Jinsi mama na mwana wavyohukumiwa kunyongwa hadi kufa, baada ya kuua mwanafamilia

Dar es Salaam. Ukimya ulitawala leo katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya Sophia Mwenda (64) na mwanae wa kiume, Alphonce Magombola (39) kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Washtakiwa hao wamehukumiwa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Beatrice Magombola, binti wa mama huyo.

Hukumu hiyo imetolewa leo Septemba 30, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, aliyepewa Mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo ya mauaji, ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 23 dhidi ya washtakiwa hao.

Sophia na mwanawe wanadaiwa kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti wa kwanza wa Sophia, kwa kumchoma kisu chini ya titi, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba mosi, 2020 eneo la Kijichi, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.

Washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Beatrice na kisha mwili wake kwenda  kuutupa eneo la Zinga, Bagamoyo mkoani Pwani.

Katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa Kituo cha Polisi Oysterbay, Sophia alikiri kumuua mtoto wake huyo ili asiende kutoa ushahidi katika kesi iliyofunguliwa na mumewe, Dogras Mwangombola (baba yake Beatrice), ambayo ilitokana na mama huyo kuuza nyumba iliyopo Mbeya, akishirikiana na Alphonce, bila kuishirikisha familia.

Mshtakiwa Alphonce Magombola na mama yake mzazi Sophia Mwenda, wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.



Inadaiwa kuwa nyumba hiyo ya familia iliyopo Mbeya iliuzwa Sh45 milioni na Sophia akishirikiana na Alphonce walichukua fedha hizo, bila kumpa taarifa mume wake, hali iliyopelekea, Mwagombola (mume wa Sophia) kufungua kesi mahakamani.

Katika fedha hizo, Sophia alipewa Sh12 milioni ambapo alitoa Sh1 milioni na kumpatia bintiye Rachel ambaye alikuwa anasoma na kiasi kilichosalia alichukua Alphonce.

Akipitia ushahidi wa mashahidi 23 wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo, hakimu Mrio amesema, hakuna aliyethibitisha kwa macho kwa kuona washtakiwa wakitenda kosa hilo, lakini ushahidi uliopo mahakamani ni wa kimazingira, ambao pia una kanuni zake kwamba hakutakiwi kukatika chain (mnyororo) wakati wa kuuthibitisha.”

“Ushahidi wa Jamhuri ulionyesha kuwa mwili uliokotwa katika eneo la Zinga huko Bagamoro na kupelekwa kuchunguzwa na baadaye ulizikwa na Halmashauri ya Bagamoyo,” alisema Hakimu Mrio

Akiendelea kupitia ushahidi huo, amesema washtakiwa waliunganishwa na tukio hilo la mwili kuokotwa eneo la Zinga baada ya kukamatwa na kuhojiwa na ilionyesha kwamba, katika maelezo yao ya onyo walikiri kuua na kwenda kuutupa mwili huo eneo la Zinga.

Hakimu Mrio, amesema pia askari aliyetoa ushahidi ambaye pia alichukua maelezo yao ya onyo, kupelekwa eneo la tukio na kuhusianisha na mwili uliokotwa eneo la Zinga, Bagamoyo ambapo walifukua kaburi na kutoa mabaki ya mwili na madaktari walichukua taya na kwenda kupima sampuni hiyo na kuoanisha na vinasaba vya baba mzazi wa Beatrice.

“Baada ya taya kupelekwa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, walipooanisha vinasaba vya baba mzazi wa Beatrice, ulibainika kuwa mwili huo ulikuwa ni wa bintiye,” alisema Hakimu Mrio.

Katika ushahidi wa daktari aliyepima mwili wa Beatrice na kuangalia chanzo cha kifo pamoja na ripoti aliyoitoa,  imeoana na maelezo ya onyo ya washtakiwa jinsi walivyotekeleza mauaji ya Beatrice.

“Kwa mujibu wa ushahidi, hakuna ubishi kuwa Beatrice aliuawa na waliomuua ni watu ambao wapo hapa mahakamani, na hakuna ubishi kuwa baada ya kuua, walienda kuutupa mwili wa Beatrice, hivyo ni dhahiri kuwa walikuwa na nia mbaya,” amesema Hakimu Mrio.

“Hivyo, kwa ushahidi huo wa kimazingira, mahakama hii inawatia hatiani washtakiwa wote kwa kosa hili la mauaji ya kuua kwa kukusudia,” amesema Hakimu Mrio.

Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi ni Mzee Magombola, baba wa marehemu Beatrice, aliyedai mara ya mwisho kuongea na binti yake ilikuwa Desemba mosi, 2020 na walizungumza kuhusu kesi aliyoifungua mahakamani kutokana na Sophia kuuza nyumba ya familia iliyopo Mbeya.

Na kwamba Beatrice alitakiwa kwenda kutoa ushahidi Desemba 7, 2020 huko mkoani Mbeya.

Magombola ambaye ni mhadhiri mstaafu wa Chuo cha Tengelu, alidai alimuoa Sophia mwaka 1986, na walibahatika kupata watoto wanne ambao ni Beatrice, Alphonce, Rachel na Deslius @Mwila na walitalikiana mwaka 2008.

Alidai taarifa za kifo cha Beatrice alizipata mwaka 2022, kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam na kipindi hicho, Beatrice na mtoto wake walikuwa wakiishi na Sophia.

Hata hivyo, mwaka 2022, alipigiwa simu na mtoto wa kaka yake aitwaye Alice na kumweleza  kuwa ameona katika mitandao ya kijamii kwamba Alphonce anachangisha fedha kwa marafiki wa Beatrice waliosoma wote Uganda, wamchangie kwa sababu anaumwa sana na amelazwa hospitalini Afrika Kusini, taarifa ambazo hakuwa nazo.

Alidai, baada ya muda alipigiwa simu na Polisi Kituo cha Oysterbay na kumweleza, Beatrice ameuawa na walitaka aende akatoe maelezo kuhusu anachokifahamu.

Mwaka 2022, Magombola alichukuliwa sampuli kwa ajili ya kipimo cha vinasaba, na aliongozana na Polisi kufukua mwili wa Beatrice katika makaburi ya Bagamoyo eneo la Ukuni.

Baada ya taratibu za polisi kukamilika, Novemba 2023, waliomba kibali cha mahakama kuruhusu kuzika mwili wa Beatrice kijijini kwao Masimbwe, Igelango Wilaya ya Njombe na waliruhusuwa.

Jamhuri yaomba adhabu kali

Awali, kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daisy Makakala ametoa sababu tano kwa nini mahakama inatakiwa itoe adhabu kali.

Sababu ya kwanza, amesema namna washtakiwa walivyofanya mauaji ni kwa kutumia kisu, silaha ambayo ina ncha kali na walithibitisha nia ya kutenda kosa.

“Pili, kutokana na sehemu waliyomchoma kisu Beatrice (chini ya ziwa la kushoto) washtakiwa hawa walionyesha ni dhahiri nia yao ni mbaya,” alidai Makakala na kuongeza;

“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa hawa baada ya kutupa mwili wa Beatrice, Zinga na kusema uongo, walijipatia pesa kwa udanganyifu kutoka kwa watu  mbalimbali wakitoa taarifa za uongo kuwa Beatrice ni mgonjwa, na inaonyesha kuwa hawakujali wala kuwa na maumivu ya damu ya Beatrice iliyomwagika,” alidai.

Wakili Makakala aliomba mama na mwana huyo, wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa washtakiwa wengine na watu wengine katika jamii wanaoweza kutenda makosa kama hayo.

“Na watu wengine waweze kujua kuwa hata mama mzazi au ndugu wa damu anaweza kukutendea unyama kama huu, hivyo tunaomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwao na kwa wengine” alidai Wakili Makakala.

Kwa upande wa utetezi, Wakili Hilda Mushi alisema hana cha kusema kwa kuwa sheria ipo wazi na adhabu ya kosa hilo ni moja, hivyo hana cha kuzungumza.

Kwa upande wake Wakili Godwin Fissoo anayemtetea Sophia, alidai kuwa anaomba aingizwe kwenye rekodi ya mahakama kuwa anakusudia kukata rufaa.

Hakimu Mrio baada ya kusikiliza shufaa za pande zote mbili, alikubaliana na maombi na sababu za Jamhuri.

Alisema mujibu wa sheria, adhabu kwa kosa la mauaji ni moja tu nayo ni kunyongwa hadi kufa na mikono ya majaji na mahakimu imefungwa na sheria na kipengele hicho cha adhabu ni kigumu, lakini ni suala lililowekwa kwa mujibu wa sheria.

“Hivyo, washtakiwa wote wawili nawahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kila mmoja,” amesema hakimu Mrio.

Licha ya kutolewa adhabu hiyo, ndugu wachache waliojitokeza mahakamani hapo walionekana kawaida, tofati na hukumu nyingine za mauaji zinapotolewa, ambapo ndugu, jamaa na marafiki huangua vilio.

Lakini, pia hata washtakiwa hao, baada ya kuhukumiwa adhabu hiyo, ndani ya kizimba cha mahakama ya wazi namba moja, walionekana kawaida na wakajifunika nguo usoni.