Dar es Salaam. Jaji mstaafu Joseph Warioba amewataka Watanzania kuendelea kuenzi mazuri yaliyofanywa na Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim ikiwamo kusimamia ukweli, kwa wazalendo kwa nchi, kujali haki za watu na utu.
Warioba amesema hayo leo Septemba 30, 2025 katika kongamano la kwanza la kumbukizi ya Dk Salim Ahmed Salim kama mwanadiplomasia aliyefanya kazi kubwa Tanzania na Afrika.
Kongamano hilo lilibebwa na kauli mbiu ya “Daraja la kimataifa, sauti za Afrika: kuadhimisha urithi wa kudumu wa Dk Salim Ahmed Salim.”
Akizungumza katika kongamano hilo, Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na makamu wa kwanza wa Rais mstaafu, amesema alikuwa miongoni mwa watu waliopata nafasi ya kufanya kazi kwa karibu na Dk Salim jambo lililomfanya kumfahamu vizuri utendaji kazi wake na mpaka sasa hajaona mwanadiplomasia anayeweza kufikia kiwango chake.
Amesema kufuatia namna ya uongozi aliokuwa nao Dk Salim, ilifanya kila mtu kuona kuwa anafaa kuwa kiongozi wa ngazi yoyote nchini na hata Rais wa nchi.
“Hiyo ni kwa sababu alikuwa ni kiongozi aliyeubeba Utanzania, alikuwa Mtanzania wa kweli, alikuwa na dini, kabila cheo lakini vyote aliviweka pembeni na kusimama kama Mtanzania kwa ajili ya nchi yake,” amesema wakati akiwasilisha mada katika kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim.
Licha ya kuwa na nafasi ya juu ya uongozi serikalini, mara zote Dk Salim aliendelea kuwa mnyenyekevu, mwadilifu na hata siku moja hakuwahi kuwa na mbwembwe bali aliheshimu watu na aliitumikia nchi nje na ndani kwa uadilifu.
“Aliheshimu watu na haki zao, aliamini binadamu wote ni sawa, Dk Salim ni mwaminifu na mara zote alisimama kama Mtanzania wala hakupendelea upande mmoja. Kuna wakati kulikuwa na mvutano kati ya Pemba na Unguja, lakini yeye alipenda kuona umoja wa Zanzibar, hata wakati mmoja hakuipendelea Pemba,”amesema Jaji Warioba.
“Kama kuna tatizo la Tanzania bara na visiwani, alikuwa anashughulika kama Mtanzania, kwake cha kwanza alikuwa ni Mtanzania, si anapotoka si kwa dini yake, alijali utu, hata kwenye kazi zake ndani na nje ya nchi aliheshimu yoyote.”
Amesema katika watu aliofanya nao kazi, Dk Salim alikuwa mtu asiyekuwa na tamaa na mara zote alifanya kazi anayopewa kwa uadilifu kupitia maono yake na upeo wake mkubwa katika utendaji wa shughuli mbalimbali.
“Dk Salim angekuwa Rais wa nchi hii, hakuutafuta urais lakini alikuwa anapendekezwa, mimi ni kati ya watu ambao tulikuwa tunaamini kuwa Dk Salim anaweza kuwa Rais tukamshawishi, lakini yeye alisema hawezi kuwa mgombea kama nyumbani kwao hawatamuunga mkono, tulikubaliana na mimi nikaenda Zanzibar kuuliza akashawishika akaingia,” amesema.
Warioba amesema yapo mengi ambayo yamefanywa na Dk Salim yanayopaswa kuenziwa huku akitoa rai kwa taasisi hiyo kuanza kuwajenga vijana wengine ili wawe wana diplomasia nguli kama alivyokuwa Dk Salim kwa kile alichokisema, hadi sasa hajaona mwanadiplomasia wa mfano wake.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Salim Ahmed Salim, Dk Felix Wandwe amesema kongamano hilo linalenga kutambua mchango wa Dk Salim kupitia kazi aliyoifanya ndani ya nchi na nje ya nchi.
“Hilo linaenda sambamba na kuadhimisha urithi wa kudumu ulioachwa na Dk Salim ili vijana waweze kujua mambo mazuri aliyoyafanya wakati wa utumishi wake wa umma ili waweze kuyaenzi.
“Dhamira ya kongamano hili ni kukumbuka yale yaliyofanywa na Dk Salim Ahmed Salim kama mwanadiplomasia aliyefanya kazi kubwa Tanzania na Afrika kwa jumla, lililobebwa pia kama daraja la kimataifa,” amesema Dk Wandwe.
Pia, amesema Dk Salim amekuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia wa Tanzania, aliyefanya kazi katika nyanja ya kidiplomasia ya kimataifa tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960.
Ni mwanadiplomasia nguli aliyehudumu katika nyadhifa mbalimbali duniani na alikuwa Waziri Mkuu wa tano wa Tanzania (1984-1985) na Katibu Mkuu wa nane wa OAU (1989-2001) na Oktoba 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alizindua makavazi ya kidijitali Dk Salim.
Balozi Modest Mero amesema Dk Salim ni mzalendo na mfano wa kuigwa na watu wengi ambaye anapaswa kuenziwa kupitia mazuri aliyoyafanya.