KILICHOTOKEA jana Septemba 30, 2035 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Yanga ikibanwa na Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara, wakubwa wengine hawataki kukiona kikiwatokea leo.
Katika kuukwepa mtego huo wa Yanga kudondosha pointi mapema, Simba na Azam leo Oktoba 1, 2025 zina vibarua kwenye viwanja tofauti ikiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara.
Simba tayari mechi ya kwanza imeshinda mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, huku Azam nayo ikiichapa Mbeya City mabao 2-0. Kila moja ina pointi tatu, wakati wapinzani wao, JKT Tanzania (4) na Namungo (4) zote zikishuka dimbani mara mbili.
Simba ipo nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuikaribisha Namungo, wakati Azam inaifuata JKT Tanzania, mechi ikichezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

“Tunarajia kuwa na mechi ngumu, kama mkiangalia rekodi, Namungo imekuwa ikitusumbua licha ya kuifunga mechi mbili za mwisho, wana kocha mzuri anayeijua Simba, tutaingia na tahadhari kubwa,” amesema Seleman Matola ambaye ni kocha msaidizi wa Simba.
Simba licha ya kufanya vizuri mechi zilizopita, kilio kikubwa kwao ni kutotumia vizuri nafasi ambapo akizungumzia changamoto hiyo, Matola aliyekabidhiwa kikosi hicho baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids, amesema: “Tunalijua hilo tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi shida imekuwa kuzimalizia, tumelifanyia kazi kwa kiwango kikubwa.”
Msimu uliopita, Simba iliipa Namungo kichapo cha mabao 3-0 kwenye mechi zote mbili nyumbani na ugenini, huku rekodi za jumla zikionyesha zimekutana mara 12 kwenye ligi.

Katika mechi hizo 12, Simba imeshinda saba na sare tano, huku Namungo ikiwa haijaonja ladha ya ushindi.
Ni mechi moja pekee ambayo Simba imetoka uwanjani bila bao dhidi ya Namungo, ilikuwa Julai 8, 2020, huku zingine 11 lazima Wekundu wa Msimbazi watikise nyavu.
Namungo imeuanza msimu kiaina ikiwa imeshacheza mechi mbili zote nyumbani ikianza na sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, kisha ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons na sasa inakwenda kucheza mchezo wa kwanza ugenini msimu huu.

Wauaji wa Kusini wanatakiwa kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Simba ikiongozwa na Jonathan Sowah ambaye baada ya kuuwasha moto msimu uliopita ameshaanza balaa lake akiwa tayari ana bao moja alilofunga kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate.

Presha pekee kwa Simba mbele ya Namungo ni wapinzani wao kuwa na kocha Juma Mgunda ambaye amewahi kuwafundisha wekundu hao mara mbili kwa vipindi viwili vya mpito.
Mgunda anaijua Simba, pia amefanya kazi na Matola ambaye anaiongoza timu hiyo kwa sasa.
Vijana wa Mgunda watatambia uwepo wa Wakongomani wawili kwenye safu yao ushambuliaji, Heritier Makambo na Fabrice na Ngoy.
Mgunda akizungumzia mechi hiyo, amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kushindana na Simba huku wakitarajia mchezo mgumu wakitambua wanakwenda kukutana na timu ngumu.
“Tuna siku tatu hapa mjini, tumejiandaa vizuri kuja kukutana na timu nzuri, yenye wachezaji wazuri, maandalizi yote tumeyafanya ili tufanye vizuri, tuhaiheshimu Simba tumekuja kushindana nao,” amesema Mgunda.

Kabla ya mechi hiyo itakayoanza saa 2:15 usiku, saa 12:00 jioni ni JKT Tanzania dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar.
Timu zote mbili zimeuanza msimu kibabe ambapo JKT baada ya sare ya bao 1-1 mbele ya Mashujaa, ikaenda kuichapa Coastal Union 2-1, zote ikiwa ugenini.
Azam ikiwa imeuanza msimu kwa moto ikifanya vizuri kimataifa lakini ikiwa imeshacheza mechi moja ya ligi ikiichapa Mbeya City mabao 2-0, sasa itakuwa ugenini kusaka pointi zingine tatu ili kufikisha sita.
JKT Tanzania ambayo ilianza msimu kwa kuongoza ligi, ikikaa juu ya msimamo, haijawahi kuwa ngumu mbele ya matajiri hao wa Chamazi na kwenye mechi 10 walizokutana Azam imeshinda saba huku ikitoa sare tatu.
Azam ikiwa chini ya Kocha Florent Ibenge, itaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kwani inakumbuka timu hizo zikiwa kwenye maandalizi ya msimu huu zilicheza mechi ya kirafiki na JKT ikashtua kwa kushinda 2-1.
JKT inatakiwa kujipanga kuwazuia kiungo wa Azam Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye tayari ana bao moja sambamba na washambuliaji Nassoro Saaduni na Jephté Kitambala Bola.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema licha ya kikosi chake kushinda ugenini bado kitakuwa na mchezo mgumu mbele ya Azam yenye kikosi kizuri na benchi kubwa la ufundi.
“Tunaijua Azam ni timu kubwa, ngumu wana wachezaji wazuri na benchi lenye makocha wakubwa, nikweli tumetoka kushinda ugenini lakini huwezi kuilinganisha Coastal Union na Azam, tutakwenda kuwa na mchezo mgumu,” amesema kocha huyo.
Azam safu yake ya ulinzi ambayo haijaruhusu bao tangu msimu uanze sio kimataifa wala ligi kuu, itatakiwa kuwachunga winga Saleh Karabaka ambaye tayari ana bao moja msimu huu na mshambuliaji wao wa zamani Paul Peter ambaye naye ana bao moja.
Akizungumzia mechi hiyo, Ibenge amesema wataingia uwanjani wakifahamu wanakutana na timu nzuri lakini watatafuta ushindi ili wachukue pointi zote tatu au moja.
“Tumejiandaa na mchezo mgumu, nimeiona JKT tulikutana nao sio timu rahisi, tuna kazi ya kuendeleza kucheza kwa ubora, tunachotakiwa kufanya kesho (leo) ni kushinda na kama sio kushinda basi tupate pointi moja,” amesema Ibenge.
Rekodi zinaonyesha JKT Tanzania na Azam zimekutana mara 10 kwenye Ligi Kuu Bara, Azam ikishinda mechi saba na sare tatu. JKT Tanzania haijaonja ushindi bado.