TFS YAANZISHA MIRADI KATIKA VIJIJI VILIVYOPO JILANI NA SHAMBA LA MITI SILAYO

…………….

Wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Shamba la Miti Silayo  lililopo wilayani Chato Mkoani Geita wameishukuru Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuanzisha miradi ya kimaendeleo ikiwemo Zahanati.

Mbali na hilo, pia wamedai kunufaika moja kwa moja kwa kufanya kazi mbalimbali ndani ya shamba hilo.

Wameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Ujenzi wa shule ya Msingi Silayo, Miradi ya maji, Zahanati na utoaji wa ajira za muda mfupi na mrefu ndani ya shamba hilo.

Mingine ni pamoja na ufugaji nyuki,huduma ya miche ya bure pamoja na kuruhusiwa kufanya shuguli za kilimo ndani ya shamba hilo.

Akizungumza na Torch Media, Mwenyekiti wa kijiji cha Butengo, amebainisha kuwa hapo awali kulikuwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na kutembea umbali mrefu kupata huduma ya afya,ukilinganisha na hali ilivyo sasa.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo, Juma Mwita Mseti, amebainisha miradi mbalimbali walioianzisha pamoja na miche ya miti ambayo tayari wamegawia wananchi katika kuendeleza juhudi za kupanda miti na kutunza mazingira

Aidha, Mseti amesema uwepo wa shamba hilo umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii huku akiwahimiza wananchi kujenga tabia ya kutunza mazingira.

Shamba la Miti Silayo lilianzishwa kwa lengo la kurejesha hali nzuri ya mazingira katika hifadhi ya Kahama mkoani Shinyanga na Biharamulo mkoani Kagera baada ya awali maeneo hayo kuharibiwa na shuguli za kibinadamu ikiwemo kukata miti, ufugaji, kilimo cha kuhama hama, kuchoma mkaa na kukata kuni pamoja na ujenzi wa makazi ya kudumu ndani ya hifadhi hiyo.