“NDIYO, yule alikuwa anaitwa Thomas Christopher, ni mtoto wa aliyekuwa tajiri yake Unyeke.”
Nikaona pale palikuwa na habari nzito. Nikamuuliza yule mzee:
“Inaelekea wewe unajua mambo mengi kuhusu huyu Thomas na kuhusu Unyeke…”
“Nilikuwa dereva wa Unyeke. Na huyu Thomas alikuwa mtoto aliyekuwa akimlea pale nyumbani. Hakuwa amemzaa mwenyewe.”
“Unyeke unayemzungumzia wewe ni Unyeke yupi? Mimi namfahamu Rama au Lazaro Unyeke. Pia namfahamu Frenk Unyeke…”
“Hao unaowataja ni watoto wa huyo Unyeke mwenyewe. Unyeke mwenyewe alishakufa.”
“Unafahamu kwamba hao watoto wa Unyeke walipata kesi ya mauaji?”
“Nafahamu na pia nilitoa ushahidi wangu mahakamani. Wao ndio waliomuua Thomas.”
“Ni kisa kirefu. Walimuua ili wapate mali aliyokuwa akimiliki baba yao.”
Nikaona niende na yule mzee vilevile ili nipate kile alichokuwa anakijua.
“Baba yao alikuwa akimiliki mali gani?” nikamuuliza.
“Unajua, Unyeke hakuwa na mali yoyote. Alikuwa masikini ohe ahe, isipokuwa alikuwa rafiki wa baba yake Thomas. Huyo rafiki yake alikuwa akiitwa Christopher. Christopher ndiye aliyekuwa tajiri.”
“Ndiyo,” nikamuitikia mzee huyo kwa namna ya kumhimiza aendelee kunieleza.
“Christopher alikuwa Mnyasa aliyetoka Songea miaka mingi iliyopita. Alipofika hapa Tanga rafiki yake wa kwanza alikuwa Unyeke. Christopher alianza kazi ya kuuza magazeti mitaani. Baadaye akajiingiza katika biashara ya madini. Biashara hii ndiyo iliyomfanikisha na kumtoa katika umasikini.”
“Christopher akaanza kununua majumba na magari, akaoa mke na akamzaa mtoto. Alizaa mtoto mmoja tu. Mke wake akaja kufariki kwa ajali ya gari. Ikabidi mtoto wake alelewe na yaya. Kumbe wakati wote kansa ilikuwa inamla Christopher kwenye ini bila mwenyewe kujua.
“Ghafla akaanza kuumwa. Aliwahi kulazwa hospitalini kwa muda mrefu akitibiwa. Wakati huo alimuachia mamlaka ya mali zake rafiki yake Unyeke.
“Alipopata nafuu na kutoka hospitali aliendelea kushirikiana na Unyeke katika kazi zake. Walishirikiana na Unyeke kwa karibu miaka mitatu.
“Ule mwaka wa tatu madaktari walimwambia Christopher kuwa amebakisha miezi mitatu tu ya kuishi kwani ini lake lilikuwa limeshaharibika. Christopher hakuwa na ndugu na mtoto wake alikuwa bado mdogo. Akamuita rafiki yake Unyeke na kumwambia kwamba madaktari wamemwambia umri wake wa kuishi kabla ya kufa ni miezi mitatu. Kwa hiyo alikwenda naye kwa wakili kumuandikishia mali zake pamoja na mtoto wake.
“Katika mkataba wao waliounda kwa wakili, ni kwamba Unyeke amlee Thomas mpaka atakapofikisha umri wa miaka kumi na minane, kisha amkabidhi mali ile na yeye Unyeke awe msaidizi wake. Unanisikiliza vizuri?”
“Ndiyo, nakusikiliza.”
“Kweli, baada ya miezi mitatu na wiki mbili Christopher akafa. Ikabidi Unyeke arithi mali ya Christopher pamoja na kumlea Thomas. Lakini wakati huo Unyeke naye alikuwa na watoto wake wanne ambao aliwalea pamoja na Thomas.
“Hao watoto walikuwa wakijiona kama ndugu tu na walikuwa wakubwa kuliko Thomas. Thomas alipofikisha umri wa miaka 19 ndipo Unyeke alipowapa wanawe ile siri kwamba ile mali waliyokuwa wakiiona si yake yeye, bali ni urithi wa Thomas kutoka kwa baba yake aliyefariki dunia, na kwamba anajiandaa kumkabidhi mali yake. Kitendo hicho hakikuwafurahisha wale wanawe.
“Wakawa na njama za kumuua mwenzao. Siku moja walimchukua kwenye gari kwenda matembezi kumbe ndiyo siku waliyopanga kumuua. Wakaenda naye shambani, wakamnyonga kisha wakamzika huko huko.
“Yule wakili ambaye alikuwa na ule mkataba wa Christopher na Unyeke alikuwa akiwatembelea pale nyumbani mara kwa mara. Baada ya Thomas kupotea, yule wakili ndiye aliyetoa ripoti polisi.
“Katika uchunguzi wao polisi walimhoji mtumishi wa ndani nyumbani kwa Unyeke ambaye alisema siku ya mwisho alimuona Thomas akiondoka na wenzake, lakini waliporudi Thomas hawakuwa naye.
“Wale vijana wakaanza kukamatwa. Kwanza alikamatwa mmoja. Baada ya kuhojiwa na kuteswa akatoa ile siri. Polisi wakaenda pale mahali walipomzika, wakamfukua na kuondoka naye. Baada ya uchunguzi wao, yule kijana alikwenda kuzikwa pale Chuda.
“Unyeke alipopata habari kwamba wanawe wamemuua mwenzao na mmoja ameshakamatwa, akapata presha akafa pale pale.
“Wale vijana waliendelea kusakwa na kukamatwa mmoja mmoja. Kila aliyekamatwa alipelekwa mahakamani kushitakiwa kwa mauaji.
“Wa kwanza alihukumiwa kunyongwa. Alihukumiwa bila wenzake. Wenzake wawili wakahukumiwa pamoja, na yule aliyekamatwa mwisho alihukumiwa peke yake kwa sababu wenzake walikuwa wameshahukumiwa.
“Ile mali, kwa sababu haikuwa na mwenyewe, ilichukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na nyumba ya Chuda walipokuwa wanaishi. Nasikia serikali iliuza mali zote.”
“Mzee, nakushukuru umenisaidia sana kwa maelezo yako. Sasa nitakutambulisha mimi ni nani na kwa nini nilikuwa nakutafuta.”
Nikajitambulisha kwa yule mzee na kumueleza kuhusu tukio la kuachiwa kwa kina Unyeke na mkuu wa gereza, na badala yake kunyongwa wafungwa wengine kwa kutumia majina yao.
Mzee alishangaa sana aliposikia kisa hicho. Nikaendelea kumueleza kuhusu kunyongwa kwa kina Unyeke waliokuwa uraiani wakiwa wamebadili majina.
“Uchunguzi wetu unaonesha kuwa aliyewanyonga ni huyo huyo Thomas Christopher. Jambo hilo ndilo linaumiza akili zetu,” nikamwambia yule mzee.
Mzee huyo alishtuka kidogo akanitolea macho ya mshangao.
“Umenichanganya kidogo,” akaniambia na kuniuliza:
“Umeniambia huyo marehemu Thomas ndiye aliyewanyonga hao vijana?”
“Ndio, uchunguzi wetu unavyoonesha.”
“Huyo kijana si alishauawa?”
“Ndiyo, alishauawa kama ambavyo umenielezea lakini tunashangaa kuona yeye ndiye muuaji wa hao vijana.”
Nikamueleza kuhusu zile alama zake za dole gumba zilizopo kwenye karatasi tulizozikuta kwenye shingo za watu walionyongwa. Kadhalika, nikamueleza kuhusu ujumbe alionitumia kunijulisha kuwa ameshamaliza kazi na amerudi kaburini.
Mzee akatikisa kichwa. Sikuweza kujua alitikisa kichwa kusikitika au kuonesha kuwa jambo hilo haliwezekani.
“Umenieleza jambo la ajabu sana kwamba mfu ameua watu waliomuua kisha amerudi kaburini!”
“Na hiyo namba ya simu ni ya marehemu. Tumethibitisha kutoka kampuni ya simu. Namba ina jina la Thomas Christopher.”
Mzee aliendelea kutikisa kichwa.
“Kwa maoni yangu hicho kitu hakiwezekani, labda kwa miujiza. Mtu aliyekwisha kufa hawezi kurudi tena duniani.”
“Tutaendelea kuchunguza tupate ukweli, lakini nashukuru kwa historia uliyonipa.”
Nikainuka na kutia mkono kwenye mfuko wa suruali yangu na kutoa pochi yangu ya pesa. Nilitoa noti mbili za shilingi elfu kumi kumi nikampa.
“Mzee wangu, chukua hizi pesa zitakusaidia kununua kitu utakachopenda,” nikamwambia.
Mzee alizipokea pesa hizo na kunishukuru.
“Nitakapohitaji tena maelezo yako nitakufuata.”
“Asante sana. Karibu, na ninakukaribisha kwa mara nyingine tena. Utakapohitaji kuja kwangu usisite, njoo tu.”
Nikamuaga na kuondoka. Wakati narudi kituo cha polisi nilijiambia kuwa kwa kukutana na mzee yule nimeweza kupata mwanga kuhusu kuuawa kwa Thomas na pia kuhusu kesi iliyokuwa inawakabili kina Unyeke.
Muda ule nilikuwa nimeweza kujua Thomas alikuwa akiishi pamoja na kina Unyeke baada ya baba yake mzazi kufariki dunia na akakabidhiwa kwa mzee Unyeke.
Laiti kama Thomas angekuwa hai ningeweza kusema kwamba kunyongwa kwa vijana wa Unyeke kunatokana na kisasi. Lakini Thomas mwenyewe ndiye aliyetangulia kuuawa, na mwili wake tumeukuta kaburini.
Lakini dole gumba la marehemu tumelikuta na rangi ya bluu ambayo ilikuwa ikitumika kuweka alama ya dole hilo kwenye karatasi walizokuwa wanawekewa kina Unyeke waliponyongwa.
Hilo ndilo tatizo la uchunguzi huu.
Tunamchunguza mtu aliyekwishakufa lakini athari ya vitendo vyake inaendelea kuwepo duniani kama vile bado yuko hai.
Nilikwenda kwa afisa upelelezi ambaye nilimkuta ofisini. Nikamueleza habari niliyoipata kwa mzee Abuu wa Makorora.
Afisa wangu alipoupata undani wa kisa cha kuuawa kwa Thomas aliniambia:
“Kumbe hawa watu walikuwa wamoja!”
“Walikuwa wamoja lakini kwa sababu ya tamaa ya kupata mali wasiyostahili kuipata wakamuua mwenzao.”
“Sasa kitendawili cha kina Unyeke kuwa hai tumeshakitegua, bado kitendawili cha Thomas.”
“Kina Unyeke hatukuwakuta makaburini, lakini Thomas tumemkuta! Kina Unyeke waliachiwa kijanja, lakini Thomas amekufa kweli. Sasa nini kimetokea?”
“Unajua, bila juhudi tusingekitegua kitendawili hicho cha awali. Tungekiacha kiporo tu. Sasa juhudi zinahitajika tena kwa kitendawili hiki cha pili. Kazi bado iko kwako. Wewe ndiye utakayekitegua.”
Sikumjibu kitu afande wangu. Nilibaki kumtazama kwa macho makavu. Kimoyomoyo nilikuwa nikijiambia:
“Kazi ninayo.”
Sasa nikiwa ndani ya gari nikielekea ofisini kwangu, simu yangu ikaita. Nikaichukua na kuitazama skrini. Nikaona Hamisa ndiye aliyekuwa akinipigia simu.
Nikashituka kidogo.
“Hamisa ananipigia simu, kulikoni?” nikajiuliza.