Dk Nchimbi aahidi kumaliza tatizo la barabara Ukonga, Kivule

Dar es Salaam. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi kusimamia vyema kutatua changamoto ya barabara katika majimbo ya Ukonga na Kivule.

Pia, ameahidi chama hicho kikichaguliwa, kitajenga masoko mawili Gongo la Mboto na Kivule ili kukidhi mahitaji ya wananchi na wafanyabiashara wa maeneo hayo.

Dk Nchimbi amewaambia wananchi majimbo hayo kwamba ahadi hizo zitatekelezwa iwapo watajitokeza kwa wingi Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kuwapigia kura wagombea wa CCM wa udiwani, ubunge na urais.

Mgombea mwenza huyo amesema hayo leo Jumatano, Septemba 30, 2025 katika mkutano wa kampeni, uliofanyika Uwanja wa Kampala Relini, ukihusisha majimbo ya Ukonga na Kivule. Ojambi Masaburi ni mgombea ubunge wa Kivule na Jerry Silaa anagombea tena Ukonga.

Jimbo la Kivule limezaliwa kutoka Ukonga, baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuligawa.

Ahadi ya barabara, ameitoa baada ya Silaa kueleza changamoto hiyo na kumwomba Dk Nchimbi kuiangalia kwa jicho la kipekee kwani wananchi wanahangaika.

Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo, wamedhamiria kutekeleza ujenzi wa barabara kama zilizong’ang’aniwa na mbunge wenu, Silaa na Serikali ya CCM inakwenda kuzifanyia kazi.

Baadhi ya barabara ambazo Dk Nchimbi ameahidi kujengwa kwa kiwango cha lami na changarawe ni za Pugu – Majohe, Mombasa- Kivule, Pugu Mpakani – Majohe – Kigogo Fresh na barabara ya Chuo cha Kimataifa cha Kampala.

Barabara zingine ni ya Bonyokwa- Majichumvi – Kimanga, Segerea- Kanisa la KKKT, Kifuru- Pugu Stesheni na kukamilisha ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka.

Kuhusu masoko yaliyoombwa na Silaa, Dk Nchimbi amesema: “Kuboresha masoko yetu, tuliyonayo yakarabatiwe na yafanane na ya Ukonga na ombi la mgombea wenu ubunge la masoko mapya, tutakwenda kujenga Chanika na Gongo la Mboto.”

Katika afya, Dk Nchimbi ameahidi ujenzi wa hospitali mpya yenye hadhi ya wilaya, ujenzi wa vituo vipya vitatu ambapo huduma haijafikiwa na kukifanyia upanuzi Kituo cha Afya Chanika.

Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo wanakwenda kujenga madarasa mapya 240 katika shule za msingi na 304 ya sekondari ili kupunguza msongamano darasani kwa wanafunzi.

Dk Nchimbi amegusia mikopo ya asilimia 10 ya wanawake, vijana na wenye ulemavu akisema utaratibu wa mwanzo haukuwa mzuri lakini baada ya kusimamishwa na Rais Samia na kurejea tena kupitia benki, itaondoka kasoro zilizokuwepo.

“Tunakwenda kusimamia vizuri mikopo ya asilimia 10, kwani ilikuwa inatolewa kwa ubaguzi na upendeleo. Rais Samia akasema hakuna usawa, ukasimamisha na utaratibu mpya ukaanzishwa na katika siku 100 za mwanzo, Sh200 bilioni zitatolewa ili zisaidie wajasiliamali wadogowadogo,” amesema.

Dk Nchimbi amesema amefurahi kupata mapokezi mazuri wilayani Ilala yenye majimbo manne ya Ukonga, Kivule, Segerea na Ilala.

“Leo naingia wilaya yangu, kwa sababu wazazi wangu wanatoka Tabata, kwa hiyo mmenilindia heshima yangu.”

Akimnadi Ojambi Masaburi, mgombea ubunge wa Kivule, Nchimbi amesema: “Kivule kwamba chaguo lililopo hapa ni chaguo sahihi, mkawaambie ambao hawapo hapa, kwamba mgombea mwenza ametwambia katika mtu anayeweza kufikisha kero zetu ni Ojambi Masaburi.

Huyu Ojambi, baba yake mzazi (Didas Masaburi) alikuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam na alikuwa rafiki yangu, anaweza kuja kwa baba yake na mimi nikampeleka kwa shangazi yake Mama Samia haraka,” amesema.

Awali, Silaa amesema katika kipindi cha miaka minne na miezi sita ya Rais Samia madarakani, amefanya mambo mengi na makubwa ambayo kila mtu anayaona.

Amesema mwaka 2020, Jimbo la Ukonga lililokuwa na kata 13, miongoni mwa changamoto kubwa ilikuwa ni foleni kubwa, mfano kutoka Gongo la Mboto hadi Kariakoo, ilikuwa ni saa tatu hadi nne.

Silaa amesema tuliahidi mkitupa fursa, tutajenga barabara ya mwendokasi na sasa barabara inakwenda kukamilika, ukija usiku utafikiri uko Ulaya na sasa kufika Kariakoo inaweza kuwa muda mfupi zaidi.

Waziri huyo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, amesema jimbo hilo lina kero ya barabara nyingi za ndani lakini fedha zimetolewa na wakandarasi wameanza kuzifanyia kazi: “Na katika ilani yetu, zipo barabara nyingi za DMDP…kazi kubwa imeahidiwa na inafanyika.”

Silaa amesema jimbo hilo lilikuwa na changamoto ya maji lakini kuna tenki kubwa limejengwa Bangulo ambalo ni kubwa na limesaidia kupunguza adha ya maji maeneo mbalimbali na wananchi wanasherekea matunda ya Serikali ya CCM.

Eneo la afya, Silaa amesema, katika kata 13 zote kuna vituo vya afya kikiwemo cha Mzinga ambacho ni cha ghorofa ni kama cha wilaya na hiyo ni kazi kubwa imefanyika.

“Ukonga ya 2020 na Ukonga ya 2025 imepata maendeleo makubwa, naomba ufikishe salama kwa Rais Samia kwa maendeleo aliyotuletea,” amesema.

Katika elimu, Silaa amesema shule zimejengwa, madarasa yamejengwa na wanafunzi wanaendelea kusoma katika mazingira mazuri.

Katibu wa Oganizesheni wa CCM, Issa Gavu Ussi amesema chama hicho kinatambua uwepo wa tatizo la ajira na ndiyo maana ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030 inaeleza jinsi ya kutatua ikiwemo kurasimisha biashara ndogondogo.

“Chama chetu kinao uwezo na kubeba jukumu hilo, chama chetu kina uwezo na uzoefu wa kuongoza, wachagueni wabunge, madiwani na Rais wetu, tunahitaji mafiga matatu ili kazi ifanyie vizuri,” amesema Gavu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda amesema kazi kubwa imefanyika.

“Sisi wanawake tutatoa kura za heshima kwa sababu chama kimetuheshimisha sana kwa kututeulia mgombea mwanamke ambaye naye ametuheshimisha kwa kazi kubwa aliyoifanya katika sekta mbalimbali,” amesema Chatanda.