Wachezaji wa nafasi ya beki wameitwa kwa idadi kubwa kulinganisha na wa nafasi nyingine katika kikosi cha taimu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia, Oktoba 8 mwaka huu.
Katika kikosi kilichotangzwa jana, mabeki walioitwa ni 10, viungo saba, washambuliaji sita na makipa watatu.
Baada ya kukosekana kwa muda mrefu katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, kiungo wa Simba, Morice Abraham na nyota wengine nane wameitwa katika kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mechi ya mwisho zya kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia, Oktoba 8 mwaka huu.
Nyota hao nane ambao walikuwa nje ya kikosi cha Stars kwa muda mrefu ni Haji Mnoga, Miano Danilo, Offen Chikola,Habibu Khalid, Aziz Andabwile, Tarryn Allarakhia na Edwin Balua.

Kikosi hicho kimewaweka nje nyota watano waandamizi ambao ni Aishi Manula, Mbwana Samatta, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein na Saimon Msuva.
Beki majeruhi wa Simba, Abdulrazack Hamza naye amekosa uteuzi katika kikosi cha sasa ambacho pia kimemuweka kando kiungo Ahmed Pipino wa KMC.
Benchi la ufundi la Taifa Stars limeendelea kuwaamini makipa Yakoub Suleiman, Hussein Masalanga na Zuberi Foba na mabeki walioitwa ni Mwenda, Lusajo Mwaikenda, Mwamnyeto, Lameck Lawi, Miano Danilo, Haji Mnoga, Wilson Nangu, Dickson Job, Pascal Msindo, Ibrahim Abdulla na Novatus Dismas.

Viungo walioitwa ni Aziz Andabwile, Yahya Zayd, Yusuph Kagoma, Feisal Salum, Halid Habibu na washambuliaji ni Charles Mmombwa, Suleiman Mwalimu, Morice Abraham, Edwin Balua, Chikola, na Allarakhia.
Taifa Stars inahitajika kupata ushindi katika mchezo dhidi ya Zambia ili ifikishe pointi 13 na kujihakikishia nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E la kuwania kufuzu Kombe la Dunia linaloongozwa na Morocco.
Ikiwa itamaliza katika nafasi ya pili, Taifa Stars inaweza kupata nafasi nne za kucheza hatua ya mchujo kuwania tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo zitafanyika katika nchi za Canada, Mexico na Marekani.