TPHPA INAVYOSAIDIA WAKULIMA KUDHIBITI WADUDU WAHARIBIFU WA MAZAO .

Na Mwandishi Wetu , Gairo

WAKULIMA mkoani Morogoro wanaendelea kunufaika na mafunzo muhimu yanayotolewa na wataalamu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kuhusu  mbinu bora na sahihi za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao mashambani ili kuongeza tija.

Mtaalam wa Mamlaka hiyo, Clemence Kivuyo ameyasema hayo mbele ya mkuu wa mkoa wa Songwe, Jabir Makame ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Gairo na muasisi wa Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo yanayoingia  msimu wa nne 2025.

Makame alipewa heshima ya kuzindua maonesho  ya msimu wa nne  yaliyofanyika katika kijiji  na kata ya Leshata , wilayani Gairo  yakilenga  kuhamasisha “kilimo biashara chenye tija na endelevu” yatafikia kilele Oktoba 4, 2025.

Mkuu wa mkoa huyo alipata fursa ya kulitembelea banda la Mamlaka hiyo na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wakulima.

Kivuyo amesema ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na tatizo la viwavijeshi  vyenye uharibifu wa mazao , Mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu ya utambuzi wa wadudu na hatua za uharibifu kwa wakulima.

Amesema Mamlaka hiyo pia imekuwa ikitoa viuatilifu vyenye ruzuku vilivyotolewa na Serikali kwa ajili ya udhibiti wa wadudu ambapo wakulima hutoa taarifa  kwa Mamlaka kupitia halmashauri za wilaya.

“ Baada ya kupitia utaratibu huu zoezi la kudhibiti kwa kutumia viuatilifu hufanywa na Wataalam kutoka Mamlaka  katika mashamba ya Wakulima  na kuongeza tija ya kilimo’ amesema Kivuyo. 

Kivuyo amesema Mamlaka hiyo inaendelea kuwahamasisha wananchi na wadau wa kilimo kutembelea banda lake ili kupata elimu na huduma za kitaalamu kwa maendeleo endelevu ya kilimo nchini.

Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Gairo wakiwemo wa kata ya Leshata  wakati wa uzinduzi huo ,Makame , amesema Serikali inatambua  mchango wa  kilimo kuwa ni njia pekee ambayo inaweza kumuinua mwanachi kiuchumi.

Makame amesema Serikali imeweka njia mbalimbali za kumuinua mkulima ikiwa ni pamoja na kutoa  ruzuku mbalimbali katika pembejeo za kilimo, chanjo, mbegu na mbolea.

 “ Hatuna budi kumshukuru mheshimiwa  Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi mahiri aliyebeba wakulima kupitia ruzuku hizi  na kufanya sekta ya kilimo kuwa sekta yenye tija katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minne” amesema Makame.

Mkuu wa mkoa wa Songwe amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Gairo kwa kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuunganisha wadau wa kilimo na wakulima na kupeana elimu ya namna bora ya kufanya kilimo chenye tija ili kumkwamua mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.

Mtaalam wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ,Clemence Kivuyo (mwenye kuvaa jaketi) akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa wa Songwe, Jabir Makame ( watatu kushoto) ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Gairo na muasisi wa Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo yanayoingia  msimu wa nne 2025 kuhusu utoaji wa  mafunzo kuhusu  mbinu bora na sahihi za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao mashambani ili kuongeza tija kwa wakulima.Mkuu wa mkoa wa Songwe, Jabir Makame ( kulia) ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Gairo na muasisi wa Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo yanayoingia  msimu wa nne 2025 akisililiza maelezo ya mtaalamu wa  Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ,Clemence Kivuyo juu ya utoaji mafunzo kuhusu  mbinu bora na sahihi za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao ili kuongeza tija kwa wakulima.

Wananchi wa kata ya Leshata, wilayani Gairo  mkoa wa Morogoro akiangalia teknolojia mbalimbali za kisasa za udhibiti wa za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao ili kuongeza tija kwa wakulima zilizopo katika banda la   Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwenye Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo yanayoingia msimu wa nne 2025  ( Picha na Mwandishi Wetu).