-1. Kabla ya hapo, hatua ya awali iliitoa Al Ittihad ya Libya kwa bao la ugenini baada ya sare ya 2-2.