Zoezi la ufungaji taa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam limekamilika jana Septemba 30, 2025.
Kukamilika kwa uwekaji taa hizo kunafanya sasa Uwanja huo uwe tayari kwa kutumika kwa mechi za usiku za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine.
Na mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa usiku itakuwa kesho baina ya wenyeji JKT Tanzania na Azam FC ambayo itaanza saa 12:00 jioni.
Kabla ya mechi hiyo, leo kuna mchezo wa majaribio ya taa hizo uwanjani hapa ambao unakutanisha timu za vijana chini ya umri wa miaka 20 za JKT Tanzania na Azam FC.
Kufungwa kwa taa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kunafanya sasa kuwepo viwanja vinavyoweza kuchezeka mechi za usiku viwe sita nchini.
Viwanja hivyo ni Azam Complex, Mkwakwani, Meja Jenerali Isamuhyo, Benjamin Mkapa, Jamhuri Dodoma na Majaliwa.
Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ni miongoni mwa viwanja vilivyoteuliwa kutumika kwa mazoezi katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Fainali hizo za AFCON 2026 zitafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zikishirikisha timu za taifa 24.
Pia ulitumika kwa mazoezi katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN) 2024.