Na Mwandishi Wetu
OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mkama ameipongeza kampuni ya Saruji Tanga kwa kuweka historia ya kuwa kampuni ya kwanza kutoa hisa stahiki zenye thamani kubwa kuliko zote zilizowahi kutolewa katika masoko ya mitaji hapa nchini.
Ambapo thamani ya hisa hizo ni shilingi bilioni 204, sawa na asilimia 134.2 ikilinganishwa na hisa stahiki za Benki ya CRDB zenye thamani ya shilingi bilioni 152, zilizotolewa mwaka 2015.
Akizungumza Septemba 29,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mauzo ya hisa stahiki za Kampuni ya Saruji Tanga(Tanga Cement PLC) CPC.Mkama amesema anaipongeza Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya Saruji Tanga kwa ujasiri wa kuchukua hatua na kutekeleza mikakati ya kuongezeka ufanisikatika utendaji wa kampuni
Ambapo amesema umewezesha bei ya hisa za kampuni hiyo kuongezeka kwa asilimia 763.3 na kufikia shilingi 2,590 kwa hisa moja hivi sasa, ikilinganishwa na bei ya shilingi 300 kwa hisa moja wakati wa mauzo ya awali ya hisa za kampuni hii mwaka 2002.
“Hatua za Kimkakati zinazotekelezwa na kampuni ya Saruji Tanga sio tu zina faida kwa kampuni hii, bali pia zinaweka msingi thabiti wa mageuzi ya kiutendaji kwa kampuni zilizouza hisa kwa umma na kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam.
“Hatua hizi zinatarajiwa kuwa na matokeo chanya zaidi katika kukuza sekta ya viwanda, hususan katika uzalishaji na usambazaji wa saruji, ambayo ina mchango mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya Taifa letu, na hivyo kutekeleza moja ya malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) ya kuwa na miundombinu bora na endelevu ya Taifa letu.”
Pia amesema nchi yetu ya Tanzania inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi huku akifafanua mikakati hiyo inatekelezwa kwa kutumia nyenzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050).
“Dira ambayo ina malengo ya muda mrefu ya nchi yetu kufikia hadhi ya Kipato cha Juu cha Kati na uchumi wa Dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2050. Pia Dira ya Taifa ya Maendeleo (TDV 2050) inalenga kuwa na uchumi shindani, himilivu na jumuishi kwa maendeleo endelevu kwa Watanzania wote.
“Kupitia Dira hii, wananchi wanapaswa kutumia fursa ya kuinua vipato vyao kwa kutumia njia za uchumi jumuishi, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wananchi kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni za ndani,”amesema CPC.Mkama.
Akieleza zaidi amesema utoaji wa Hisa Stahiki za kampuni ya Saruji Tanga ni mojawapo ya njia za kufanikisha azma hii. Hivyo ninawapongeza Menejimenti ya Kampuni ya Tanga kuwezesha kufikia malengo ya Dira ya Taifa.
Pia amesema Serikali kupitia CMSA ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.
Aidha, CMSA ina jukumu la kuidhinisha maombi ya utoaji wa bidhaa mpya katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na utoaji wa hisa stahiki, kama hizi za kampuni ya Saruji Tanga ambazo leo hii tunazindua rasmi mauzo yake.
“CMSA imeidhinisha Waraka wa Matarajio wa kampuni ya Saruji Tanga kuuza Hisa Stahiki 127,342,090 kwa wanahisa wake kwa bei ya shilingi 1,600 kwa kila hisa katika uwiano wa hisa mpya mbili kwa kila hisa moja aliyonayo mwekezaji hivi sasa, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 204 kinatarajiwa kupatikana.
“Idhini imetolewa baada ya kampuni hii kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hisa Stahiki 2000”
CPA.Mkama amesema hivyo mauzo ya hisa stahiki za kampuni ya Saruji Tanga yamekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya Mitaji. Tunaipongeza Kampuni ya Saruji Tanga kwa kukidhi matakwa ya Sheria, na hatimaye kupata idhini ya CMSA.Mchakato wa kuidhinisha mauzo ya hisa unahusisha taasisi na wataalam mbalimbali.
Aidha amesema mauzo ya hisa stahiki za kampuni ya Saruji Tanga kwenye soko la awali yamefunguliwa leo Septemba a 29 Septemba 2025 na yanatarajiwa kufungwa Oktoba 24 2025, ambapo Wanahisa wa kampuni hiyo wamepewa fursa ya kununua hisa hizo kwa bei ya shilingi 1,600 sawa na punguzo la asilimia 38.2 ikilinganishwa na bei ya soko ambayo ni Sh. 2,590.
CPA .Mkama ametoa mwito kwa wanahisa wote kutumia fursa hii kununua hisa stahiki za kampuni ya Saruji Tanga ili kunufaika na punguzo hili la bei; na kuimarisha uwekezaji wao ndani ya kampuni hiyo.