:::::::
BEI ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mwezi Oktoba 2025 zimeendelea kushuka ambapo bei za rejareja za petroli zimepungua kwa sh. 55, dizeli sh 50 ikiwa ni muendelezo wa kupungua kwa bei za bidhaa hizo .
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dk James Mwainyekule, kupungua kwa bei hizo kumetokana na kupungua kwa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa wastani wa 5.10% huku gharama za kuagiza mafuta ya petroli kwa bandari ya Dar es Salaam zikipungua kwa wastani wa 1.95% .
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya mafuta yaliyopokelea bandari ya Dar es Salaam, imepungua kutoka sh 2,807 hadi 2,752 kwa petroli, na kutoka sh. 2,754 hadi sh. 2,704 kwa dizeli huku bei ya mafuta ya taa ikisalia kuwa sh. 2,774 kama ilivyokuwa Septemba 2025.
Kwa mafuta ya petroli yaliyopokelewa katika Bandari ya Tanga, bei ya rejareja nayo imepungua kutoka sh. 2,868 hadi sh. 2,813, dizeli kutoka sh 2,816 hadi sh. 2, 766 na bei ya mafuta ya taa ikisalia kuwa sh. 2,835 kama ilivyokuwa kwa mwezi uliopita.
Kwa mafuta yanayopokelewa Bandari ya Mtwara, bei ya petroli imepungua kutoka sh. 2,899 hadi sh. 2,844, na dizeli kutoka 2,847 hadi 2,797 huku bei ya mafuta ya taa ikisalia sh 2, 866 kama ilivyokuwa Septemba 2025.
Mwisho.