Wanafunzi wabuni mifumo ya kupunguza foleni na ajali za bodaboda

Dar es Salaam. Katika juhudi za kutatua changamoto zinazolikumba Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, wanafunzi wa shule za sekondari wameibuka na bunifu za kiteknolojia zenye lengo la kupunguza foleni pamoja na ajali zitokanazo na bodaboda.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chang’ombe jijini Dar es Salaam wamebuni mfumo walioupa jina la Digital Traffic Management Programme (DTMP), ambao umeelezwa kuwa na uwezo wa kubaini kwa kutumia akili uende (AI) upande wa barabara wenye msongamano mkubwa wa magari na kuamua muda wa taa za kuongoza magari.

Akizungumza katika kongamano la 15 la wanasayansi chipukizi lililofanyika jijini humo hivi karibuni, mmoja wa wabunifu wa mfumo huo, Marko Marko alisema:

“Mfumo huu ukifungwa kwenye taa za kuongoza magari, unaweza kugundua upande wenye msongamano mkubwa na kutoa muda mrefu zaidi wa taa ya kijani kwa magari kupita, hivyo kusaidia kupunguza foleni.”

Aidha, mbunifu mwenza wa DTMP, Junior Pastor, alieleza kuwa mfumo huo unaendeshwa kwa msaada wa kamera maalum zenye uwezo wa kubaini namba za magari yanayovunja sheria za barabarani kwa kupita wakati taa nyekundu zimewaka. 

Alisema taarifa hizo hutumwa moja kwa moja katika tovuti maalumu kwa ajili ya hatua zaidi.

 “Kwa msaada wa teknolojia hii, tunaamini tukiwezeshwa, tunaweza kusaidia si tu kupunguza foleni, bali pia ajali zinazosababishwa na madereva wasiovumilia taa nyekundu,” alisema Pastor.

Wakati huohuo,  wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Masanga wamebuni kofia maalum ya usalama kwa ajili ya madereva na abiria wa bodaboda. 

Kofia hiyo, ambayo imeunganishwa moja kwa moja na mfumo wa pikipiki, huifanya pikipiki kushindwa kuwaka endapo dereva au abiria hajavaa kofia hiyo.

Edson Yombason, mmoja wa wabunifu wa kofia hiyo alisema: “Tunataka kupunguza majeruhi wa ajali za bodaboda, hasa vichwani. Mfumo huu unahakikisha kuwa bila kuvaa kofia hiyo, pikipiki haiwezi kuwaka.”

Bunifu hizo ni miongoni mwa 45 zilizowasilishwa na wanafunzi kutoka shule mbalimbali nchini katika kongamano hilo lililoandaliwa na Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST).

Katika hotuba yake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa alisema vijana wa Tanzania wana uwezo mkubwa wa ubunifu, lakini changamoto kubwa ni namna ya kuyaendeleza mawazo hayo.

 “Tunahitaji kushirikiana kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa bunifu hizi hazibaki mezani bali zinageuzwa kuwa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazotukabili kama Taifa,” alisema Profesa Kihampa.

Naye Mwanzilishi mwenza wa YST, Dk Gozibert Kamugisha alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa inayowakumba wanasayansi chipukizi ni ukosefu wa majukwaa ya kuonyesha bunifu zao.

“Hili ndilo lililotufanya tuanzishe kongamano hili, ambalo kwa miaka 15 sasa limekuwa jukwaa muhimu la kuwawezesha vijana kuonyesha na kuendeleza bunifu zao,” alisema.

Kongamano hilo lilihitimishwa kwa utoaji zawadi kwa wanafunzi waliobuni mifumo yenye tija zaidi, ambapo Shule ya Sekondari ya St Joseph Cathedral iliibuka mshindi wa jumla kwa mwaka huu.