Dar es Salaam. Katika hatua za kutanua wigo wa utoaji huduma kwenye sekta ya anga Shirika la Ndege la Taifa la Tanzania, (ATCL) limetangaza nafasi za ajira 173.
Shirika hilo linalomilikiwa na Serikali linatafuta marubani wapya, wahudumu wa ndege, na wafanyakazi wa ardhini kama sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano (2022/23–2026/27).
Mpango huo unalenga kupanua njia za safari na kudumisha mafanikio ya uendeshaji yaliyopatikana katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa tangazo la ajira lililotolewa na shirika hilo, nafasi zilizopo ni nahodha 23, marubani wasaidizi 45, wahudumu wa ndege 100 (ikiwemo 20 wanaozungumza kifaransa na kichina), mhasibu mmoja na wasaidizi wa mizigo wanne. Ambapo watakao chaguliwa kwenye ajira hizo wataajiriwa kwa mikataba ya miaka 10.
Ajira hizo zimetangazwa wakati ambapo ATCL inaendelea kuongeza nguvu zake kimataifa. Tayari shirika linafanya safari kwenda Guangzhou (China), Mumbai (India), na Dubai (Falme za Kiarabu), sambamba na mtandao wa safari za kikanda na ndani ya nchi.
Kuongezwa kwa ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner na Airbus A220-300 kumeimarisha uwezo wa shirika kushindana katika safari za masafa marefu na kuongeza faraja ya abiria.
Mtaalamu wa masuala ya anga na rubani wa zamani, Hassan Rweyemamu amesema mkakati huu wa upanuzi unahitaji kizazi kipya cha wafanyakazi wenye ujuzi ili kudumisha shughuli.
“Unaponunua ndege na kufungua njia mpya, hatua inayofuata ni kujenga wafanyakazi watakaoweza kulifanya shirika liendelee kushindana. Ajira hizi zinaonyesha kwamba ATCL iko makini na ukuaji wake siyo tu ndani ya nchi bali pia katika kuunganisha Tanzania na masoko makubwa ya kimataifa,” amesema Rweyemamu.
Kwa nini wahudumu wa ndege wanaozungumza Kifaransa na Kichina?
Miongoni mwa nafasi zilizotangazwa ni zile zinazohitaji wahudumu wa ndege wanaozungumza Kifaransa na Kichina.
Wataalamu wanasema hii inaonyesha dhamira ya ATCL katika kuongeza utofauti wa lugha na tamaduni kwenye huduma kwa wateja.
“Kifaransa ni muhimu kwa safari zinazolenga Afrika Magharibi na Kati, ambako lugha hiyo imesambaa sana, wakati Kichina ni la lazima kwa Guangzhou, ambayo imekuwa kituo muhimu kwa wafanyabiashara na wauzaji nje wa Kitanzania,” amesema Aneth Luhanga, mtaalamu wa masuala ya anga kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
“Abiria hujisikia vizuri zaidi pale wanapowasiliana kwa lugha zao. Hii si heshima tu bali ni mkakati wa kibiashara unaojenga imani na uaminifu,” aliongeza.
Nafasi kwa vijana wa Kitanzania
Kwa nafasi zaidi ya 170, ajira hizi pia zinaonesha nafasi ya ATCL kama mwajiri mkubwa katika sekta ya anga, sekta ambayo kwa muda mrefu imekuwa na changamoto ya wingi wa wahitimu wasiopata ajira.
Mchumi wa usafirishaji kutoka Mwanza, Julius Katabale amesena tangazo hilo limeleta matumaini kwa vijana wa Kitanzania wanaosomea fani za anga.
“Wahitimu wetu wengi wanamaliza masomo wakiwa na ujuzi wa kiwango cha dunia, lakini wanapata shida kupata ajira. Upanuzi wa ATCL unawapa nafasi na kuhakikisha kwamba taasisi kama NIT haziandai tu wahitimu kwa ajili ya masoko ya nje, bali pia kwa ukuaji wa ndani ya nchi,” amesema.
Aliongeza kuwa kujumuishwa kwa nafasi za mhasibu na wafanyakazi wa ardhini kunathibitisha kwamba “anga siyo suala la kuruka tu ni mfumo mzima unaotoa fursa katika taaluma mbalimbali.”
Urejeo wa ATCL katika miaka ya hivi karibuni umechochewa na uwekezaji mkubwa wa serikali katika ununuzi wa ndege na maboresho ya miundombinu, ikiwemo viwanja vya ndege nchini.
Wachambuzi wanasema kwamba zaidi ya usafiri, shirika hili pia ni bendera ya taifa la Tanzania nje ya nchi.
“Kadri shirika la taifa linavyokua, ndivyo linavyotangaza Tanzania kwa dunia,” amesema Katabale.
“Kila ndege ya ATCL inapowasili kwenye mji mkuu wa kigeni, haibebi tu abiria, bali pia inapeperusha utambulisho wa taifa. Upanuzi huu unamaanisha watalii zaidi, wawekezaji zaidi, na hadhi kubwa ya Tanzania kama mshiriki muhimu katika sekta ya anga,” aliongeza.
Kwa ajira mpya zilizotangazwa na safari mpya zinazotarajiwa, wadau wanaona hatua hii ya ATCL kama hatua muhimu ya kujikita zaidi katika soko la ushindani wa usafiri wa anga.
Kwa vijana wengi wanaotamani kuingia sekta ya anga, tangazo hili ni ishara ya mwanzo wa fursa mpya katika sekta ambayo mara nyingi huonekana ya kifahari na ngumu kufikika.
“Ajira katika sekta ya anga huleta manufaa yenye athari pana,” amesema Luhanga wa NIT.
“Inainua siyo mtu binafsi pekee, bali pia familia na uchumi mzima.”
Kadri ATCL inavyozidi kupanua mbawa zake, waajiriwa wapya wanatarajiwa kuwa nguzo kuu ya safari hiyo, kuhakikisha anga la Tanzania linaendelea kuwa wazi, lenye ushindani, na linalotambulika zaidi kimataifa.