NIKWAMBIE MAMA: Waumbueni wanasiasa wenye njaa

Pesa huwa haitangazwi bali inajitangaza. Mtu yeyote anayeranda barabarani kwa majigambo kuwa na pesa, huwa hana kabisa au anazo za kawaida. Watu wenye pesa za kufurika hujificha kwani zinawakera.

Katika nchi kama ya kwetu, utaamshwa kila alfajiri na ndugu, jamaa, majirani na wengine usiowajua. Kila mmoja atakuwa na mahitaji anayoamini kuwa wewe una uwezo wa kuyakidhi.

Lakini hata ukizificha, pesa zinajitangaza mbele za watu bila mwenyewe kutegemea. Yupo mzee aliyekwenda kujificha kijijini baada ya kushindwa maisha ya kitajiri. Alishinda bahati nasibu ya mabilioni, akawa anakesha na kudamka na shida za watu. Nadhiri ilikuwa ikimsuta pale alipokataa kumpa masikini hela ya unga wakati mbwa wake wanakula vyakula ghali.

Kule kijijini alimkataza bintiye mdogo kusema ukweli juu ya utajiri wao. Waliishi kimasikini hadi watu wakawachukulia hivyo. Lakini siku moja binti alikutana na hoja darasani: “Elezea misha ya familia masikini”.

Mwalimu alimchagua yeye kuanzisha mjadala huo. Binti aliongea pointi zilizomshangaza kila mmoja; “Masikini hawana nyumba za ghorofa, tena magari yao ni ya kizamani…”

Hivyo ndivyo fedha zinapojitangaza. Kinyume chake mtu anayejisifu kuwa na utajiri mwingi, anaweza kuumbuliwa pale umasikini wake utakapojitangaza.

Mtu mwingine alijigamba kukinai kuku aliokuwa akiwala kila siku. Siku hiyohiyo alichafukwa na tumbo, akatapika maharagwe hadharani. Alipoulizwa kulikoni yale maharagwe. Akadai “kuku wapo huku chini ya kitovu…”

Hiyo nayo ni njia ya umasikini kujitangaza. Kwenye maandalizi ya kampeni za uchaguzi, mgombea mmoja wa urais kutoka kambi ya upinzani aliushangaza umma. Msimu huu wagombea wote wa urais walikabidhiwa magari kwa ajili ya kampeni zao. Sasa mgombea huyu aliishangilia gari ile hadi akapitiliza.

Ni kama vile gari ilimsahaulisha kuwa alikuja kuchuana na wengine, tena hasa yule wa chama tawala. Alijikuta akimpigia dua kiongozi aliye madarakani aendelee kutawala, na kwamba wao wapinzani watasubiri mpaka baada ya mtawala kumaliza muda.

Watu wakajiuliza kama gari la kampeni tu limeweza kumchanganya mgombea kiasi hicho, je akikabidhiwa nchi itakuwaje? Maana nchini hakuna magari pekee, kuna raslimali kama maliasili, migodi na kadhalika. Huyu si atakufa kabla ya kuapa?

Kuna tofauti kubwa ya uwezo wa kifedha kwa vyama vinavyogombea kushika dola. Chama tawala kinajieleza wazi kwenye matukio ya kampeni zake.

Wana maandalizi mazuri, wanasafiri wakiwa na misafara mikubwa hadi vitongojini, wana uwezo wa kuwagharamia waandishi wao pamoja na wale wa kujitegemea, pamoja na kuyarusha matangazo yote katika vipindi maalum. Mwisho, wagombea wake hawana njaa.

Kwa hali hiyo, baadhi ya wapinzani wanaonesha kujipendekeza ili kupata hisani ya chama tawala. Tunaweza kuyaona haya kwenye baadhi ya vituko katika kampeni. Kwa mfano yule mgombea wa urais kupitia upinzani alipomwombea dua mgombea wa CCM ashinde. Hii inaonesha wazi kuwa baina yao kuna tofauti kubwa sana. Kutoshikamana kwao kunaweza kuleta matokeo ya kupingana wao kwa wao.

Lakini hayo si kwa wagombea tu, wapo viongozi na wanachama wanaojizima data na kujilipua wakati wa kampeni za wenzao. Tunashuhudia kila kukicha, wanachama wa upinzani wakitaliki vyama vyao na kwenda “kuunga mkono jitihada za mama”.

Imekuwaje katika kipindi hiki ndio wanayaona mazuri ya chama tawala, na si wakati mwingine wowote? Tena basi si ofisini, ila kwenye majukwaa ya kampeni.

Iwapo Chama cha Mapinduzi kinahitaji viongozi makini, kiachane na viongozi wenye hulka za bendera kufuata upepo. Pengine hawa wameshtukiwa udhaifu wao kule walikotoka, sasa wanayahamishia magonjwa yao kwenye kambi mpya.

Wengine wana nia ya kusafisha nyota ili kama si kuteuliwa, wabaki kuokota mabaki chini ya meza za wakubwa.

Nao hawana tofauti na wale wanaobembeleza kupewa kitu kidogo ili walipuke.

Watu wa aina hii ni hatari kubwa kwa taasisi iliyojipanga. Ieleweke kuwa mfuko haujawahi kutosheka na hela, wala tumbo kutosheka na chakula.

Ndio maana mfanyabiashara anayemiliki viwanda bado anauza pipi na biskuti za rejareja. Wanachama hao wanaotangatanga wasipopata nafasi walizotarajia, wanaweza kurubuniwa tena kwa vijisenti na kufanya umamluki unaoweza kusababisha nyufa kwenye chama husika.

Kujilipua kwenye majukwaa ya kampeni za mahasimu kunatoa taswira ya kuomba rushwa. Pamoja na kwamba wakubwa wana uwezo wa kutoa msaada wa kuwainua wadogo, na kwamba kumsaidia asiyejiweza kunapelekea thawabu kwa mtoaji, lakini kumpa rushwa masikini ni dhambi.

Mtoaji na mpokeaji wa mlungula wote wana kipimo kilekile kwenye mzani wa sheria. Wapigakura wa sasa wana uelewa wa hali halisi ya nchi yao. Hawadanganyiki na mbwembwe za watu kuacha vyama vyao na kuhamia upande wa pili hasa nyakati za kampeni.

Wanajua kuwa hiyo ni mbinu ya wanaodhani ni ujanja kufunga hesabu kila uchaguzi ulipopita.

Ingawaje si dhambi kukihama chama, lakini hakuna mwanamume anayepeleka posa wakati mwali anaolewa na mume mwingine.