Dk Mwinyi awaahidi wavuvi wadogo uvuvi wa bahari Kuu

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi ameahidi kuwa endapo atapata ridhaa ya kuongoza kwa muhula wa pili, serikali yake itaweka mkazo mkubwa katika kuwawezesha wavuvi wadogo kuvua bahari kuu ili kuongeza kipato chao na kukuza uchumi wa taifa.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Septemba 30, 2025, alipowatembelea wachuuzi, wavuvi na wajasiriamali katika soko la samaki la Malindi, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni zake.

Amesema sekta ya uvuvi ina nafasi kubwa katika kuinua maisha ya wananchi wa Zanzibar, hivyo serikali itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu, vifaa vya kisasa na mafunzo kwa wavuvi.

“Wavuvi walituambia wanataka maboti makubwa ili waweze kufika bahari kuu. Tumelipokea na tutalifanyia kazi ili tuwawezeshe kupata samaki wengi zaidi,” amesema.

Dk Mwinyi amesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya ajenda ya maendeleo ya uchumi wa buluu, ambao umekuwa kipaumbele katika uongozi wake wa awamu ya kwanza.

Ameongeza kuwa mwaka 2020 aliahidi kuwasaidia wavuvi, wakulima wa mwani na wajasiriamali na ahadi hizo zimetekelezwa kwa vitendo.

“Tumetoa maboti, vifaa vya kisasa kama fish finder, nyavu na zana nyingine, na takwimu zinaonyesha upatikanaji wa samaki umeongezeka. Tutazidi kuwasaidia ili kuongeza kipato chao,” amesema.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kujenga masoko na madiko katika Unguja na Pemba, sambamba na kuwawezesha wajasiriamali kupata mitaji na maeneo mazuri ya kufanyia shughuli zao.

Dk Mwinyi amewaomba wananchi kumpa kura pamoja na wagombea wengine wa CCM ili kuendeleza mipango ya maendeleo ya nchi kwa kipindi cha 2025 hadi 2030.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Dimwa amesema safari ya chama hicho katika miaka mitano iliyopita imejikita katika kuwawezesha wajasiriamali na kuimarisha mazingira ya biashara.

“Tumetekeleza kwa vitendo. Sasa tumeanza safari nyingine kuomba ridhaa ya wananchi ili serikali ya CCM iendelee kuwaletea maendeleo,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Banda la Papa Malindi, Nia Juma Mbwana ameibua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara sokoni hapo ikiwamo uchakavu wa banda lenye zaidi ya miaka 10, uhaba wa vyoo na upungufu wa huduma za maji safi.

Amemuomba Dk Mwinyi kushughulikia matatizo hayo na kuwasaidia kupata mikopo ili kukuza biashara zao.

“Sekta ya uvuvi na biashara ya samaki inaweza kuchangia zaidi kukuza uchumi wa Zanzibar. Tuna imani kubwa na wewe, na kura zetu zote Oktoba 29 ni za CCM,” amesema.