ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ametaja vitu vitatu anavyoviona ndani ya kikosi hicho vinayoweza kuipa urahisi kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Fadlu ambaye kwa sasa anaifundisha Raja Casablanca ya Morocco baada ya kuondoka Simba hivi karibuni, amesema anaamini timu hiyo aliyoifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, inaweza kuvuka kikwazo kilichopo mbele yake dhidi ya Nsingizini Hotspurs na kucheza hatua ya makundi kutokana na nidhamu ya mazoezi iliyopo, ubora wa kikosi na ari ya ushindani.

“Nilifanya kazi na wachezaji hawa, nawajua vizuri. Wana kiwango cha juu, nidhamu ya mazoezi na ari kubwa ya ushindani. Wakidumisha msimamo huo, hakuna kinachoweza kuwazuia kufika hatua ya makundi,” amesema Fadlu.
Simba imetinga hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitupa nje Gaborone United ya Botswana kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1. Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Botswana, Fadlu ndiye aliyekuwa kwenye benchi na akaiongoza Simba kushinda bao 1-0.

Baada ya kuondoka, kikosi kilimalizia mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa chini ya kocha wa muda, Hemed Suleiman ‘Morocco’ na kutoka sare ya bao 1-1.
“Ni lazima nitoe pongezi kwa wachezaji wangu wa zamani. Walipambana vilivyo na kuonyesha Simba bado ni timu kubwa barani Afrika. Hatua ya kufika raundi ya pili ni mwanzo mzuri na naamini wanaweza kupenya zaidi hadi hatua ya makundi,” amesema Fadlu.

Simba chini ya Fadlu iliandika historia kubwa baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini ikapoteza mbele ya RS Berkane kwa jumla ya mabao 3-1.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa wekundu hao wa Msimbazi kufika fainali katika historia ya michuano ya CAF baada ya miaka 32.

Katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Simba ilimaliza nafasi ya pili kwa alama 78, nne nyuma ya Yanga iliyotwaa ubingwa.
Kikosi hicho chini ya Fadlu kilipata ushindi kwenye mechi 25, sare tatu na kupoteza mbili tu ambazo ni dhidi ya Yanga.
Kwa sasa, Simba inakabiliwa na kibarua kingine kigumu dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini na iwapo itafanikiwa kuvuka hapo, itafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Simba itaanzia ugenini kukabiliana na wapinzani wake hao kati ya Oktoba 17 na 19, 2025, kisha marudiano jijini Dar es Salaam kati ya Oktoba 24 na 26, 2025.