KVZ yaanza mbwembwe, yautaka ubingwa Ligi Kuu

BAADA ya msimu wa 2024-2025, KVZ kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), kocha wa timu hiyo, Ali Khalid amesema safari hii ni zamu yao kuwa mabingwa.

KVZ iliukosa ubingwa huo kwa tofauti ya mabao 23 dhidi ya Mlandege iliyomaliza kinara zote zikiwa na pointi 62. Mlandege ilifunga mabao 67 na kuruhusu 21, wakati KVZ ikifunga 35 na kuruhusu 12.

Kati ya timu za vikosi zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar ambazo hazijawahi kubeba ubingwa wa ligi hiyo, KVZ ni mojawapo tangu kuanza kwa ligi hiyo mwaka 1984. Nyingine ni Kipanga na Uhamiaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Khalid amesema timu kukosa ubingwa imekuwa pasua kichwa upande wao ingawa msimu uliopita imefanikiwa kufika hadi nafasi ya pili.

KV 01


Amesema kosa lililotokea msimu uliopita ambalo limewagharimu ni kutoa sare michezo 11 raundi za mwanzoni, lakini msimu huu wamejipanga kusawazisha hilo mapema na ana imani kufikia hilo kutokana na kikosi alichonacho.

“Kwa sajili ambazo tumezifanya tuna imani na kikosi chetu kutwaa ubingwa lakini kawaida ya mpira unabaki dakika 90 za uwanjani ambazo zitaamua ubora,” amesema Khalid.

Kocha huyo amesema, mkakati wa msimu huu ni kupata mabao na matokeo mazuri kila mechi kwani hawawezi kuwa mabingwa endapo hawajajiandaa kushinda mechi hizo.

Akizungumzia mechi ya raundi ya kwanza ya ZPL kati ya KVZ na JKU itakayochezwa Oktoba Mosi 2025 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja, saa 10:15 jioni, kocha huyo amesema haitakuwa rahisi kwani kila mmoja anahitaji alama tatu muhimu kuanza vyema msimu huu.

KV 02


“JKU ni timu bora lakini KVZ ni bora zaidi, tutahakikisha tunakuwa na nidhamu ya mchezo na kuvuna pointi tatu, hakuna jambo lingine zaidi ya hilo,” amesema. Wachezaji ambao wamesajiliwa msimu huu na timu hiyo ni Abdul Halim, Raphael Lucas, Razack Shekimweri, Kassim Gatuso, Muhsin Suleiman, Ramadhan Kiparamoto, Emanuel Chacha na Hassan Babu.

Waliotoka ni Saleh Machupa, Suleiman Abrahman, Matias Julian, Mukrim Julian, Mukrim Madai na Abdul Hamahama.