Shinyanga. Mtoto Sofia Ndoni (3) amefariki dunia kwa madai ya kushambuliwa kwa kipigo sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kukabwa shingo na bibi yake Christina Kishiwa aliyekuwa akiishi naye Mtaa wa Nyakato, Kata ya Nyasubi Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Mtoto Sofia enzi za uhai wake alikuwa akiishi na mtuhumiwa ambaye ni mama mdogo wa mama wa marehemu (bibi mdogo wa marehemu).
Siku ya tukio ambayo ni Septemba 28,2025, mtuhumiwa anadaiwa kumpiga mtoto huyo kwa kutumia fimbo na bomba za maji za plastiki, kisha kumkaba shingo na kumpigiza ukutani kwa tuhuma za kutompa salamu bibi yake baada ya kuamka asubuhi huku akiwa amekojoa kitandani.
Baada ya kipigo cha muda mrefu bibi wa marehemu aliondoka na kuelekea harusini huku akitoa maelekezo kuwa mtu yeyote asijue kilichotokea na endapo mama mzazi wa mtoto atahojiwa na majirani ajibu mtoto ameteleza na kuanguka kwenye vigae (tiles).
Mmoja wa wanafamilia ambaye hakutaka jina lake litajwe, akizungumza kwa njia ya simu leo Septemba 30, 2025, amesema taarifa zilizowafikia kijijini kwao ni kwamba ndugu yao amepata msiba, mtoto ameanguka na kufariki hivyo waandae mazingira ya kuustiri mwili wa marehemu kwa haraka.
Amesema “Sisi tulijua mtoto ameanguka kama tulivyoelezwa, lakini nilipofika nikamkagua mtoto alikuwa na alama za fimbo, nikamuuliza mama yake hataki kusema, alipoona nimeita polisi ndipo akanieleza kuwa mtoto amepigwa na mama Kenedi. Mama Kenedi alitaka mtoto azikwe kimya kimya bila hata nzengo kujua, tukakataa.”
Mmoja wa wapangaji wa nyumba hiyo Jenifa Emanuel amesema siku ya tukio alitoka kwenda saluni huku akiwaacha wanafamilia wa mwenye nyumba wake wakiwa pamoja kibarazani majira ya mchana na aliporudi ndipo akamkuta mama mzazi wa mtoto Sofia akilia na kumweleza kuwa mtoto wake amefariki.
Anasema alipomhoji mama huyo aliogopa kusema ukweli akiogopa kukamatwa na polisi kwa mauaji kutokana na mwenyeji wake ambaye ni Christina (mama Kenedi) kumwambia akilia au kutoa siri kwa majirani atawaeleza polisi kuwa yeye ndiye aliyemuua mwanae na angekamatwa na kufungwa.
Amesema “Asubuhi mida ya saa nne tulisikia mtoto analia kwa muda mrefu, alikuwa anapigwa, baada ya hapo mimi nikaenda saluni, kumbe alimuumiza na akamwambia mamaake mzazi kwamba akiulizwa mtoto imekuwaje, aseme ameanguka kwenye vigae (tiles), vinginevyo atakamatwa na polisi kuwa ameua.”
Amesema ni tabia ya mama mwenye nyumba wake kuwapiga wanafamilia anaoishi nao akiwemo mama mzazi wa marehemu ambaye anamsaidia kazi za nyumbani.
Amesema “Huyu mama ni kawaida yake kupiga ndugu zake, hili siyo tukio la kwanza, kuna kipindi aliwahi kupelekwa polisi kwa kumpiga msichana wa kazi na kumchoma na pasi ya moto na kisu cha moto, huwa anapiga sana. Mimi niliogopa kumshitaki maana ni katili halafu alishaniambia yeye ni kiongozi wa mtaa huu, sijui cheo chake.”
Naye Bakari Fundikira mkazi wa Nyakato amesema, “Nilikuwa napita niko kwenye pikipiki natoka harusini, nilipofika hapa kuna mama wa jirani na nyumba hii akaniita akiwa anaomba masaada kwamba wakamfate mama mwenye nyumba kwa kuwa mtoto ameanguka amepoteza fahamu.”
Amesema baada ya kusogea nyumba ya tukio alimkuta mama mzazi wa mtoto akiwa amem-beba mwanae akiwa amelegea, ndipo akapigiwa simu mama yake mdogo na mtoto ambaye alifika na kubaini kuwa mtoto ameshafariki lakini ana majeraha ya alama za kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Amesema ndipo alipotoa taarifa polisi ambao nao walifika na kuondoka na mwili wa marehemu pamoja na baadhi ya ndugu waliokuwa wamefika wakitokea kijijini.
Amesema “Baada ya kuona mazingira ya utata kwa tukio la mtoto, mama mdogo akaanza kumhoji mama yake mzazi na marehemu Sofia, ambaye naye alikuwa anaishi kwenye nyumba hiyo, ndipo akaeleza kuwa mtoto alichapwa na bibi yake, na yeye aliambiwa asiseme kwani polisi watamfunga kwa mauaji.”
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato, Hussein Mwita amekiri tukio hilo kutokea kwenye mtaa wake na kueleza kuwa uongozi wa mtaa haukupata taarifa kwa wakati kwani baada ya kifo, mtuhumiwa aliandaa mazingira ya kwenda kuzika kijijini kwao pasipo kuujulisha uongozi.
Amesema “Ni kweli hili tukio limetokea kwenye mtaa wangu na mama mwenye nyumba ametokomea kusikojulikana, wakati naingia madarakani nilikuta kumbukumbu za mama huyu kushtakiwa kwa kumfanyia ukatili msichana wa kazi, kesi ikawa polisi, nikweli aliandaa mazingira ya kuusafirisha mwili kwenda kuuzika kijijini kwao kimya kimya.”
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha tukio hilo na kulaani vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya watu, huku akieleza kuwa jitihada za kumpata mtuhumiwa (mama Kenedi ) zinaendelea.
Amesema “Chanzo cha ukatili huu ni marehemu kutomuamkia bibi yake asubuhi alipoamka lakini pia alijikojolea kitandani kwa hiyo bibi akapata hasira na kumtandika hadi umauti. Bibi huyu ametoroka ila tutampata na sheria itafata mkondo wake.”
“Alikuwa akimpiga kwa kutumua fimbo na bomba la maji la plastiki sehemu mbalimbali za mwili wake. Niwakumbushe wanashinyanga kuwa, malezi ya watoto ni jukumu letu sote, tuwalinde.”
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama ulipohifadhiwa mwili huo, Dk Michael Mushi, amesema waliupokea mwili huo usiku wa kuamkia jana Septemba 29, 2025, ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Tulipokea mwili wa mtoto Sofia Ndoni (4), kwa uchunguzi wetu wa awali tulibaini marehemu alikuwa na majeraha yaliyoonyesha alipigwa na kitu kisichokuwa na ncha kali, kichwani, mgongoni, kifuani, tumboni, mikononi na sehemu nyingine za mwili wake na kupelekea kifo chake.”