Mbeya. Mgombea ubunge Uyole, Dk Tulia Ackson amewahakikishia wananchi wa Kata ya Iduda Jiji la Mbeya, kuondokana na adha ya maji na mgawo uliopo kufuatia Serikali kuja na suruhisho la kudumu la mradi wa kimkakati kutoka chanzo cha Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe.
Dk Tulia amesema leo Jumatatu Septemba 29,2025 kwenye mkutano wa kampeni kuomba kura za wagombea wa nafasi ya Rais ,wabunge na madiwani sambamba kueleza utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020-2025.
Amesema Serikali ilitoa Sh119 bilioni kutekeleza ujenzi wa mradi wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira ambao ni miongoni mwa miradi iliyomo kwenye ilani ya uchaguzi 2020-2025.
“Ndugu zangu wana Uyole nyie mna bahati wakati nipo Mbeya Mjini mambo mengi nimefanya nikiwa na kata 36 ,lakini kutokana na heshima kubwa ambayo mlitupa Mimi na Rais Samia Suluhu Hassan kutupigia kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020 ndio maana tumerejesha heshima ya kuleta maendeleo,” amesema.
Ametaja baadhi ya miradi iliyopo katika kata hiyoni pamoja na kupandisha hadhi shule ya Sekondari Iduda kuwa na kidato cha tano na sita,ujenzi wa mabweni, kisima cha maji na kupandisha hadhi kituo cha afya Igawilo kuwa Hospitali ya Wilaya.
“Hapa Iduda CCM, tumerejesha heshima mlituheshimisha Oktoka 2020 lazima nasi tuwashike mkono kwa kuleta maendeleo makubwa,” amesema.
Amesema Serikali inakuja na mpango mkakati wa dira mpya ya elimu ya mwaka 20/50 itakayo lenga kuboresha ubora wa elimu utakaosaidia walimu kuwa mbinu na ufundishaji wanafunzi na sio kukalilisha.
“Yapo mapinduzi na makubwa yanakuja katika sekta ya elimu Serikali imejipanga kuona watoto mashuleni hawakalili bali wanaelewa vyema kutokana na ujio wa nyenzo na mbinu za ufundishaji,” amesema.
Katika hatua nyingine amesema akipata ridhaa watashirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya Uwsa), kuona namna ya kufunga mabomba ya maji ardhini kusukuma maji kutoka kisima cha Shule ya Sekondari ya Iduda kuhudumia jamii inayo zunguka,”amesema.
“Wana Iduda Oktoba 29, 2025 tukapige kura mkachague mgombea urais Samia Suluhu Hassan na mimi mbunge wenu Dk Tulia Ackson ili kuwaletea mabadiliko ya kweli katika nyanya mbalimbali,” amesema.
Amesema Serikali ya CCM wamejipanga kufanya kazi moja ya kufikisha huduma muhimu kwa Watanzania sambamba na uwekezaji wa miundombinu ya majengo ya mama na mtoto nchi nzima.
Mgombea udiwani Kata ya Iduda, Joseph Emmanuel amesisitiza kumuomba mgombea ubunge Uyole, Dk Tulia kuboresha miundombinu ya barabara atakapopata ridhaa kuchaguliwa ili kuwezesha wananchi kusafirisha mazao na mchanga kutoka maeneo mbalimbali kutokana na miundombinu mingi kuwa chakavu.