Musoma. Mgombea urais kupitia Chama cha Democratic (DP), Abdul Mluya amesema kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, hatua yake ya kwanza itakuwa kufunga mipaka ya nchi ili kuwazuia waliopo ndani wasitoroke, kwa lengo la kuwachukulia hatua mafisadi waliotafuna fedha za walipa kodi.
Hata hivyo, Mluya hakufafanua jinsi atakavyowachukulia hatua mafisadi, ila alisema mipaka ikifungwa, watakaozuiwa ni waliomo nchini huku walio nje wakiruhusiwa kuingia kama kawaida.
Mluya ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 30, 2025 kwenye mkutano wa kampeni ambapo amesema ufisadi umesbabisha Watanzania kuishi maisha magumu licha ya kuwepo kwa rasilimali nyingi nchini.
“Wana Mara na Watanzania kwa ujumla mnaoneka mnaishi kwa bahati na kuzaliwa kwenu ni laana, rasilimali zetu tulizopewa na Mungu zimegeuzwa na wachache na kuonekana kama laana kwetu hili halitakubalika kwa Serikali ya DP, lazima itambulike kuwa rasilimali tulizopewa na Mungu ni baraka na neema kwetu,” amesema.
Amesema watu wa kwanza atakaoshughulika nao wakati mipaka ya nchi ikiwa imefungwa ni pamoja na wale waliohusika kuruhusu uingizwaji wa nyavu zisizokidhi viwango na kusababisha wananchi wengi hasa wavuvi kuwa masikini baada ya kunyang’anywa nyavu hizo na kuchomwa moto.
“Nyavu zinaingizwa kupitia bandari na zinatozwa kodi, wananchi wananunua na kisha wanakuja watu kuwanyang’anya na kuzichoma moto swali la kujiuliza ilikuwaje Serikali ijiingizie kipato kupitia nyavu hizi halafu wananchi wasio na hatia watiwe umasikini,” amehoji.
Amesema wakati wa kuwashughulikia mafisadi Serikali yake haitajali cheo alichokuwa nacho mtu hata kama alikuwa Rais, Waziri Mkuu ama kiongozi yeyote atashughulikiwa.
Mluya amesema kuwa akipewa ridhaa ya kuwa Rais, Serikali yake itaondoa Uwanja wa Ndege wa Musoma kwa kuwa upo katikati ya mji na unahatarisha usalama wa wananchi, badala yake eneo hilo litajengwa chuo kikuu ili kutoa fursa kwa wakazi wa Mara kupata elimu ya juu.
Amesema Serikali yake itajenga uwanja wa kisasa nje kidogo ya mji utakaotumika kuimarisha uchumi wa mkoa na kuodoa changamoto za usafiri kwa wakazi hao.
Kuhusu kikokotoo, Mluya amesema Serikali yake itafuta kikokotoo na kwamba mbadala wa kikokotoo ni kuboresha maisha na maslahi ya watumishi wa umma kabla ya kustaafu.
Amefafanua kila mtumishi wa umma atakopeshwa nyumba bora na ya kisasa mkopo ambao utakatwa kweye mshahara wake wakati wa utumishi wake, hali ambayo amesema itawaondolea adha wanayokutana nayo wastaafu kutokana na uwepo wa kikotoo.
“Watumishi wa umma sisi tutahakikisha wanafanya kazi kwa starehe kwa kuwaboreshea maslahi yao na hii itaongeza morali kwenye kazi, hivyo watafanya kazi zao kwa weledi na ubora wa hali ya juu.
Amesema suala la uboreshaji wa huduma za kijamii litapewa kipaumbele na Serikali yake huku akisema hivi sasa upatikanaji wa huduma za kijamii zinapatikana kwa kusuasua licha ya uwepo wa miundombinu ikiwepo majengo.
“Mfano tunaambiwa mahospitali yamejengwa, lakini ukweli ni kuwa tuna majengo na sio hospitali kwani huduma kule haziridhishi, nichagueni nikaboreshe huduma ili wananchi wa kawaida wenzangu mpate huduma bora za viwango,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa DP Tanzania bara, Chrisant Nyakitita chama chake ndicho chama kinara kwa kudai mabadiliko ya katiba ambapo amesema madai hayo yalisababisha chama hicho kukosa usajili wa kudumu kwa zaidi ya miaka tisa huku viongozi wake wakikamatwa na kufungwa jela kwa kudai mabadiliko.
“Mabadiliko ya katiba kama wanavyodai wengine tulianza siku nyingi hali iliyosababisha chama kukosa usajili wa kudumu huku mwanzilishi wake marehemu Christopher Mtikila akikamatwa zaidi ya mara 40 na kufungwa miaka miwili, hivyo mwanzilisji wa mabadiliko ya katiba ni DP,” amesema Nyakitita
Amesema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa kupiga kura ni haki yao ya kikatiba, inayowapa fursa ya kumchagua kiongozi bora kupitia sera na ilani za vyama vya siasa.
“Mimi sina shaka na ilani na sera zetu sisi ni bora kuliko vyama vingine, hivyo msifanye makosa jitokezeni kwa wingi mkakipigie chama hiki kura ili tuelete mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwa nchi yetu,” amesema.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa DP Mkoa wa Mara, Bagaile Konjo, amewaomba Watanzania wakichague chama hicho ili kiweze kuleta maendeleo nchini.
“Nchi ina matatizo, wananchi wana matatizo na hata mgombea wetu ana matatizo yanayofanana na ya kwenu na kama chama chetu kinavyosema saa ya ukombozi ni sasa kwa hiyo msifanye makosa mkachague diwani, mbunge na rais anayetokana na chama chetu,” amesema.