Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Sophia Mwenda (64) na mwanaye wa kiume Alphonce Magombola (39) kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwanafamilia huyo.
Sophia na mwanaye wanadaiwa kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti yake wa kwanza wa kumzaa kwa kumchoma kisu chini ya titi, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba Mosi, 2020 eneo la Kijichi, Wilaya ya Kigamboni.
Washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Beatrice na kisha mwili wake kwenda kuutupa eneo la Zinga, lililopo Bagamoyo mkoani Pwani, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba Mosi, 2020, eneo la Kijichi Wilaya ya Temeke.
Hata hivyo, katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa Kituo cha Polisi Oysterbay, Sophia alikiri kumuua mtoto wake huyo ili asiende kutoa ushahidi katika kesi iliyofunguliwa na baba yake Beatrice ambayo inatokana na Sophia kuuza nyumba iliyopo Mbeya akishirikiana na Alphonce, bila kushirikisha familia.
Nyumba hiyo ya familia iliyopo Mbeya iliizwa Sh45 milioni na Sophia akishirikiana na mwanaye Alphonce walichukua fedha hizo, bila kumpa taarifa mume wake, hali iliyopelekea, Dogras Mwagombola (mume wa Sophia) kufungua kesi mahakamani.
Katika mgao huo wa Sh45 milioni , Sophia alipewa Sh12 milioni ambapo alitoa Sh1 milioni na kumpatia mwanaye Rachel ambaye alikuwa anasoma na kiasi kilichosalia alichukua Alphonce.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Jumanne, Septemba 30, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, aliyepewa Mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi ya mauaji.
Hakimu Mrio alisema, kwa mujibu wa sheria adhabu ya kosa la kuua kwa kukusudia ni moja tu nayo ni kunyongwa hadi kufa.
“Kwa kusema hayo, Mahakama hii ina wahukumu Sophia na Alphonce, kunyongwa hadi kufa na haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo hamjaridhika na adhabu iliyotolewa,” alisema Hakimu Mrio.
Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii