MSHAMBULIAJI wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma amesema kitendo cha makocha kujifunza mbinu mpya kila wakati, kumeleta mabadiliko ya mpira wa miguu kuchezwa kisasa zaidi.
Aliitaja ni kati ya sababu ya kila msimu Ligi Kuu kuonekana ngumu na yenye ushindani, lakini mchezaji anayetamani kufika mbali kufanya bidii ya mazoezi na kutunza kiwango.
“Kadri miaka inavyokwenda ndivyo mabadiliko ya mpira wa miguu yanavyoonekana, kama mchezaji nafurahia mbinu zao zininanipa uhuru wa kuonyesha kucheza kwa kujiachia.
“Timu zinapokutana zote zinatumia ufundi na mbinu, lazima mashabiki watafurahia kuona burudani ya mechi pia inawasaidia wachezaji kuonyesha vipaji vyao,” amesema Juma.
Amesema tofauti na zamani ambapo kwa asilimia kubwa katika mechi ilikuwa inatumika nguvu, lakini kwa sasa akili kubwa, ufundi na mbinu za makocha ndizo zinazoamua matokeo.
“Fiziki ilikuwa inazingatiwa zaidi, ila kwa sasa unaona wachezaji wanatumia akili kubwa wakicheza baadhi yao unaweza ukaona mpira wa miguu ni mwepesi kumbe sivyo,” amesema Juma aliyemaliza msimu uliyopita na bao moja, huku akitamani itokee avunje kuifikia rekodi ama kuivunja ya mabao 13 aliyofunga msimu wa 2016/17.