TFF yatangaza rasmi uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu

KAMATI ya uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza rasmi kuwa uchaguzi mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara  (TPLB) utafanyika Novemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ni sehemu ya mchakato wa kidemokrasia unaolenga kuhakikisha usimamizi wa mashindano makubwa ya soka nchini unakuwa na viongozi wenye uwezo, uzoefu na maono ya kuendeleza mchezo huo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Benjamini Kalume, amesema ratiba ya mchakato mzima tayari imekamilika.

Amebainisha kuwa kuchukua na kurejesha fomu za kugombea uongozi kutaanza Oktoba 2 na kuhitimishwa Oktoba 6, 2025.

Kwa mujibu wa Kalume, nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti mmoja, Makamu Mwenyekiti mmoja, pamoja na wajumbe wa klabu mbalimbali.

Wajumbe hao watahusisha wawakilishi watatu kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara, wawili kutoka NBC Championship na mmoja kutoka First League.

Ada ya fomu kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti imepangwa kuwa shilingi 200,000, huku wajumbe wakitakiwa kulipia shilingi 100,000.

Aidha, Kalume amefafanua kuwa wagombea wa nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti lazima wawe viongozi waliopo katika klabu zinazoshiriki Ligi Kuu, Championship au First League.

“Walengwa wa nafasi hizi kubwa za uongozi ni lazima wawe na nafasi za Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti katika klabu zao. Hii inalenga kuhakikisha uongozi unakuwa na watu wenye uzoefu wa moja kwa moja katika usimamizi wa timu na mashindano,” amesema.

Kuhusu ratiba ya mchakato mzima, Kamati imepanga Oktoba 7 hadi 9 kufanya mchujo wa awali wa wagombea wote.

Baada ya hapo, kuanzia Oktoba 12 hadi 14, itapokea mapingamizi ya rufaa dhidi ya wagombea watakaopitishwa au kuenguliwa.

Hatua ya usaili wa wagombea wote itafanyika Oktoba 18 na 19 na kampeni rasmi zitaanza Oktoba 23 na kumalizika Oktoba 28.

Wakili Kalume ameeleza  kamati yake imejipanga kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa huru, wazi na wa haki kwa kushirikisha wadau wote muhimu wa soka.

Pia aliwataka viongozi wa klabu na wadau wa mpira wa miguu kuhakikisha wanashiriki kwa weledi na kujiepusha na vitendo vitakavyoweza kuathiri taswira ya mchakato huo.