Dar es Salaam. Watafiti wa masuala ya kilimo nchini wameonya matumizi ya nafaka kama mbegu, wakisema ni muhimu wakulima kununua mbegu bora ili kupata mavuno ya kutosha.
Wamesema mkulima anapotumia mbegu bora na kupata mazao mengi, halafu baadaye kutumia mazao yaliyotokana na mbegu hizo kama mbegu na kurejea kuotesha, si sahihi.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 30, 2025 jijini Dar es Salaam na Mtafiti wa Masuala ya Kilimo na Mratibu wa Biotechnology Society of Tanzania (BST), Dk Ammarold Mneney, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari namna ya kuandika habari za sayansi
Semina hiyo imeratibiwa na Jukwaa la Bioteknolojia ya Kilimo (OFAB) chini ya ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika (AATF) iliambatana na utoaji wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari za sayansi.
“Ni lazima watu wapande mbegu zilizothibitishwa, huwezi kuvuna mahindi yako na kuyafanya mbegu; lazima utapata mazao yaliyoduni, ukitaka kuwa mkulima wa kawaida lima nafaka, lakini kama unataka faida, nenda kanunue mbegu bora zilizoongezewa ubora,” amesema Dk Mneney.
Amesema dhana iliyopo kwenye jamii kuwa mbegu za asili zinapotea kutokana na mbegu zilizoongezewa ubora kuoteshwa, haina ukweli wowote, kwa kuwa uboreshaji wa mbegu haumaanishi wataalamu wanakwenda kuchukua mbegu maabara.
Amefafanua kuwa mbegu zilizoongezewa ubora maana yake ni kuwa wataalamu wanachukua mbegu inayokosa sifa fulani na kuongeza sifa hizo ili iwe na uzalishaji mkubwa au kuhimili magonjwa.
“Mtafiti anasikiliza changamoto za mkulima na kwenda kuongeza sifa ambazo hazipo kwenye mbegu husika na kuzileta. Sasa ukipanda ambazo hazijaongezewa ubora, itaota lakini mazao yataendelea kupungua kama ilivyokuwa kabla mbegu haijaboreshwa.
Hii ni kwa sababu ule ubora ulioongezewa unapotea, kwa hiyo unapaswa kupanda mbegu mpya kila unapolima,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu, amesema tume hiyo imetumia Sh40 bilioni katika kipindi cha miaka 15, kufadhili utafiti na ubunifu mbalimbali wa kisayansi na kiteknolojia zenye kutatua changamoto za jamii.
Amesema fedha hizo zimesaidia kuibua matokeo makubwa ikiwemo kuingizwa sokoni kwa mbegu 12 mpya zinazostahimili ukame, ambazo zinasaidia wakulima kuongeza tija na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Aidha, zaidi ya wakulima laki mbili wamefikiwa na kupewa elimu kupitia tafiti na bunifu hizo, huku kiuatilifu cha Kanintangaze kikiwa miongoni mwa bidhaa zilizozalishwa chini ya COSTECH na kwa sasa kinatumika na kufanya vizuri sokoni.
“Tumefadhili tafiti mbalimbali zenye tija kwa jamii, mfano, miaka mitano iliyopita tuliwezesha upatikanaji wa vifaa vya haraka vya kupima malaria ambavyo vilisambazwa katika mikoa saba,” amesema.
Mbali na sekta ya kilimo na afya, COSTECH imeendelea kusaidia vijana wabunifu kupitia vituo 20 vya ubunifu vilivyopo nchi nzima, ambapo zaidi ya wabunifu 50 wanapata msaada wa kitaalamu na kifedha.
Aidha, vyuo vikuu vimekuwa vikipewa ufadhili wa miradi ya ubunifu ikiwemo Sh400 milioni zilizotolewa miaka iliyopita kusaidia tafiti hizo.
Kwa upande wake, Mtafiti wa Sayansi za Kilimo kutoka Kenya, Dk David Tarus amesema ni muhimu kuandaa mazingira rafiki ya tafiti yenye kutambua na kuthamini mchango wa wanahabari katika kuripoti habari za kisayansi.
Amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kusaidia jamii kuelewa tafiti na teknolojia mpya, hivyo ni jukumu la watafiti kushirikiana nao kwa karibu ili taarifa za kisayansi ziwafikie wananchi kwa lugha rahisi na sahihi.