Baada ya kuibuka na ushindi katika mechi nne mfululizo msimu huu zikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imesimamishwa na Mbeya City kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu Bara wakati timu hizo zikishindwa kufungana.
Hii ni mara ya kwanza Yanga inashindwa kupata ushindi baada ya kucheza mechi tano za mashindano msimu huu, huku mashabiki wakimtaka kocha Romain Folz kuondoka kikosini hapo baada ya matokeo hayo.
Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, mashabiki wa Yanga walilipuka wakipaza sauti wakishinikiza Kocha Folz aondoke huku wakisema ‘Hatumtaki! Hatumtaki! Hatumtaki! Aondoke’ huku uongozi wa Yanga ukijibu kelele hizo.

Timu hizo zimekutana leo uwanjani hapo baada ya mara ya mwisho kutoka sare ya mabao 3-3, Juni 6, 2023, ambapo Mbeya City ilitangulia kufunga mabao matatu, Yanga ikasawazisha. Mabao ya Mbeya City yalifungwa na Richardson Ng’ondya aliyepachika mawili na George Sangija, huku Bernard Morison (mawili) na Salum Aboubakar wakiisawazishia Yanga.
Matokeo hayo katika msimu huo 2022-2023, yaliifanya Mbeya City kwenda kucheza mechi za mtoano na kushuka daraja kabla ya kurejea msimu huu 2025-2026.
Msimu huu, Yanga hiyo ilikuwa mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara baada ya kuanza na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Pamba Jiji 3-0, huku Mbeya City ikiwa mechi ya tatu ikianza na ushindi wa 0-1 dhidi ya Fountain Gate na kupoteza mmoja mbele ya Azam kwa mabao 2-0, zote ikicheza ugenini.
Hata hivyo, Yanga ilikuwa na mwenendo mzuri ikiwa na matokeo ya ushindi wa mechi nne mfululizo, ikianza na Ngao ya Jamii ilipoichapa Simba bao 1-0, kisha ikaenda Ligi ya Mabingwa Afrika ikiitandika Wiliete SC mabao 3-0 ugenini na nyumbani 2-0. Pia Ligi Kuu Bara ikiifunga Pamba Jiji 3-0.

MECHI ILIVYOKUWA
Dakika tano za kwanza katika mechi ya leo, Yanga ililisakama zaidi lango la Mbeya City na kuwapa wakati mgumu mabeki na kipa Beno Kakolanya.
Mbeya City iliamka na kuuelewa mchezo na kuamua kufunguka na kufanya mechi kuwa ya kushambuliana, japokuwa Yanga ndio ililishambulia zaidi lango la mpinzani.
Katika dakika 45 za kwanza, Yanga ilipiga kona tatu dhidi ya moja kwa wenyeji, lakini maeneo yote hayakuwa na utulivu katika kutumia nafasi zilizopatikana na kwenda mapumziko bila kufungana.
Mbeya City ilipiga mashuti mawili nje ya lango la Yanga na moja ambalo kipa Djigui Diarra alidaka, huku Kakolanya akiokoa mawili yaliyolenga lango lake na mengine takribani matano yakitoka nje.

Beki wa Mbeya City, Ibrahim Ame alionekana kuwa bora kipindi cha kwanza kutokana na hatari nyingi alizookoa huku Pacome ZouZoua akiwapa misukosuko Mbeya City kwa mashambulizi aliyofanya.
Kipindi cha pili, Yanga ilianza kwa mashambulizi zaidi, ambapo Mbeya City iliamua kuwapumzisha Willy Mwani aliyeumia na kuingia Peter Mwalyanzi, huku Yanga ikimtoa Mohamed Doumbia na kuingia Célestin Ecua.
Pia Yanga ilifanya mabadiliko, ambapo wachezaji Maxi Nzengeli na Duke Abuya waliwapisha Lassine Kouma na Edmund John katika dakika ya 67 huku Israel Mwenda akimpisha Prince Dube dakika ya 79.
MSIKIE FOLZ
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Folz amekubali kukutana na ugumu akieleza kuwa ni sehemu ya matokeo akiahidi kuwa anaenda kusahihisha makosa yaliyojitokeza.
Amesema kwa kuwa ligi inasimama, anaenda kuboresha maeneo yote kuhakikisha timu inafanya vizuri haswa mechi za kimataifa zinazoikabili Yanga akiwatuliza mashabiki kuwa wavumilivu.
“Hatukutarajia kupata matokeo haya ila tunakubali yapo makosa ambayo yalionekana upande wa ushambuliaji kushindwa kutumia nafasi tulizopata, tutatumia mapumziko haya kusahihisha,” amesema Folz.

HII HAPA KAULI YA YANGA
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema wamesikia kelele za mashabiki lakini uongozi unaendelea kufanya tathimini na muda ukifika utaamua iwapo itahitajika la kufanya.
Amewaomba mashabiki kuwa watulivu akieleza kuwa timu yao ni bora na uwanja wa Sokoine umeendelea kuwa mgumu kwao kupata matokeo mazuri.
“Uongozi unaendelea na tathimini kwa hiki kilichosikika kwa mashabiki, tukubali Sokoine kwa historia umeendelea kuwa mgumu kwetu na mambo mengine yatafanyiwa kazi,” amesema Kamwe.