UNAWEZA kusema Singida Black Stars ikikutana na Mashujaa, ina uhakika wa kuondoka na pointi tatu bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa kwani tayari imefanya hivyo mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara.
Ushindi wa bao 1-0 ilioupata Singida Black Stars leo Septemba 30, 2025 dhidi ya Mashujaa na kukaa kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi sita, ulikuwa ni wa tatu tangu timu hizo zianze kukutana Oktoba 4, 2024.
Rekodi zinaonesha msimu uliopita, Mashujaa ikiwa nyumbani Oktoba 4, 2024, ilipoteza kwa bao 0-1 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, kisha ikafungwa tena 3-0, Februari 26 2025 kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
Singida Black Stars inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Miguel Gamondi, katika mechi ya leo iliyochezwa Uwanja wa KMC uliopo Mwenge jiji Dar es Salaam, imepata bao dakika ya 45+5 kupitia Elvis Rupia.
Bao hilo lilikuja baada ya Singida Black Stars kutengeneza nafasi nyingi tangu dakika ya kwanza, tofauti na Mashujaa ambayo muda mwingi safu ya ulinzi ilikuwa bize kulinda lango lao.
Uwepo wa kiungo mkabaji Khalid Aucho, ulionekana kuisaidia Singida Black Stars kutawala eneo la kati, huku Clatous Chama akipandisha mashambulizi kwenda Mashujaa.
Japokuwa kipindi cha pili kilionekana kwa Mashujaa kuongeza umakini zaidi katika eneo la ulinzi na kuweka mipango ya kushambulia, shuti la kwanza lililolenga goli lilikuwa la mshambuliaji Ismail Mgunda aliyefunga mabao mawili msimu uliopita kabla ya kutimkia AS Vita ya DR Congo na kurejea Mashujaa.
Dakika tatu za nyongeza kabla ya filimbi ya mwisho, Mashujaa ilikuwa inapambana kusawazisha ikitengeneza nafasi, lakini bahati haikuwa upande wao, kutokana na Singida Black Stars kulinda vizuri bao lao hilo.
Hii ilikuwa mechi ya tatu kwa Mashujaa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuanza na sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania na kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, zote ikicheza nyumbani Uwanja wa Lake Tanganyika.
Kwa upande wa Singida Black Stars, ni mchezo wa pili ikianza na ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC, kabla ya leo kupata ushindi kama huo mbele ya Mashujaa, mechi zote zikichezwa Uwanja wa KMC.