JKCI YAONGEZA SIKU ZA UPIMAJI BURE WA MOYO KUFUATIA MWITIKIO MKUBWA

 


::::::::::;

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam

Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza kupima afya ya moyo, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeongeza siku mbili zaidi za upimaji wa bure, hatua inayolenga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma hiyo muhimu.

Upimaji huo ulioanza katika Hospitali ya Dar Group jijini Dar es Salaam ulikuwa umepangwa kufanyika kwa siku moja tu, lakini idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza imeilazimu taasisi hiyo kuongeza muda ili kutoa nafasi kwa watu wengine zaidi kupima afya zao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema zaidi ya watu 230 walihudumiwa siku ya kwanza pekee, hali inayoonesha mwamko mkubwa wa wananchi katika kujali afya ya moyo.

“Kwa siku ya leo pekee tumewahudumia watu 232. Ili kufanikisha dhamira yetu ya kuelimisha na kuzuia magonjwa ya moyo, tumeongeza siku mbili za upimaji. Tunataka wananchi wengi zaidi wapate huduma hizi,” alisema Dkt. Kisenge.

Aidha, Dkt. Kisenge alifafanua kuwa takwimu za kiafya zinaonyesha kuwa kila mwaka watoto wapatao 10,000 huzaliwa nchini wakiwa na matatizo ya moyo, huku zaidi ya 4,000 kati yao wakihitaji upasuaji wa haraka ili kunusuru maisha yao.

Kwa upande wa watu wazima, alieleza kuwa sababu kubwa zinazochangia matatizo ya moyo ni pamoja na ulaji usiozingatia lishe bora, kutokufanya mazoezi, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi pamoja na magonjwa nyemelezi kama kisukari na shinikizo la damu.

Katika kuendeleza juhudi za utoaji wa huduma kwa wananchi, JKCI inaendesha kampeni ya kitaifa ijulikanayo kama Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services, ambayo tayari imewafikia watu zaidi ya 23,000 katika mikoa 23 nchini.

“Tunaendelea na huduma za tiba mkoba ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu, upimaji na matibabu ya moyo. Tunawahimiza wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kujikinga na magonjwa haya,” alisema Dkt. Kisenge.

Naye Mkurugenzi wa JKCI–Dar Group, Dkt. Tulizo Shemu alieleza kuwa gharama za matibabu ya moyo ni kubwa, hivyo ni muhimu kwa wananchi kufanya vipimo mara kwa mara ili kubaini matatizo mapema.

“Kuzibua mshipa wa moyo hugharimu zaidi ya Sh milioni 6. Vifaa kama ‘pacemaker’ vya kusaidia umeme wa moyo vinaweza kugharimu hadi Sh milioni 10. Njia rahisi ni kujikinga kabla ya matatizo kuwa makubwa,” alisema Dkt. Shemu.

Huduma hizo za upimaji bure zinaendelea kutolewa kwa siku mbili zaidi katika Hospitali ya Dar Group, na wananchi wote wanahimizwa kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo za kitabibu.