Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imezuia kuhamishwa Sh390.9 milioni kutoka katika benki tatu tofauti, mali ya mtuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi, hadi kesi hiyo itakapoamuliwa.
Benki hizo ni Exim Bank PLC ambayo kuna akaunti yenye Sh110.3 milioni, ABSA Bank Ltd yenye akaunti yenye Sh195.2 milioni na CRDB Bank PLC yenye akaunti yenye Sh59.7 milioni, zote zikiwa na jina la mshitakiwa Amaniel Stanley Lwiva.
Mbali na fedha hizo, lakini Jaji Sedekia Kisanya wa mahakama hiyo Kanda ya Dar es Salaam, ametoa amri inayozuia kuuzwa au kuhamisha umiliki wa magari, viwanja na mali nyingine zinazomilikiwa na washitakiwa wote wanne kati kesi hiyo.
Amri hiyo imetolewa leo Septemba 30, 2025 wakati Jaji Kisanya akitoa uamuzi wa maombi yaliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) dhidi ya washitakiwa wanne, ambao ni Lwiva, Shadrack Chawinga, Alex Ngonyani na Grey Chizala.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuingilia mifumo ya kompyuta ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), kuiba na kuisababishia hasara mamlaka. Kesi hiyo ipo katika Mhakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Maombi hayo ya DPP yaliambatanishwa na kiapo cha Inspekta Yohanah Elisante Wilfred, ambaye ni mchunguzi mwandamizi kutoka ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi wa Jinai (DCI), kitengo cha Uhalifu wa Kifedha jijini Dar es Salaam.
Kulingana na kiapo cha Inspekta Yohanah, Julai 16, 2024, Kaimu Meneja Operations wa TTCL aliripoti katika kitengo cha uhalifu wa kifedha cha Jeshi la Polisi, kuwa kuna watu wameingilia mifumo ya T-Pesa na kuhamisha fedha.
Fedha hizo zilihamishwa kwa njia haramu na za kugushi kwenda kwenye simu mbalimbali za kiganjani za TTCL na taarifa hiyo ilianzisha uchunguzi ambao ulifanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kufunguliwa mashitaka.
Kulingana na kiapo hicho, DPP alidai kuwa upelelezi ulibaini kuwa kati ya Machi 2023 na Oktoba 2024, kinyume cha sheria, mjibu maombi wa kwanza, Chawinga, aliingilia mfumo wa TTCL T-Pesa na kupata laini za simu (sim cards) 77.
Kupitia laini hizo, Chawinga anadaiwa alizihamishia Sh1.5 bilioni ambazo zilitumika vibaya, na sehemu ya fedha hizo zilitolewa kama fedha taslimu na nyingine zilihamishiwa katika akauti za Lwiva na kwenye laini nyingine.
Uchunguzi huo ulibaini zaidi kuwa Chawinga anadaiwa kutumia fedha hizo haramu kujipatia mali vikiwamo viwanja katika eneo la Kigamboni na maeneo mengine katika mikoa mbalimbali, vikiwa na majina tofauti tofauti ya watu wengine.
Pia, kupitia fedha hizo, Chawinga anadaiwa kununua magari BMW 5 Series namba T365 EHF na Mazda CX-5 namba T950 EHU yakiwa na majina tofauti.
Kulingana na kiapo hicho, mjibu maombi wa pili, Lwiva naye anatuhumiwa kujipatia mali kwa fedha hizo haramu, zikiwamo fedha taslimu Sh390.9 milioni, kiwanja eneo la Tuangoma, Temeke na gari aina ya Mazda CX-5.
Kiapo cha Inspekta Yohanah kinadai kuwa uchunguzi zaidi ulibaini mjibu maombi wa kwanza anatuhumiwa alitakatisha sehemu ya fedha hizo na kuhamisha Sh16 milioni kwenda kwa mjibu maombi wa tatu, Alex Jacob Ngonyani.
Ngonyani naye anadaiwa kutumia fedha hizo kuwekeza katika duka la nguo lililopo mtaa wa Mlandizi, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Lakini pia mjibu maombi wa nne, Chizala naye anadaiwa alitumia sehemu ya fedha haramu zilizopatikana katika ‘dili’ hilo kuanzisha duka la nguo na vipodozi Njiapanda ya Himo, katika Wilaya ya Moshi iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Ilidaiwa kuwa wajibu maombi wote wanne hawana chanzo halali cha mapato kinachoweza kuhalalisha kupata mali walizonazo na kwamba wamejihusisha katika kuhamisha na kutoa fedha hizo ili kuficha chanzo halisi cha fedha hizo.
Maombi hayo yalipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa Septemba 24, 2025 mbele ya Jaji Kisanya, DPP aliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Juma Mahona na wajibu maombi hawakuhudhuria kwani lilikuwa shauri la upande mmoja, ex-parte.
Katika uamuzi wake alioutoa leo Septemba 30, 2025, Jaji Kisanya amesema maombi hayo ya DPP yana mashiko na tuhuma dhidi ya wajibu maombi zinaangukia katika makosa makubwa (serious offence) chini ya sheria ya mazao ya uhalifu (Poca).
Jaji amesema amezingatia kuwa wajibu maombi au washtakiwa bado hawajatiwa hatiani na kesi inayowakabili bado iko katika upelelezi na kwamba, ili mahakama itoe amri ya kuzuia mali hizo, inapaswa kuzingatia mambo mawili.
Moja ni lazima kuwepo na sababu za kuamini kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo na pili mali zinazobishaniwa ni lazima ziwe zina viashiria au mlalamikiwa lazima awe amepata manufaa kutokana na kosa hilo analoshitakiwa nalo.
“Kama ilivyoonyeshwa, wajibu maombi wanadaiwa kuingilia mfumo wa TTCL T-Pesa na kujipatia laini 77 ambazo waliziingizia Sh1, 507, 771, 030. Baadhi ya fedha hizi zilitolewa taslimu na zingine zilihamishiwa benki mbalimbali,” ameeleza Jaji.
Kutokana na ushahidi huo, Jaji amesema anaona zipo sababu zenye mashiko za kuamini huenda wajibu maombi walitenda kosa hilo ambalo linahitaji ushahidi kuthibitishwa wakati shauri hilo litakapoanza kusikilizwa mahakamani.
Hivyo Jaji ametoa amri tano za zuio ambazo ni kuwazuia wajibu maombi, mawakala wao au mtu yeyote anayewajibika kwa niaba yao, kuuza, kuhamisha umiliki au kukodisha mali ambazo zinadaiwa ni za wajibu maombi hao wanne.
Mali hizo ni pamoja na viwanja, magari na bidhaa za dukani na fedha taslimu zilizopo katika benki tatu nchini na pia amri ya kuzuia benki hizo kuhamisha au kutoa fedha hizo kutoka kwenye akaunti za mjibu maombi wa pili.
Mbali na amri hiyo, Jaji ametoa zuio kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kamishna wa Ardhi na wakurugenzi wa Halmashauri vilipo viwanja wa wajibu maombi, kutohamisha umiliki wa viwanja hivyo.