Ukichambua ahadi na ilani za wagombea urais na vyama, kilimo ni eneo limezingatiwa kwa mkazo mkubwa. Hiyo inaleta mwangaza kwamba wanasiasa wana ufahamu wa kutosha kuhusu sekta mkombozi wa taifa.
Hamad Rashid Mohamed, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Alliance for Democratic Change (ADC), ajenda yake kubwa kwa Wazanzibari ni kilimo.
Hamad anasema kuwa, Wazanzibari wakimchagua awe Rais, atahakikisha anawaongoza vizuri na kuondoa tatizo la uhaba wa chakula. Anaahidi kwamba Zanzibar, chini ya uongozi wake, haitaagiza chakula kutoka nje, zaidi, yenyewe ndiyo itakayokuwa inauza kwa sababu itazalisha hadi kutengeneza ziada. Hilo, Hamad anaamini, litafanikiwa endapo wakulima watawezeshwa.
Kipaumbele chake kikubwa ni kilimo cha mpunga. Hamad anasema kuwa, wakulima wa Zanzibar wakiwezeshwa na ardhi ya kilimo ikitumika ipasavyo, mchele utapatikana kwa wingi, ambao utawatosheleza Wazanzibari na mwingine utauzwa nje ya Zanzibar. Hesabu za Hamad ni kuwafanya wakulima wa Zanzibar waendeshe kilimo cha biashara ili kupata matokeo ambayo anayakusudia.
Hamad anasema kuwa, ardhi inayofaa kwa kilimo cha mpunga Zanzibar ni hekta 10,000. Anafafanua kuwa wakulima 30,000 wakiwezeshwa vema, wakalima kisasa ndani ya ardhi hiyo, mpunga utapatikana kwa wingi, na mchele utakaopatikana kupitia mpunga huo utatosheleza walaji wote wa Zanzibar, na kutakuwa na ziada ya kutosha ambayo itauzwa nje ya visiwa hivyo. Hamad anaamini kuwa wakulima 30,000 peke yake wanatosha kuifanya Zanzibar kuwa muuzaji wa mchele nje ya nchi.
“Hekta moja ya mpunga iliyomwagiliwa maji kwa kutumia utaalamu ina uwezo wa kuzalisha tani tatu mpaka tano za mpunga ambazo ni sawa na mchele kilo 1,500 (tani moja na nusu).
“Kwa hiyo sasa, hekta 10,000 zilizopo Zanzibar, kama wakulima 30,000 wakitengenezwa vizuri, Zanzibar itajitegemea kwa chakula na itauza hata nchi nyingine,” anasema Hamad.
Hamad Rashid Mohamed, au HRM, ni mwanahistoria wa siasa za mageuzi Tanzania. Alikuwa mmoja wa waasisi wa Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 1992. Alishiriki kuanzisha CUF ikiwa ni miaka minne baada ya kufukuzwa Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1988. Kwa CCM ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Hamad alitafsiriwa kama mmoja wa wakaidi wa mfumo, ambao ilionekana ni lazima watimuliwe.
Kwa mtazamo, Hamad si aina ya viongozi wenye mihemko wala papara. Ni mtulivu anapojenga hoja, lakini ana misimamo mikali anaposhikilia lake. Bila shaka, msimamo huo ndiyo uliomwondoa CCM, ukamfanya awe CUF. Akiwa CUF, akawa mfungwa wa kisiasa kati ya mwaka 1997 mpaka 2001 kwa kesi ya uhaini.
Mwaka 2015, baada ya kuwa CUF kwa miaka 23, alilazimika kukiacha chama hicho na kuanzisha Alliance for Democratic Change (ADC), baada ya mgogoro wake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki dunia Februari 17, 2021.
Hamad alipishana na Seif katika eneo la ujenzi wa chama. Alitaka fedha za ruzuku zitumike vizuri kukijenga chama, kisha akataka awe Katibu Mkuu wa CUF ili atekeleze vizuri kazi ya ujenzi wa chama, kwa sababu wakati huo Seif alikuwa pia Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, hivyo alimuona hatimizi vizuri majukumu ya ukatibu mkuu. Alitaka apumzike kwenye eneo hilo.
Kama ilivyokuwa mwaka 2015 na 2020, Hamad ndiye anayepeperusha bendera ya ADC katika mbio za urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025. Mwaka 2015 na 2020, aligombea na hakutikisa, tofauti na ukubwa wake wa kisiasa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya marudio ya uchaguzi Zanzibar mwaka 2016, Hamad aliteuliwa na Mwenyekiti wa saba wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, kuwa Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi. Mwaka 2018, Shein alimbadilisha Hamad wizara na kumhamishia Wizara ya Afya, ambayo aliihudumia mpaka muhula ulipofikia tamati Novemba 2020.
Hamad ni mtaalamu wa fedha. Ajira yake ya kwanza ilikuwa mwaka 1972, alipoajiriwa na Benki ya Watu wa Zanzibar kama karani, na baadaye kupanda cheo hadi kuwa msimamizi wa benki mwaka 1973, kisha meneja msaidizi wa Benki ya Watu, Tawi la Chakechake, Pemba kati ya mwaka 1973 mpaka 1976. Mwaka 1976 mpaka 1977, alikuwa meneja wa Benki ya Watu, Tawi la Wete Pemba.
Mwaka 1978 mpaka 1982, Hamad aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Nje wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Mwaka 1979 mpaka 1982, Hamad alikuwa pia mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro. Mwaka 1979 mpaka 1982, Hamad alikuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Muungano Tanzania.
Kwa mara ya kwanza, Hamad alichaguliwa kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, akiwakilisha lililokuwa jimbo la Mkoa wa Kusini, Pemba. Alidumu kwenye ubunge mpaka mwaka 1988 alipotimuliwa uanachama wa CCM.
Mwaka 1982, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alidumu kwenye nafasi hiyo mpaka mwaka 1987 alipohamishiwa Wizara ya Fedha na Uchumi kama Naibu Waziri. Mwaka 1988, akiwa na mwaka mmoja Wizara ya Fedha, alivuliwa uanachama wa CCM.
Kabla ya kufukuzwa CCM, Hamad pia aliihudumia Zanzibar kama mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, vilevile mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Kati ya mwaka 1982 mpaka 1988, Hamad alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa CCM (NEC).
Mwaka 2001, baada ya kuachiwa huru katika kesi ya uhaini, aliteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa mbunge. Mwaka 2005, alishinda ubunge jimbo la Wawi, Pemba. Alishinda tena jimbo hilo mwaka 2010. Hamad alikuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni mwaka 2005 mpaka 2010. Mwaka 2015, aligombea urais wa Zanzibar..
Hamad ana uzoefu wa kuongoza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kipindi cha Serikali ya chama kimoja na wakati wa vyama vingi. Amehudumia karibu mabunge yote kikanda na duniani kwa nyakati tofauti.
Alizaliwa Machi mosi, 1950, Wawi, Chakechake, Pemba. Alisoma Shule ya Msingi Chakechake Wavulana mwaka 1958 mpaka 1968. Sekondari alisoma Fidel Castro, Pemba mwaka 1969 mpaka 1971. Mwaka 1979, alitunukiwa stashahada ya Sayansi ya Siasa, Chuo cha Itikadi cha Kivukoni, Zanzibar. Ana diploma nyingine ya Stadi za Maendeleo ya Jamii, aliyotunukiwa mwaka 1981 na Chuo Kikuu cha Francis Xavier, Canada.
Ana cheti cha Mafanikio ya Uongozi, alichotunukiwa na Chuo Kikuu cha Pyongyang, kilichopo Korea Kaskazini. Ana stashahada ya Umahiri wa Uongozi, aliyofuzu Chuo cha Stadi za Uongozi, London, Uingereza. Ana shahada ya uzamili ya Usimamizi wa Miradi, Chuo Kikuu cha Salford, Uingereza, aliyosoma kati ya mwaka 2014 na 2018.
Hamad anasifiwa kuwa alifanya vizuri kwenye Baraza la Mapinduzi chini ya Dk Shein kati ya mwaka 2016 – 2020.
Hamad anaahidi, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, ni kuchagiza mapinduzi ya elimu, kwamba itatolewa kidigitali na hakutakuwa na matumizi ya karatasi shuleni.
Wazanzibari wanamfahamu Hamad. Ni mmoja wa alama za mageuzi, lakini pia mpigania demokrasia tangu Tanzania ikiwa chini ya mfumo wa chama kimoja. Hamad ni aina ya wanasiasa ambao hawahitaji utambulisho mkubwa Zanzibar. Kingine, Hamad ni mmoja wa wanasiasa wachache kutoka Zanzibar ambao haiba zao zilipenya Tanzania Bara, tena kwa heshima kubwa.