Serikali yaingia makubaliano na Streit Group kutengeneza magari ya jeshi

Kibaha. Serikali ya Tanzania kupitia Kituo cha Teknolojia ya Magari na Mitambo (TATC) cha Nyumbu, Kibaha mkoani Pwani imeingia ubia na kampuni ya Streit Group FZ-LLC kutoka Falme za Kiarabu kwa ajili ya kutengeneza, kukarabati na kuuza magari ya kivita, hatua inayotajwa kuimarisha uwezo wa nchi katika sekta ya viwanda na usalama.

Mkataba huo wa ubia umesainiwa jana Septemba 29, 2025 katika eneo la Nyumbu na unatajwa kuwa wa kwanza wa aina yake barani Afrika, ukiwa na lengo la kuongeza thamani ya teknolojia ya ndani pamoja na kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania, hususan wahandisi na mafundi wenye ujuzi wa kiufundi.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini huo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax aliyekuwa mgeni rasmi, alisema ubia huo ni ishara ya hatua kubwa ya maendeleo na mafanikio ya sera ya uchumi wa viwanda inayoendelezwa na Serikali.

Waziri huyo amesema Watanzania wanapaswa kuhakikisha wanafanya vizuri kwa manufaa ya nchi, kwa kutumia ubia huo kwa umakini, nidhamu na weledi ili kufanikisha ndoto za kujenga nchi yenye nguvu kiuchumi na kiusalama.

Picha matukio mbalimbali ya kusaini mkataba uliofanyika Kibaha Mkoa wa Pwani. Picha na Sanjito Msafiri



Alisema mchakato huo ulianza tangu mwaka 2022 kwa mazungumzo ya pande zote mbili ikihusisha wataalamu na kutokana na kuridhia, hatimaye wamesaini mkataba kisheria.

“Tutaanza kutengeneza magari ya kijeshi lakini kadri tunavyoendelea, tutapanua wigo na yatatengenezwa magari ya taasisi na baadaye tutaenda hadi yatakayouzwa soko la Afrika Mashariki,” amesema.

Amesema hatua hiyo inaakisi uwepo wa mazingira bora yanayoandaliwa na Serikali ili kuvutia wawekezaji kutoka mataifa ya mbali, kuja kuwekeza nchini, hali ambayo si tu kuwa inaimarisha uchumi wa nchi, bali hata kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la TATC, Balozi mstaafu, Wyajonea Kisamba alisema ubia huo utakuwa na mchango mkubwa kwa vijana hasa wahitimu wa vyuo vya ufundi na wahandisi wa Kitanzania.

Picha matukio mbalimbali ya kusaini mkataba uliofanyika Kibaha Mkoa wa Pwani Picha na Sanjito Msafiri



Alisema mradi huo utatoa nafasi kubwa kwa vijana kushiriki moja kwa moja katika teknolojia ya kisasa ya magari na taasisi hiyo itahakikisha ajira na mafunzo ya vitendo yanawafikia Watanzania wengi, ili kukuza uwezo wa ndani na kuondoa utegemezi.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda alisema mradi huo ni nyenzo muhimu kwa usalama wa nchi na unaakisi dira ya kujitegemea kijeshi na kiteknolojia.

Alisema wabia hao watahamisha teknolojia kwa kuwafundisha wazawa, jambo ambalo litaleta manufaa ya kudumu kwa nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Streit Group, Guerman Gouutorow alisema Tanzania imechaguliwa kutokana na mazingira yake ya kiuchumi, kisiasa na kijografia ambayo yanaipa nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha usambazaji wa magari hayo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Ushirikiano huo, pia, unatarajiwa kufungua milango kwa sekta binafsi kushirikiana na TATC katika ubunifu wa teknolojia nyingine zinazohusiana na magari ya usafiri na viwanda vya chuma, hatua inayotajwa kuwa kichocheo cha ajira na ukuaji wa uchumi wa viwanda.


Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwanachi kutoka Mtaa wa Juhudi, jirani na eneo kunakojengwa kiwanda hicho, wameeleza matumaini yao kuwa mradi huo utafungua milango ya fursa mpya za ajira na kuongeza umaarufu wa Tanzania katika ramani ya dunia ya utengenezaji wa magari ya kivita.


Streit Group FZ-LLC ni moja ya kampuni kubwa zaidi duniani zinazojihusisha na utengenezaji wa magari ya kijeshi na yenye uwezo wa kujilinda katika mazingira hatarishi.

Kampuni hiyo ilianzishwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita na makao yake makuu yako Ras Al Khaimah, Falme za Kiarabu. Streit Group inauza magari yake katika zaidi ya nchi 100 duniani, ikiwa na viwanda vya uzalishaji na mabohari katika mabara mbalimbali.


Kituo cha Teknolojia ya Magari Tanzania (TATC), kinachojulikana zaidi kama Nyumbu, kilianzishwa mwaka 1985 kwa lengo la kukuza teknolojia ya magari na mitambo nchini.

TATC kimekuwa kikihusika na utafiti, utengenezaji, ukarabati na ubunifu wa magari maalumu kwa matumizi ya kiraia na kijeshi.