Dodoma. Chama Cha United People’s Democratic Party (UPDP) kimetangaza kubadiri neno hukumu za mahakamani kuwa tuzo ili kila mhalifu apate haki yake.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Septemba 30, 2025 na mgombea urais wa chama hicho Twalibu Kadege wakati akinadi sera zake katika stendi ya daladala soko la majengo jijini Dodoma.
Katika mkutano huo, Kadege amesema hakuna namna nyingine yoyote zaidi ya kuwakamata watu wanaovunja sheria lazima wapate alichokiita tuzo.
Amesema kila mtenda kazi anastahili haki yake na ndivyo itakavyokuwa kwa wahalifu kupewa tuzo wanayostahili hata kama ni miaka 50.
“Hatutaongoza Serikali ya watu wabadhirifu na wavunja sheria, tutashughulika na kila mtu bila kumuonea aibu wala hadhi yake, tuzo itatembea kwa kila mtu ili kuweka hali ya utulivu,” amesema Kadege.
Mgombea huyo amewataka mahakimu kwamba lazima wawe watenda haki katika Serikali atakayoiongoza na itakuwa aibu na fedheha hakimu kutoa hukumu halafu mtu akate rufaa na kushinda.
Amesema hukumu ya haki ndiyo itakuwa kipimo cha hakimu aliyesomeshwa kwa fedha nyingi, lakini akikatiwa rufaa katika kesi yake halafu mtuhumiwa ashinde, atambue haitakuwa na kazi tena maana itaonyesha alikosea kumhukumu mtu.
Kadege amesema ilani ya UPDP inataja namna watakavyotenganisha maeneo ya wakulima na wafugaji ili kila mmoja asimfuate mwenzake na kama itatokea mmoja kwenda kwa mwingine vyombo husika vitamkamata mara Moja na kumpatia tuzo hata kama ni miaka 50 jela na kulipa kiwango cha uharibifu uliotokea.
Mbali na hilo, kila raia ambaye ardhi anayomiliki ikikutwa kuwa na rasilimali kama madini, hataondoka hapo badala yake atakubaliana na mwekezaji kwa asilimia watakazokubaliana bila kuingiliwa na Serikali na wakina mama kuanzia siku atakayoapishwa wataanza kupewa mkopo wa Sh5 milioni ili kuwaondoa kwenye kausha damu.
Katika hatua nyingine amewataka wakuu wa mikoa kuwa makini katika kuwatumia watu ili waikwepe tuzo ya mahakama.
“Wengine ni wale tutakaowasomesha nje ya nchi, lazima mtu akimaliza arudi nchini kuja kuwatumikia Watanzania, akikataa tunamfuata na kumnyang’anya cheti kisha anashtakiwa mahakamani ili kuwa fundisho kwenye matumizi ya rasilimali za nchi zisitumiwe kizembe.
Kuhusu watumishi amesema wataishi kama walio peponi kwani Serikali yake itaanza kwa malipo ya mshahara wa Sh2.8 milioni wakati madaktari watalipwa sawa na wenzao wanavyolipwa Marekani na uwezo huo upo.
Kuhusu kauli za wagombea majukwaani amewaomba vyombo vya ulinzi kuwakamata na kuwazuia wasifanye kampeni kwani katika Baraza la Vyama vya Siasa hawakukubaliana hilo badala yake kila mgombea anatakiwa kunadi sera siyo vinginevyo.