KIPA wa Mashujaa, Patrick Munthari aliyemaliza na clean sheets 14 msimu uliyopita, amesema pamoja na kuwakubali Yona Amosi wa Pamba Jiji na Djigui Diarra wa Yanga akiwataja kama makipa wenye akili kubwa katika kulinda lango, anapigia hesabu kuweka rekodi mpya msimu huu.
Munthari aliyekuwa mshambuliaji enzi akicheza michuano ya Copa Cocacola kabla ya kugeukia ukipa amesema anaamini msimu huu akikomaa anaweza kuvuka clean sheets aliyoweka msimu uliopita na kufika mbali, huku akiisaidia Mashujaa kufanya makubwa katika Ligi Kuu iliyopo raundi ya tatu.
Kipa huyo amesema mbali na kusaka rekodi hiyo, anakiri amekuwa akiwafuatilia makipa wengine ili kujifunza makubwa akiwataja Diarra na Amosi.
Makipa hao ni miongoni mwa waliomaliza na clean sheets nyingi – Diarra akiwa na 17 akishika nafasi ya pili nyuma ya kipa wa Simba, Moussa Camara aliyekuwa kinara na 19, huku Amos akiwa na 11 na Munthari amewaelezea sifa zao kuu ni kujua kucheza na eneo lao, kupanga timu, kuusoma mchezo, kuanzisha mashambulizi na kutuliza presha pindi mpira unapokwenda golini kwao.
“Nikitulia napata muda wa kuzitazama mechi mbalimbali ili kujifunza vitu tofauti kutoka kwa wengine, hivyo hao makipa wawili niligundua wana sifa nilizozitaja pia wanajiamini kupita kiasi,” amesema Munthari na kuongeza;
“Mbali na hao, wakati nipo ngazi za chini niliyekuwa napenda kumuangalia zaidi na kupenda aina ya uchezaji wake ni kipa wa zamani wa Yanga, Yaw Berko raia wa Ghana, alikuwa mtulivu hata akishambuliwa vipi.”
Kipa huyo alifichua enzi akicheza soka la vijana kupitia michuano ya Copa Cocacola alikuwa mshambuliaji na kilichombadilisha nafasi hiyo ni baada ya kuumia kipa wao, hivyo akaambiwa asaidie kuziba pengo.
“Michuano ya mikoa, Copa Cocacola nilikuwa mshambuliaji, ilipotokea kuziba nafasi ya mtu, makocha waliona nafiti eneo hilo. Inanisaidia kutambua hatari za washambuliaji wanaotumia miguu ya kulia na kushoto, wakiwa na mpira mguuni, najua namna ya kujipanga,” amesema Munthari na kuongeza;
“Kati ya washambuliaji waliokuwa hatari kwangu msimu uliopita ni Prince Dube wa Yanga, aliyemaliza msimu uliopita na mabao 13 na asisti nane, hatumii nguvu ila ana akili kubwa ya kufunga.”