Viongozi wa Serikali Mufindi wapewa mbinu kukabili moto msituni, mashamba

Iringa. Viongozi wa Serikali za mitaa Wilaya ya Mufindi wametakiwa kuimarisha juhudi za kudhibiti matukio ya mioto ili kuondokana na athari zinazojitokeza kila mwaka katika maeneo ya misitu na mashamba.

‎Wito huo umetolewa  Septemba 30, 2025 katika ukumbi wa mikutano uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, katika semina maalumu iliyowakutanisha viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo.

‎Mhifadhi Tebby amesema matukio ya moto hutokea kwa sura tofauti na mara nyingi huathiri siyo tu mali za serikali, bali pia raslimali na maisha ya wananchi wa maeneo jirani.

‎“Wananchi hupata hasara kubwa pale moto unapoteketeza mashamba yao, nyumba au mali nyingine. Ni wajibu wa viongozi kusimamia kikamilifu mikakati ya udhibiti,” amesema Mhifadhi Tebby.

‎Akizungumzia vifaa vya kuzimia moto, alisema kuwa kwa sasa kuna changamoto lakini bajeti zijazo zitatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.

‎Hata hivyo, Mhifadhi Tebby aliwahimiza wananchi kutumia matawi ya miti kuzima moto kwa dharura kwani ni njia rahisi na yenye msaada mkubwa.

‎Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mashaka Mfaume amesema kuwa viongozi ni nguzo muhimu katika kusimamia mikakati ya udhibiti wa moto.

‎Ofisa Tarafa wa Wilaya ya Mufindi, Robert Kileo amesema kuwa elimu ya kudhibiti moto itasaidia kupunguza uharibifu unaojitokeza kila mwaka katika shamba la Sao Hill na maeneo mengine.

‎Aidha, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Reuben Chongolo alieleza kuwa hatua ya kuandaa mikakati ya udhibiti wa moto ni mwanzo wa safari mpya ya kulinda mazingira.

‎“Huu ni uzinduzi wa mchakato endelevu wa kudhibiti mioto katika maeneo jirani na msitu wa Sao Hill hivyo tunataka viongozi wawe mstari wa mbele,” alisema Chongolo.

‎Baada ya semina hiyo, imepangwa vijiji zaidi ya 25 vitapitiwa ili kufanya mikutano ya kutoa elimu ya kudhibiti moto kwa wananchi.

‎Viongozi hao wamekumbusha kuwa matukio ya moto hayaiathiri serikali pekee, bali jamii nzima inayozunguka maeneo hayo.

‎“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuchukua hatua. Tunanufaika na misitu hii ya Sao Hill, hivyo tunapaswa kuwa walinzi wake wa kwanza,” amesema Chongolo.

‎Viongozi walihimizwa kuwa chachu ya mabadiliko ya fikra za wananchi katika kulinda raslimali za taifa.

‎Katika kipindi hiki cha maandalizi ya usafishaji mashamba, wananchi wamekumbushwa kuwa waangalifu ili kuepuka kusababisha moto.

‎Pia, wananchi wametakiwa kuwekeza zaidi katika upandaji wa miti kwa wingi ili kuimarisha uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.

‎“Uchumi wa Wilaya ya Mufindi unategemea miti na hii ndiyo sekta muhimu ya ajira na upatikanaji wa malighafi viwandani,” amesema Chongolo.

‎Kwa mujibu wa viongozi, kuwekeza katika upandaji miti Chongolo amesema kwamba kutasaidia kuongeza bidhaa za mbao, ajira na mapato ya serikali.

‎Baadhi ya viongozi wa Serikali za mitaa kutoka halmashauri ya Wilaya ya Mufindi waliopata semina hiyo waliishukuru Serikali kwa elimu iliyotolewa na kushauri iendelee kushirikiana na jamii kikamilifu.

‎Yona Mkakazi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igowole halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, amesema kuwa Wananchi wapo tayari kushirikiana lakini ni vyema pia Sao Hill ikatenga muda wa kufanya mazoezi ya pamoja ya kuzima moto.

‎“Wananchi wanahitaji kuona vitendo. Tukifanya mazoezi ya kuzima moto kwa pamoja, watapata uzoefu na ujasiri wa kukabiliana na majanga hayo,” amesema Mkakazi.

‎Kwa sasa, jamii imeendelea kuhamasishwa kuwa walinzi wa kwanza wa mazingira kwa kutoa taarifa mapema endapo kuna viashiria vya moto.

‎Kwa ujumla, semina hiyo imeweka mwelekeo mpya wa kuhakikisha viongozi wa Mufindi wanashirikiana na wananchi katika udhibiti wa moto.