Mufindi. Kanisa Katoliki la Jimbo Mafinga limetoa ufafanuzi kuwa Padri Joardan Kibiki wa kanisa hilo aliyedaiwa kujiteka, amebainika kuwa alipata msongo wa mawazo baada ya kupata hasara ya hasara ya Sh3.5 milioni kwenye biashara ya, tandaoni (eBay).
Ufafanuzi huo umetolewa leo Septemba 30, 2025 na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga, Vincent Mwagala kwa waandishi wa habari, kuwa padri huyo alipata tatizo hilo kutokana na hali aliyokuwa anapitia.
Kwa mujibu wa Askofu Mwagala hali ya unyongefu inaweza kumtokea mtu yeyote yule kutokana na hali ya kimaisha ambayo anakuwa anapitia, hivyo kama kanisa kwa sasa linaangilia afya ya padri huyo ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.
Amesema Septemba 26, 2025 baada ya kuzungumza naye na kuhisi hakuwa vizuri, waliamua kumpeleka Hospitali ya Rufaa Tosamaganga kwa ajili ya kuangaliwa afya yake na kubainika kwamba ana unyongefu (depression), hivyo kuanzishiwa matibabu.
Pia, amesema hali hiyo ilichangiwa baada ya padre huyo kugundua kuwa amepata hasara ya Sh3.5 milioni kwenye biashara ya mtandaoni (eBay).
“Alipata hisia kwamba ameibiwa pale alipombiwa atume fedha nyingine kinyume na makubaliano ya awali,” amesema.
“Lengo letu si kuituhumu kampuni ya (ebay) kuwa ni kampuni ya wizi, la asha. kwa sababu baada ya kuifuatilia tumegundua ni kampuni ambayo imeasajiliwa kihalali huko nchini Marekani na inafanya biashara ya mtandaoni, bila shaka kama biashara yoyote inavyoweza kuingiliwa na watu wenye nia ovu, kwani alijisajili kama ajenti (wakala) na kuanza kutafuta maajenti (mawakala) wengine.
Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo ambazo Padri Kibiki alihisi amepata hasara, Sh500,000 alikuwa ameziazima kwa Paroko, Padri Isaac; Sh1.5 milioni alikuwa ameziazima kwa Mhasibu wa Jimbo la Mafinga, Padre Godwin Maliga huku Sh1.5 milioni zilikuwa fedha zake mwenyewe.
“Hivi naweza kuona kwa kweli hakuwa na madeni makubwa kiasi hicho, kwa hali ya kawaida na mtu mwenye afya ya akili asingeweza kutelekeza porini gari lenye thamani ya Sh25 milioni,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi kwa kuzingatia hali ya padri huyo limefuta tuhuma zake na kumwachia huru kutokana na kosa lililokuwa linamkabili la “kusambaza taarifa za uongo kuwa ametekwa wakati alikuwa amejiteka mwenyewe.”
Hata hivyo, Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbia kuzungumzia suala hilo, amemtaka mwandishi asubiri taarifa rasmi kwa kuwa alikuwa nje ya mkoa.
Askofu Mwagala pia amesema kwa mujibu wa Sheria za Kanisa, jinai au madai yanayomhusu padri binafsi si ya kanisa, bali ni yake mwenyewe.
Hata hivyo, amesema ni wajibu wa kanisa kutafuta ukweli wa tuhuma bila kuingilia kazi ya vyombo vya uchuguzi vya Serikali.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limemaliza kazi yake na kubaini padri huyo hana kosa la kujibu, hivyo kwa sasa wanaendelea kushughulia afya ya padri huyo ili arudi kwenye hali yake.
“Kwa sasa kipaumbele chetu ni afya ya padri wetu, hivyo niwaombe mapadri, watawa na waumini wote kwa ujumla tumuombee padri wetu aweze kurudi katika afya yake ya akili na utulivu, kisha mambo mengine yataendelea,” amesema.
Septemba 24, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alitoa taarifa kuhusu padri huyo aliyedai kutekwa, kwamba alitoa taarifa za uongo kupitia mtandao wa WhatApp akidai ametekwa na kusafirishwa kuelekea Mbeya.
Hata hivyo, alisema baada ya uchuguzi wa polisi ilibainika alikuwa amejiteka na kusafiri hadi Wilaya ya Mbalizi, Mkoa wa Mbeya.