Mbeya. Mgombea ubunge Uyole, Mkoa wa Mbeya, Dk Tulia Ackson amesema endapo akipata ridhaa ataondoa vumbi kwa kuja na mkakati wa ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami ili kurahisha shughuli za kiuchumi.
Katika hatua nyingine amesema atahakikisha anaondoa changamoto ya tatizo la mgawo wa maji kwa hususani kwa wananchi waishio jirani na Shule ya Sekondari Iduda ambako kuna mradi wa kisima kirefu chenye uwezo wa kuhudumia kaya nyingi.
Dk Tulia amesema hayo Jumatatu Septemba 29,2025 kwenye mkutano wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu sambamba na kuomba kura kwa wananchi.
“Serikali ya CCM imekuja kivingine kwa kazi ya kuleta maendeleo ya wananchi wa Iduda, nimepata ombi lenu la ubovu wa barabara za mitaa na maji nitakuja na suruhisho endapo mtatupigia kura za kishindo Oktoba 29, mwaka huu,” amesema.
Amesema CCM, ikipata ridhaa itabadilisha taswira ya Uyole ikiwepo uwezeshaji wananchi kiuchumi, sekta ya kilimo, ujenzi wa miundombinu ya afya hususani majengo ya mama na mtoto nchi nzima.

“Hayo yote yanapatikana Chama cha Mapinduzi (CCM), ambayo yapo kwenye utekeleza wa ilani ya uchaguzi 2025, 2030 sasa ili kuyapata Oktoba 29, mwaka huu wananchi mkatiki mafiga matatu kwa Rais Samia Suluhu Hassn, Dk Tulia na Diwani wenu Joseph Emmanuel, “amesema.
Katika hatua nyingine amesema kwenye sekta ya elimu kata ya Iduda Serikali imefanikisha kujenga miundombinu ya vyumba vya madarasa, mabweni ya kisasa ,ujenzi wa kisima cha maji na kupandisha kidato cha tano na sita.
“Awali wanafunzi wa pembezoni waliokuwa wakichaguliwa kujiunga kidato cha tano walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu,lakini baada ya mimi kuwa mbunge Mbeya mjini nilitoa ombi kwa Rais Samia ambaye alitoa fedha za ujenzi,” amesema.
Amesema lengo la Serikali ni kuona wananchi wake wanapata huduma stahiki kwa wakati ikiwepo huduma ya maji safi na salama, elimu, afya barabara na nishati ya umeme.
Dk Tulia amefafanua kuwa kufuatia uwekezaji wa miundombinu kwenye sekta ya elimu hakuna mzazi atakaye takiwa kuchangia fedha za madawati na ujenzi vyumba vya madarasa kwa wanafunzi watakao jiunga kidato cha kwanza mwaka 2026.
“Hakuna mtoto atakaye changia madarasa wala madawati tayari serikali imetekeleza kwa vitendo kila shule nchini ,lengo ni kuwatua mzigo wazazi na walezi sambamba na kuja na dira ya mpango wa 2025/2050 wa utoaji elimu bora,” amesema.
“Serikali imeondoa michango kwa wanafunzi watakao chaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2026, sambamba kusaidia mahitaji ya sare hususani mpango wa bima ya afya kwa wote kwa kaya zisizo jiweza,” amesema.
Wakizungumza mara baada ya kuhitimisha mkutano wa kampeni wamesema hatua ya Serikali kuondoa michango kwa elimu ya sekondari imewatua mzigo mkubwa wazazi.
“Kimsingi tunaona mwanga kwa Serikali ya CCM kama ilani ya uchaguzi 2025, 2030 itasimamia mwelekeo huo jambo ambalo litawezesha wazazi kusimamia kiwango cha taaluma kwa watoto,” amesema Subiraga Haule.
Amesema awali wazazi wengi walikuwa wakikwepa kuwa endeleza watoto elimu ya sekondari kutokana na michango holela na kulazimika kuwapeleka vyuo vya ufundi kupata ujuzi, lakini ametoa angalizo Serikali kusambaza walaka wa katazo hilo mashuleni.
Diwani Kata ya Iduda, Joseph Emmanuel amewataka wananchi ifikapo Oktoba 29, mwaka huu kujitokeza kwa wingi kupiga kura kuchagua wagombea nafasi ya Rais, wabunge na madiwani ili kuwezesha kufikiwa na maendeleo.