Haya yatamuepusha mtoto kuzaliwa na maradhi ya moyo

Mwanza/Dar. Wakati takwimu zikionesha kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa na magonjwa ya moyo ikiongezeka, watalaamu wa afya wametoa angalizo kwa wajawazito kuhakikisha wanapata virutubisho, kuepuka matumizi ya pombe na sigara kwa kuwa ndio vyanzo vikuu vinavyochangia maradhi hayo kwa watoto.

Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa katika kila watoto 100 wanaozaliwa, wawili huwa na tatizo la moyo, huku wataalamu wakieleza kuwa wengi hawagunduliki mapema na hufariki wakitibiwa magonjwa mengine ikiwemo kukosa pumzi, kifua kikuu na nimonia.

 Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), jijini Mwanza, Sista Alicia Masenga ametoa kauli hiyo leo, Septemba 29, 2025 kwenye maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika hospitali hapo na kuongeza kuwa vyanzo hivyo huchangia asilimia 20 ya watoto wachanga wanaozaliwa katika hospitali hiyo kupata matatizo ya moyo.

Hata hivyo, kutokana na uhaba wa vifaa, amesema wengi hulazimika kupelekwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Kwa wastani, watoto 20 husafirishwa kila mwezi kwenda JKCI, lakini si wote hufanikiwa kutokana na changamoto za kifedha na bima, hali inayosababisha vifo ambavyo vingeepukika iwapo huduma zingepatikana mapema.

Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto Bugando, Julieth Kabirigi, amesema hali hiyo inaweza kusababishwa na magonjwa wakati wa ujauzito, kisukari, lishe duni, upungufu wa damu, kukosa virutubisho vya msingi, ikiwemo madini chuma na folic acid, pamoja na kukosa dawa za kinga kwa mtoto na magonjwa mengine yanaweza kumshambulia na kusababisha moyo usitengenezeke vizuri.

“Pia unywaji pombe na uvutaji sigara kwa wajawazito ni baadhi ya vitu vinavyoleta changamoto, ingawaje kiwango cha akina mama wanaokunywa pombe na sigara ni kidogo na tunapochukua maelezo ni asilimia chache wanakiri kunywa pombe au kuvuta sigara. Nafikiri kuna kitu zaidi ya sigara na pombe,” amesema.

Dk Kabirigi amesema licha ya kutofanya utafiti wa moja kwa moja, tatizo hilo ni kubwa kwa Kanda ya Ziwa kwa sababu mikoa hiyo imezungukwa na shughuli za uchimbaji madini zinazochochewa na milipuko kwenye migodi na mionzi (radiation), hali inayoweza kuathiri utengenezwaji wa moyo.

“Tunaliona hilo kulingana na watoto tunaowapata kutoka Tarime, Nyamongo, Shinyanga huko Mwadui, Kahama na Geita. Hizi ni sehemu tunazopata watoto wengi wenye changamoto ya matundu kwenye moyo au shida nyingine,” amesema.

Amesema kutokana na changamoto zilizopo kwenye maeneo hayo, ni ngumu kuwahamisha watu, hivyo kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha kunakuwa na huduma bora za uzazi, elimu bora kwa wazazi na jamii kuhusu namna ya kuzuia ugonjwa huo, pamoja na kuhakikisha jamii inajijenga kwa kuwa na uchumi imara ili changamoto ya moyo inapotokea wapate tumaini la kuendelea na maisha yao.

Pamoja na sababu hizo, amesema tatizo hilo pia linaweza kuchochewa na sababu za kurithi (vinasaba) au mtoto kuzaliwa na changamoto za kimaumbile, kwani watoto wa aina hiyo asilimia 50 wanakuwa na shida za moyo.

“Katika hao, asilimia 75 ni matundu kwenye moyo na hayo matundu asilimia 10 ni yale madogo yanayoweza kuziba yenyewe kwa dawa au kwa uangalizi maalumu. Pia, asilimia 10 ni wale wanaohitaji upasuaji wa moyo,” amesema Dk Kabirigi.

Ameshauri tafiti nyingi na za kina zifanyike na elimu itolewe kwa wanawake wanaotarajia kupata watoto, ili wapate lishe bora na kinga za magonjwa mbalimbali.

“Hali ni mbaya japo kuna matumaini, kwa kuwa matatizo ya matundu ya moyo yanatibika. Unajua, ugonjwa wa moyo ukiuwahi mapema, ukaziba tundu, mtoto anapona. Nina watoto wangu wengi ambao wanaendelea vizuri baada ya kuzibwa matundu kwenye moyo,” amesema.

Kila wiki, Idara ya Magonjwa ya Moyo Bugando hupokea watoto 20 hadi 40, sawa na watoto 200 hadi 240 kwa mwezi, huku asilimia 40 hadi 50 kati yao wakiwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa au yanayosababishwa na maradhi mbalimbali.

Dk Masenga amesema changamoto kubwa ni ukosefu wa maabara tiba ya moyo (Cath Lab) ambayo ingeondoa rufaa nyingi na kuokoa maisha.

“Miaka minane iliyopita tulifanikiwa kufanya upasuaji wa moyo wa wazi kwa wagonjwa zaidi ya 100, lakini kwa sasa umesimama kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu kama Heater Cooler, mashine za uchunguzi na rasilimali watu,” amesema Masenga.

Ameongeza kuwa kuanzia mwaka 2007, wagonjwa takribani 2,000 (watoto na watu wazima) wamenufaika kila mwezi na huduma za moyo Bugando, lakini wengi huishia kupata matatizo makubwa zaidi kutokana na kuchelewa matibabu.

Kutokana na hayo, Sista Masenga amependekeza mambo matatu katika utoaji wa huduma za magonjwa ya moyo ikiwemo kufanya mafunzo endelevu, uwezeshaji wa upimaji wa moyo katika vituo vya afya ili kuzuia changamoto zinazosababishwa na kuchelewa kufika katika hospitali za rufaa.

“Kujumuisha huduma za moyo katika utoaji wa huduma za afya na kuendelea kuelimisha jamii,” amesema Masenga.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Lebba, amesema kati ya watu 225,000 waliopata huduma za magonjwa yasiyo ya kuambukiza mwaka 2024 mkoani hapa, 5,126 waligundulika na matatizo ya moyo, wakiwemo waliotibiwa Bugando.

Alitoa wito kwa wananchi kuepuka vilevi, tumbaku, uzito mkubwa, ulaji usiozingatia lishe na kutofanya mazoezi, huku akisisitiza wajawazito kufika hospitali mapema kwa uchunguzi wa awali. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwataka wananchi kulinda afya ya moyo kwa kubadili mtindo wa maisha na kula vyakula vyenye lishe bora.

Baadhi ya wazazi wa watoto waliotibiwa moyo hospitali ya Bugando, akiwemo Dorkas Misango, mkazi wa Igoma, Mwanza, amesema mtoto wake alipelekwa JKCI kwa upasuaji na anaendelea vizuri, lakini akaomba Bugando iwezeshwe upasuaji kufanyika hapo ili kuepusha gharama kubwa za kusafiri.

Naye Joseph Salaganda, mkazi wa Shinyanga, ambaye mtoto wake alipata tatizo la moyo akiwa na miezi sita, amesema familia nyingi hukimbilia tiba za kienyeji kutokana na kukosa uelewa.

“Mwanzoni madaktari walisema ni nimonia, lakini alipoletwa Bugando ikagundulika tatizo ni moyo. Akafanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri. Watoto wenye matatizo haya ni wengi kwenye jamii, lakini wanatibiwa kienyeji na kuumizwa kutokana na kukosa uelewa wa kutosha,” amesema Salaganda.

Miongoni mwa dalili za haraka zinazoainishwa na wataalamu kutambua mtoto mwenye tatizo la moyo ni pamoja na kupumua kwa shida, mapigo ya moyo kwenda kasi, kukohoa mara kwa mara na kifua kisichoisha, nimonia na kuchelewa hatua za ukuaji.

Wataalamu wa afya wanasema watoto wengi wanaozaliwa na matatizo ya moyo mbali na kurithi, idadi kubwa inatokana na kukumbwa na changamoto katika ukuaji wao akiwa tumboni mwa mama yake.

“Baadhi ya chanzo ni ukosefu wa lishe stahili, matumizi ya baadhi ya dawa tiba na matumizi ya vipodozi vyenye kemikali ambayo yanaweza kuathiri ustawi wa ukuaji wa moyo au umbo la moyo au hata ufanyaji kazi wake,” inaelezwa. Dalili nyingine ni mtoto anabadilika rangi, hasa maeneo ya kucha na midomo.

Kwa mujibu wa JKCI, matibabu ya moyo ni hadi Sh30 milioni.

Maradhi mengine ambayo wataalamu wameonya kuathiri moyo, ni shambulio la moyo ambayo matibabu ni Sh6 milioni kuzibua mshipa mmoja, kuwezesha umeme wa moyo kwa kufunga kifaa maalumu ni Sh10 milioni na moyo kushindwa kufanya kazi Sh30 milioni matibabu yake.

Wataalamu wa moyo wamesema asilimia 70 ya magonjwa ya moyo hutokana na shinikizo la juu la damu ambalo hupatikana kwa mtu kutofanya mazoezi, kula vyakula vyenye mafuta mengi na matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Haya yalielezwa leo, Septemba 29, 2025 na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo JKCI, Dar Group, Tulizo Shemu katika maadhimisho ya Siku ya Moyo duniani yaliyofanyika katika taasisi hiyo.

“Moyo unashambuliwa na changamoto mbalimbali ni muhimu mtu akafika kituo cha afya walau mara moja au mbili kwa mwaka, kupima afya yake na wale wanaobainika kuwa na shida watumie dawa,” amesema.

Dk Shemu amesema ilikuwa kawaida miaka ya nyuma watu wenye miaka 70 na kuendelea kushambuliwa na maradhi ya moyo, lakini sasa hali hiyo imebadilika kwani makundi yote yanashambuliwa na maradhi hayo.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema takwimu za wagonjwa wenye shinikizo la damu zimeongezeka kutoka milioni 1.73 mwaka 2023/2024 mpaka milioni 1.77 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 98.

Shinikizo la damu ni hali ambayo presha ya damu inazidi kiwango cha kawaida cha 120/80.

Shinikizo la damu hutokea pale ambapo nguvu ya msukumo wa damu kwenye kuta za mishipa ni kubwa kupita kiasi, hali inayoweza kusababisha uharibifu wa mishipa ya damu na viungo muhimu.

Takwimu za Mfumo wa Ukusanyaji wa Taarifa za Afya Tanzania (DHIS2) zinaonesha ongezeko la wagonjwa kutoka 1,315,000 mwaka 2019/2020 hadi 1,665,019 mwaka 2023/2024.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu ya “Kila pigo la moyo ni maisha, lilinde usilipoteze” na yalihusisha matembezi ya kilometa mbili na huduma za bure za uchunguzi wa moyo na mishipa ya damu.

Taarifa ya nyongeza na Baraka Loshilaa